Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maonyesho ya ajira Dar kutoa fursa 200

Dar es Salaam. Zaidi ya fursa 200 za ajira zinatarajiwa kutolewa kwa vijana wa Kitanzania kupitia msimu wa nne wa maonesho ya ajira ya China-Tanzania (Talent Job Fair), yanayotarajiwa kufanyika Juni 28 katika viwanja vya Maktaba Kuu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tukio hilo, Rais wa Chemba ya Biashara ya Makampuni ya Kichina nchini Tanzania, Janson Huang, alisema, “Kuanzia awamu ya kwanza hadi ya tatu, tumeona vijana wa Kitanzania wakikua na kustawi kupitia mashirika ya Kichina.”

Aliongeza kuwa toleo la mwaka huu linatarajiwa kupanuka zaidi kwa ukubwa na athari, likishirikisha takribani makampuni 100 kutoka China na ubia kati ya China na Tanzania.

Makampuni hayo yatatoa zaidi ya nafasi 200 za kazi katika sekta kama vile ujenzi, viwanda, vyombo vya habari, na huduma.

“Iwe wewe ni mhitimu wa chuo kikuu, mwanafunzi wa elimu ya ufundi, au mtaalamu chipukizi, msimu wa nne ni jukwaa hili linakufaa ili kujua mustakabali wa taaluma yako,” alisema Huang.

Alibainisha pia kuwa makampuni yanayoshiriki yanatafuta kuajiri vipaji vya ndani vyenye uelewa wa soko na ubunifu.

“Vijana wa Kitanzania wamekuwa wakituvutia kwa uwezo wao, wakileta mitazamo mipya katika biashara na kusaidia mchakato wa kuiweka katika mazingira ya ndani,” alisema.

Kwa mujibu wa Huang, makampuni ya Kichina hayatoi tu ajira bali yanatoa mafunzo ya stadi na mipango ya kukuza taaluma inayolenga kuwawezesha wataalamu wachanga kuwa viongozi.

Kwa upande wake, Mshauri wa Kiuchumi katika Ubalozi wa China nchini, Chu Kun, alisisitiza uimara wa uhusiano wa pande mbili kati ya Tanzania na China.

“Tanzania na China zinaendelea kushikamana kwa dhati katika masuala yanayohusu maslahi ya msingi na wasiwasi mkubwa,” alisema.

“Ushirikiano wetu wa kiuchumi na kibiashara umezaa matunda mengi, ukinufaisha wananchi wa pande zote mbili,” aliongeza.

Chu alieleza kuwa China imeendelea kuwa mshirika mkubwa zaidi wa biashara wa Tanzania, chanzo kikubwa cha uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni, na mkandarasi kiongozi katika miradi ya uhandisi kwa miaka kadhaa.

“Kampuni za Kichina zinashiriki kikamilifu katika miradi ya miundombinu nchini Tanzania ikiwemo barabara, reli, bandari, na umeme, na zimejikita katika kuchangia maendeleo ya kijamii ya Tanzania,” alisema.

Alibainisha kuwa kampuni hizo tayari zimezalisha zaidi ya ajira 150,000 na kusaidia kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wenye ujuzi.

“Juhudi hizi zimechangia kwa hali halisi katika safari ya Tanzania ya kujitegemea kimaendeleo na katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2050,” alisema Chu.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Zhang Xiaozhen, aliwataka vijana wa Kitanzania kuhudhuria maonesho ya ajira hayo na kuchunguza fursa zilizopo.

“Lengo hasa ni kuendeleza uhusiano mwema baina ya China na Vijana wa Afrika katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na fursa ya ajira,” alisema.

Aliongeza kuwa maonesho haya yanatoa jukwaa muhimu kwa ajili ya kujenga mitandao ya mawasiliano na makampuni ya Kichina kwa manufaa ya sasa na baadaye.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chemba ya wafanyabiashara wa Chini nchini, Juma Sharobaro, alisema kuwa maonesho hayo ya ajira ni ishara tosha ya ushirikiano imara kati ya sekta binafsi za China na Tanzania katika kuunda ajira na kuendeleza rasilimali watu.