Prime
Bei ya kahawa inavyojikita kuchochea uzalishaji, soko
Muktasari:
- Kwa Tanzania, ongezeko hili linakuja wakati mwafaka ambapo uzalishaji wa kahawa unaongezeka kutoka kilo 50.53 milioni mwaka 2024/2025 hadi kilo 76.47 milioni.
Ongezeko la bei ya kahawa aina ya Arabica na Robusta katika soko la dunia linaendelea kufungua fursa mpya kwa nchi zinazozalisha zao hilo, ikiwamo Tanzania ambayo imekuwa ikiongeza uzalishaji wake katika miaka ya karibuni.
Bei za kahawa zimeonyesha ongezeko katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita mfululizo kutokana na mchanganyiko wa sababu mbalimbali zikiwamo mabadiliko ya tabianchi yaliyopunguza mavuno katika baadhi ya nchi wazalishaji wakubwa kama Brazil na Vietnam pamoja na ongezeko la mahitaji kutoka masoko ya kimataifa.
Takwimu za soko zinaonyesha Arabika bei yake iliongezeka kutoka Dola za Marekani 150 (Sh390,750) kwa kilo mwaka 2023/2024 hadi kufikia Dola 352 (Sh916,961) mwaka 2025/2026 huku kahawa ya robusta ikitoka dola 100 za Marekani (Sh260,500) hadi kufikia dola 218 za Marekani (Sh567,890).
Kwa Tanzania, ongezeko hili linakuja wakati mwafaka ambapo uzalishaji wa kahawa unaongezeka kutoka kilo 50.53 milioni mwaka 2024/2025 hadi kilo 76.47 milioni.
Taarifa ya utendaji iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mkuu Primus Kimaryo katika mkutano wa mwaka wa bodi hiyo inaitaja mikoa ya Ruvuma, Songwe, Arusha, Mbeya na Kilimanjaro kama wazalishaji wakubwa wa kahawa ya arabika.
Mikoa hii ilizalisha kilo 21.66 milioni, 17.44 milioni, 2.97 milioni, 2.63 milioni na kilo milioni 2.29 mtawalia.
“Ruvuma na Songwe zinabeba asilimia 77.4 ya uzalishaji wote wa Arabika nchini Tanzania kwa mwaka 2025/26. Hili linaonekana wakati ambao asilimia 92 ya kahawa yote katika mwaka 2025/2026 iliuzwa katika soko la moja kwa moja,” anasema.
Akizungumzia mikakati ya kuhakikisha Tanzania inanufaika zaidi na mwenendo mzuri wa bei za kahawa katika soko la dunia, Kimaryo anasema Serikali na wadau wa sekta hiyo wamejipanga kuimarisha ushindani wa kahawa ya Tanzania katika masoko ya kimataifa kupitia hatua mbalimbali.
Anasema moja ya vipaumbele ni kuimarisha nafasi ya kahawa ya Tanzania katika masoko ya asili ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakitambua ubora wa kahawa inayozalishwa nchini.
Sambamba na hilo, juhudi zinaendelea kufanyika kuhamasisha matumizi ya kahawa ndani ya nchi ili kuongeza soko la ndani na kupunguza utegemezi wa masoko ya nje pekee.
Kimaryo anasema mkakati mwingine ni kuongeza ubora wa kahawa katika hatua zote za uzalishaji na uchakataji ili kuhakikisha zao hilo linaendelea kukidhi mahitaji ya wanunuzi wa kimataifa na kupata bei nzuri zaidi katika soko la dunia.
Aidha, alisema Tanzania inaendelea kutafuta masoko mapya nje ya nchi ili kupanua wigo wa wanunuzi wa kahawa yake, hatua ambayo itasaidia kuongeza mauzo ya nje na mapato ya fedha za kigeni.
Pamoja na hilo, Serikali inaendelea kuboresha mfumo wa masoko ya kahawa kwa lengo la kuongeza uwazi, ufanisi na ushindani katika biashara ya zao hilo.
“Mikakati hii inalenga kuhakikisha wakulima, wafanyabiashara na wadau wengine wa sekta ya kahawa wanapata manufaa zaidi kutokana na ongezeko la uzalishaji na bei nzuri zinazoendelea kushuhudiwa katika soko la dunia,” alisema.
Akizungumzia namna Tanzania inavyoweza kunufaika zaidi na ongezeko la bei ya kahawa duniani, Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Tanzania, Profesa Aurelia Kamuzora anasema pamoja na kuongeza uzalishaji ni muhimu kwa nchi kuelekeza nguvu katika kuendeleza mnyororo mzima wa thamani wa zao hilo, hususan kwa kuwashirikisha vijana.
Anasema Bodi ya Kahawa imeanza mkakati wa kuwawezesha vijana kupata maarifa ya kina kuhusu sekta hiyo kwa kuanzisha programu za mafunzo zitakazowawezesha kuelewa fursa zilizopo kuanzia uzalishaji hadi uchakataji na masoko ya kahawa.
“Tunataka vijana wajifunze mnyororo wa thamani wa kahawa na kuufahamu vizuri ili waweze kushiriki kikamilifu, hasa katika eneo la uongezaji thamani. Tunaanza mkakati wa kuwafundisha kupitia taasisi za mafunzo ili waelewe kahawa ni nini hasa na fursa zinazopatikana baada ya hatua za uzalishaji, ikiwemo kukaanga na kusindika,” alisema.
Profesa Kamuzora anasema moja ya maeneo yenye fursa kubwa ni uzalishaji wa miche ya kahawa katika vitalu. Anaeleza kuwa Bodi ya Kahawa inatarajia kuisambaza miche hiyo kupitia vyama vya ushirika vya msingi (Amcos) zaidi ya 600 vilivyopo nchini, jambo litakalofungua nafasi za ajira na biashara kwa vijana.
“Kwa sasa mche mmoja unaweza kuuzwa kati ya Sh200 na Sh1,500 kutegemeana na aina na ubora wake. Hivyo, uzalishaji wa miche kwa wingi unaweza kuwa chanzo kikubwa cha kipato kwa vijana wakati huu ambapo mahitaji ya miche yanaongezeka,” alisema.
Aidha, anasema kilimo cha kahawa kinaendelea kuwa fursa muhimu ya kiuchumi kwa vijana kutokana na uwezo wake wa kuingiza mapato makubwa baada ya mimea kuanza kuzalisha, jambo ambalo kwa kawaida huchukua takribani miaka mitatu tangu kupandwa.
Anasema halmashauri zinapaswa kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya programu za Building a Better Tomorrow (BBT) ili kuwawezesha vijana kushiriki katika uzalishaji wa miche na kilimo cha kahawa.
Ametoa mfano wa Mkoa wa Kagera ambako vijana 300 wamewezeshwa kulima kahawa katika ekari 300, kila mmoja akimiliki ekari moja huku Serikali ikiwasaidia kwa huduma za umwagiliaji kupitia uchimbaji wa visima.
“Ekari moja inatosha kumpa mtu kipato na ajira katika utekelezaji wa shughuli zake.
Mbali na kilimo, kuna fursa nyingine kama kuanzisha migahawa ya kahawa ambayo inaweza kuwa maeneo ya biashara na mikutano,” anasema.
Pia alieleza kuwa maendeleo ya mafunzo ya kahawa nchini yameanza kuzaa matunda, akitolea mfano Chuo cha Ushirika Moshi ambapo vijana wanapata mafunzo ya kutambua ladha mbalimbali za kahawa.
Anasema hatua hiyo imeiwezesha Tanzania kupata wataalamu vijana wanaoweza kushiriki mashindano na maonesho ya kimataifa ya kuonja kahawa, huku wengine wakipata ajira katika kampuni mbalimbali zinazohusika na biashara ya zao hilo.
Serikali inafanya nini
Katika hotuba ya bajeti ya kilimo kwa mwaka 2026/2027 Wizara ya Kilimo iliyosomwa bungeni na Waziri Daniel Chongolo, alisemaTanzania imeweka lengo la kuzalisha tani 85,000.
Ili kufanikisha hilo imejizatiti kutoa mafunzo kuhusu kanuni za kilimo bora cha zao la kahawa na mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa wakulima 2,300 na maofisa ugani 217 kwenye maeneo ya uzalishaji sambamba na kuweka mfumo wa kusimamia uandaaji, usambazaji na utunzaji wa miche inayozalishwa.
“Ili kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa, Bodi ya Kahawa kwa kushirikiana na TARI itazalisha na kusambaza miche ya kahawa milioni 30. Vilevile, itawezesha uanzishaji wa mashamba mapya ya kahawa yenye ukubwa wa hekta 4,000 katika Halmashauri 54 zinazozalisha kahawa,” alisema Chongolo.