Prime
Safari ya Ikomba urais CWT, anavyoitazama elimu nchini

Rais Mteule wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Suleiman Ikomba akizungumza na mwandishi wa makala haya, Hebel Chidawali 9hayupo pichani).
Muktasari:
Ni mtu anayetamani kila mtoto wa Kitanzania apewe nafasi ya kujifunza na kuonyesha kipaji chake, huku akichukizwa na walimu wazembe kazini.
Dodoma. Binadamu anaishi Kwa malengo,ndoto na wakati mwingine matamanio ya kufanya jambo jema lenye mafanikio kwa ajili yake, familia au taifa.
Kwenye malengo hayo, wako wanaoweka malengo ya muda mrefu,mfupi na muda wa kati lakini kwa ujumla ni kwamba yeyote anayeishi katika malengo hayo, atakuwa mtu mwenye kujituma na kufanya jambo kwa kiasi.
Hata hivyo, siyo kila mtu anaishi ama anafanya kile ambacho amelenga au alikusudia kukifanya kwani wengi wanaishi kulingana na mazingira ama nyakati zinazowasukuma wawe kama walivyo.
Kwa msemo wa kawaida mtaani, tunaishi tuwezavyo siyo kama tutakavyo kwakuwa tungeishi vike tutakavyo matajiri wangekuwa wengi na huenda utajiri wao ungeshuka, kwani kusingekuwa na wanunuzi wala walaji ambao ndiyo nguzo kuu kwa wenye mali.
Wako waliofanikiwa katika ndoto zao na wengine hawakufanikiwa kuzifikia ndoto, lakini upande wa pili wapo ambao wanaojua walishafika kwenye mafanikio licha ya kwamba walishakata tamaa kwamba huenda wasingeweza kuyafikia mafanikio.
Suleiman Ikomba ni miongoni mwa watu wanaoziishi ndoto zao, ni mmoja wa watu wa kupigiwa mfano kutokana na kuishi katika ndoto hata kuyafikia mafanikio.
Alianza kuishi katika ndoto ya kutamani awe mwalimu, aliishi katika malengo ya kufikia mafanikio katika kazi yake na bahati nzuri vyote amevipata, siri yake akisema ni uvumilivu na kutokata tamaa.
Huyu ndiye Ikomba, rais mteule wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) aliyechukua nafasi hiyo kutoka kwa mwanamke shupavu, Leah Ulaya ambaye waligombea katika kiti hicho wakiwa 18 lakini walimu wakasema ni zamu ya Ikomba.

Rais Mteule wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Suleiman Ikomba (Kulia) akizungumza na mwandishi wa makala haya, Hebel Chidawali.
Akiwa mzaliwa wa Igabilo katika Halmashauri ya Kigoma Ujiji, anasema alikuwa na ndoto ya ualimu tangu akiwa shule ya msingi na alipoipata, aliweka malengo ya mafanikio ikiwemo kuwa sauti ya wenzake ambapo alifanikiwa baada ya muda mfupi alipoteuliwa kuwa mwalimu mkuu hadi sasa.
Kibarua CWT
Ikomba anakiri kuna kazi kubwa ya kufanya ili kujenga imani kwa wanachama katika chama chao, kwani hata yeye anaona kuwa walimu wengi wamekata tamaa na ndio maana baadhi wameanza kukihama chama.
"Ni kweli chama kilianza kupoteza mwelekeo, tumekuwa na changamoto hiyo nami naingia nikilitambua hilo lakini lazima tuumize vichwa turudi kwenye mstari na kujenga umoja wetu ili uwe imara kama malengo yanavyotaka,"anasema.
Anaongeza: ‘’Kuna wakati tulijisahau na kutowasikiliza walimu nini wanachotaka, ndiyo maana wengi wakaanza kukimbia na kujiunga katika vyama vingine.’’
Akijibu swali kuwa CWT kimeacha kuwasemea walimu na kuwa sauti ya Serikali, Ikomba anaeleza: ‘’ Siyo kweli, sisi hatuwezi kuwa mdomo wa Serikali bali ni watumishi wa Serikali ambao tunafanya kazi kwa kushirikiana na Serikali. Unajua hilo swali limekuwa likiulizwa mara nyingi lakini niwaambie watu kwamba sisi tunafanya kazi chini ya Serikali kwa hiyo hatuwezi kuwa wanaharakati wa kupinga kila jambo.’’
Kuhusu masaibu wanayokumbana nayo walimu, ikomba anasema ndani ya uongozi wake, anapanga kuwawekea walimu mawakili kwa ngazi ya mkoa.
‘’Kama tutashindwa basi walau wakili mmoja kwa mikoa miwili ili wawe msaada kwa walimu, maana nimekutana na matatizo makubwa ya walimu wengi wanaonewa kwa sababu ya kukosa uelewa wa jinsi ya kueleza yaliyowasibu lakini wanajikuta wameingia kwenye hatia,’’ anaeleza.
Safari kielimu
Ikomba alisoma shule ya Msingi Igabilo huko Kigoma Ujiji na na kufanikiwa kwenda Shule ya Sekondari Ujiji kabla ya kujiunga na Chuo cha Ualimu cha Nachingwea ambapo alimaliza katika ngazi ya ualimu daraja tatu mwaka 1991.
Katika mazungumzo yake na Mwananchi, anasema baada ya ndoto yake ya kuwa mwalimu kutimia, ilimchukua muda mfupi lengo lake lingine kutimia, nalo ni kuwa mwalimu mkuu.
Akateuliwa kuwa mwalimu mkuu katika Shule ya Msingi Kakonko tangu alikodumu kwa miaka mitano kabla ya kupelekwa Shule ya Msingi Kagongo akiendelea na nafasi hiyo ya mwalimu mkuu na kwa sehemu kubwa huo ulikuwa mwanzo wa safari ya kuwasemea wenzake hadi sasa amekuwa sauti ya walimu nchini Tanzania.
Ahamia Dar es Salaam
"Mwaka 2000 niliondoka Kigoma kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya masoma katika Chuo cha Utumishi wa Umma Magogoni, huo ulikuwa mwanzo wa mimi kutokurudi tena katika mkoa niliozaliwa na nilianza kukubali mazingira wakati nikiwa chuoni,” anasema Ikomba.
Kwa mujibu wa maelezo yake, mara baada ya kuhitimu masomo yake alipangwa kufundisha Shule ya Msingi Yombodovya iliyopo Manispaa ya Temeke ambapo alidumu kipindi kifupi kabla ya kuteuliwa tena katika nafasi ya mwalimu mkuu, safari hii akiwa mwalimu mkuu wa kwanza na mwanzilishi wa Shule ya Msingi Mtoni Sabasaba.
Maisha ya Ikomba yakabaki Temeke lakini akihamahama kwa nafasi hiyo katika usimamizi wa Shule za msingi ikiwemo, Kingugi, Mtoni kwa Mama Mary, Minazini na kisha Shule ya Msingi Ali Hassan Mwinyi kote akiwa mwalimu mkuu.
Kwa nini ualimu?
"Binafsi nilipenda kazi hii tangu nikiwa mwananfunzi wa shule ya msingi, kwa namna fulani nilikuwa na uwezo binafsi shuleni, hivyo nikawa nawafundisha wenzangu kitendo kilichonivutia nikajiona kuwa naweza kuwa katika nafasi pana ya kuwakomboa watoto wa wanyonge wenzangu," anasema na kuongeza:
"..Hata walimu waliona kipaji kwangu wakanitia moyo kuwa ninafaa zaidi kuwa mwalimu na ndiyo maana nilipomaliza kidato cha nne, moja kwa moja nikasoma ualimu na nikaomba nipangwe kufundisha mkoani kwangu."
Kutokana na mapendo hayo, hata alipotaka kuoa alitafuta mke kutoka katika kundi la walimu, na katika watoto watatu aliojaaliwa, mmoja amelenga awe mwalimu hasa mtoto wa tatu anayesema amerithi kipaji chao.
Mafanikio
Anasifia kuwa kazi hiyo imempa mafanikio lakini kubwa kuliko yote ni jinsi alivyotimiza ndoto yake kwani anafanya kazi katika uumbaji wa akili ya mwanadamu na hilo aliliona tangu akiwa kijana mdogo akatamani.
Anajivunia kazi hiyo kumuinua na kumuunganisha na watu wengi kwani wapo wenye mafanikio makubwa waliopitia mikono yake jambo analosema ndoto na malengo kwake vimetimia kwa wakati mmoja.
Mafanikio makubwa ni kwa vijana waliopitia katika mikono yake ambapo anasema wako katika nafasi za juu kwenye utumishi na wengine wana mafanikio ya makubwa kwenye maisha yao ikiwemo kupata vipato katika uchumi.
Anavyoitazama elimu nchini
Ikomba anawashukia baadhi ya wazazi wanaowanyima nafasi za kusoma watoto wao hata kama wana uwezo.
Ikomba anasema kuna vipaji lukuki ambavyo vinafia majumbani na mitaani kwa sababu ya wazazi na jamii kutoona umuhimu wa kuwapeleka na kuwasimamia watoto wao kama inavyopaswa jambo analoliona kama adui kwa maendeleo katika sekta ya elimu.
Kuhusu walimu, kigogo huyo wa juu wa walimu nchini, anasema mtindo wa sasa wa kuwapata walimu kwa kupitia mtihani ni tishio kwa kada hiyo.
"Hiyo ni mbaya, mwalimu kafundishwa na kahitimu, umemuacha mtaani kauza miwa hata miaka mitano halafu unampa mtihani ndiyo apate ajira siyo jambo jema," anasisitiza.
Kwake anapendekeza wanaosoma ualimu wachujwe kidato cha nne na sita na waende wenye ufaule mkubwa, huku wakufunzi wao vyuoni wakiwa wale wenye uwezo ili wazalishe wahitimu wazuri.
Hata hivyo, Ikomba anaeleza kuwa ni adui na walimu wazembe na wasiojituma jambo alilopambana nalo wakati wote katika maeneo aliyopitia katika usimamizi akiwa mwalimu mkuu.
Mtalaa wa amali
Anasema anakubaliana na uamuzi wa Serikali katika kubuni mtalaa wa elimu ya amali, akieleza kuwa unakwenda kuwa mkombozi na suluhisho la ajira kwa vijana wanaomaliza masomo ya vyuo badala ya kutembea na bahasha wakiomba ajira.
Akitaja faida ya elimu hiyo ni namna ambavyo itatoa nafasi ya ujuzi wa aina yoyote kwa kila kijana ili ajue kitu cha kufanya hivyo akitoka shule au chuo anaweza kujishughulisha kwa jambo lolote la kumpatia kipato.
Hata hivyo, anashauri miundombinu kwenye shule na vyuo vinavyoanzishwa kupewa kipaumbele ili mahitaji kamili ya kujifunza na kufundishia yawepo ikiwemo walimu wenye sifa.
Nje ya majukumu ya kazi
Ikomba ni mume, baba wa watoto watatu, mlezi wa watoto kutoka familia za kipato cha chini na shabiki mkubwa wa timu ya Simba.
Ni muumini pia wa makambi ya kitaaluma kwa wanafunzi wenye madarasa ya mitihani na amekuwa akiishi na watoto wengi hata kutoka nje ya shule anayosimamia, ilimradi awasaidie kuvuka kwa kiwango cha juu katika mitihani ya kuhitimu.