Kilimo cha cocoa, korosho sasa kuwanufaisha Ulanga
Zao aina ya Cocoa likiwa shambani
Muktasari:
Haya yatakuwa ni mavuno ya kwanza ya mazao hao baada ya halmashauri hiyo kuweka mkakati wa kufufua zao la korosho na kuanzisha zao la cocoa ili kuyafanya mazao hayo kuwa mazao ya biashara yanayozalishwa na wilaya hiyo badala ya kutegemea mazao ya nafaka kwa chakula na biashara.
Morogoro.Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro inatarajia kuvuna zaidi ya tani 176 za mazao ya cocoa na korosho zenye thamani ya Sh361.2 milioni.
Haya yatakuwa ni mavuno ya kwanza ya mazao hao baada ya halmashauri hiyo kuweka mkakati wa kufufua zao la korosho na kuanzisha zao la cocoa ili kuyafanya mazao hayo kuwa mazao ya biashara yanayozalishwa na wilaya hiyo badala ya kutegemea mazao ya nafaka kwa chakula na biashara.
Kiasi hicho cha fedha kinatokana na mauzo ya wastani wa tani 100 za cocoa na tani 76 za korosho ambapo kwa bei ya soko, cocoa inauzwa kwa wastani wa Sh2,600 na Sh2,700 kwa kilo moja na korosho ni Sh1,200 kwa kilo.
Ofisa Kilimo, Mifugo na Ushirika wa Halmashauri ya Ulanga, Shehemba Kuziwa, alisema halmashauri ilianzisha kampeni ya kufufua zao la korosho na kuanzisha kilimo cha zao la cocoa kama mazao ya biashara ya wilaya hiyo mapema mwaka jana.
Kuziwa alidai kwa muda mrefu wakulima wa wilaya hiyo wamekuwa wakitegemea mazao ya chakula kama mazao ya biashara hali ambayo imewafanya wakulima wengi kushindwa kuneemeka na kilimo na kwamba kunzishwa rasmi kwa kilimo hicho kutaweza kuwaongezea kipato wakulima wa wilaya hiyo.
Ofisa kilimo, chakula na ushirika huyo alisema kuwa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2012/13, halmashauri hiyo iligawa bure wastani wa miche 42,944 ya cocoa kutoka katika vitalu ilivyovianzisha katika Tarafa za Vigoi, Mwaya, Lupiro, Malinyi na Mtimbira.
Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Furaha Lilongeri, amesema kuwa kampeni ya wilaya hiyo ya kilimo cha mazao hayo inakwenda vizuri huku yeye binafsi akiwa amepanda miche 1,600 ya cocoa.
Sliwashukuru wakazi wa Ulanga kwa kuitikia wito wa kuanza kilimo cha mazao hayo na kwamba ana imani wataendelea kunufaika kwa kipin di kirefu.