Malipo ya kidijitali kwenye mwendokasi, gym, vocha za kukwangua kuondolewa
Muktasari:
- Serikali pia kupitia Mamlaka ya TCRA itaondoa vocha za simu za kukwangua kwa mkono ikianza katika maeneo yote ya mijini.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeelekeza kuanzia mwaka 2026/27, malipo yote ya tozo, ushuru na nauli za mabasi ya mwendokasi, vivuko, madaraja, mabasi yaendayo masafa marefu, taksii mtandao, usafiri wa anga na reli pamoja na maeneo ya maegesho yafanyike kwa njia ya kidijitali.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omari wakati akiwasilisha bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/2027 leo Juni 11, 2026 bungeni jijini Dodoma.
Hatua hiyo inafuatia kuimarishwa kwa ufanisi wa mifumo ya malipo, kuongeza usalama pamoja na kuwezesha mwingiliano wa mifumo ya malipo ambapo katika kipindi cha mwaka 2025/26, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania imeboresha mfumo wa malipo ya papo kwa hapo (TIPS).
Aidha, Serikali kufanikiwa kuongeza huduma mbalimbali kufanyika kupitia mfumo huo ikiwemo malipo ya Serikali kupitia benki na mitandao ya simu pamoja na malipo ya wafanyabiashara kupitia msimbomilia (QR Code), mfumo wa TIPS umeboreshwa na kuwezesha miamala ya uhamisho wa fedha kutoka nje ya nchi.
Akieleza zaidi kuhusu malipo ya kidijitali kuanzia mwaka ujao wa fedha amesema pia, biashara zinazofanyika kwenye majengo makubwa ya biashara (shopping malls), maeneo ya mazoezi (Gyms), vituo vya kuonesha sinema, vituo vya mafuta.
Pia, uuzaji na ununuzi wa magari, kumbi za mikutano na sherehe, viwanja vya michezo pamoja na maeneo ya maonyesho ya biashara ya kimataifa kama vile Sabasaba na Nanenane.
“Ada na michango yote ya huduma za elimu kuanzia shule za awali, shule za msingi, sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu; gharama za malazi, chakula na vinywaji katika hoteli, migahawa na huduma zote zinazohusiana na utalii, biashara ya upangishaji na ununuzi wa majengo, viwanja na mashamba.
“Shughuli za sekta ya kilimo zinazotekelezwa kupitia vyama vikuu vya ushirika na Amcos katika mazao ya kimkakati (pamba, korosho, kahawa, chai, katani na tumbaku pamoja na pembejeo na viuatilifu yote yafanyike kidijitali,” amesema.
Vocha za kukwangua kuondolewa
Sambamba na hatua hizo, Serikali pia kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) itaondoa vocha za simu za kukwangua kwa mkono ambapo hatua hiyo itaanza katika maeneo yote ya mijini ambapo itasaidia kujifunza kabla ya kutekeleza pendekezo hili kwa maeneo mengine ya nchi.
Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya fedha itaendelea kuimarisha miundombinu itakayowezesha malipo kufanyika kwa njia za kidijitali ikiwemo kuongeza kasi ya utoaji wa nyenzo za malipo ya kidijitali (lipa namba, QR Codes) kwa wafanyabiashara wadogo (bodaboda na baba/mama lishe, masoko ya wazi).
“Wafanyabiashara wanaotumia njia za kidijitali kupokea malipo watapata sifa za ziada wakati wa kuomba mikopo inayotolewa na Serikali pamoja na watoa huduma za fedha,”amesema.
Hata hivyo, pamoja na hatua hizi, Serikali pia inasisitiza Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) kuanza utekelezaji wa programu ya Jamii Namba kama ilivyoelekezwa katika Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali nchini (Tanzania Digital Economy Strategic Framework 2024- 2034) kwa lengo la kuongeza uwazi na utambuzi wa taarifa mbalimbali.
Kuanzia mwaka 2026/27, Serikali itaweka sharti la uthibitisho wa malipo ya kidijitali kuwa rejea ya lazima itakayotumika kuidhinisha maombi ya uhamishaji wa mali kama vile ardhi, majengo na magari.
Hivyo, taasisi zote za umma, kama vile Mamlaka ya Mapato Tanzania, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Brela (Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni) na nyingine zitalazimika kupokea uthibitisho wa kidijitali kuidhinisha uhamishaji wa mali. Hatua hii itaanza Julai Mosi 2026.