Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mafuta ghafi ya mchikichi kutozwa ushuru wa forodha asilimia 10

Muktasari:

  • Mwaka jana, Serikali ilitangaza kutoza asilimia 10 ya ushuru wa forodha kwa mafuta ghafi ya kula isipokuwa ya mchikichi, lakini mwaka huu imetangaza kuyatoza.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imepanga kutoza ushuru wa forodha kwa kiwango cha asilimia 10 kwenye mafuta ghafi ya kula ya aina zote ikiwemo ya mchikichi na yaliyochakatwa kwa kiwango kidogo.

Hatua hiyo ya Serikali, inakuja baada ya kufanya mashauriano na wadau mbalimbali wakiwemo wazalishaji wa bidhaa hiyo na kamati mbalimbali za Bunge.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma leo, Alhamisi Juni 11, 2026 na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, alipowasilisha Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/27.

“Hatua hii inalenga kuondoa changamoto ya udanganyifu wa uainishaji wa bidhaa, unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu ambao hutumia nafuu iliyopo kwenye mafuta ya mchikichi kuingiza yaliyochakatwa,” amesema.

Amesema matumizi ya kiwango hicho yanaendana na mwelekeo wa sera unaotumika na baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa sasa ikiwemo Kenya, Uganda ambazo zinatoza ushuru wa forodha kwa kiwango cha asilimia 10 kwenye mafuta ghafi ya mchikichi kutoka nje ya jumuiya.

Kwa upande mwingine, amesema Serikali imetoa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani kwenye mafuta ya kula yaliyozalishwa kwa kutumia mbegu zinazozalishwa ndani ya nchi.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kutoza ushuru wa forodha kwa kiwango cha asilimia 35 au dola 300 kwa tani moja ya ujazo wa mafuta safi kutegemea kiwango kitakachokuwa kikubwa.

“Serikali imeacha kanuni za uagizaji mafuta ya kula nchini ili kuhamasisha na kukuza tasnia ya mafuta ya kula yanayozalishwa kwa kutumia mbegu za ndani ya nchi,” amesema.

Katika hatua nyingine, amesema Wizara ya Kilimo itaratibu utoaji vibali vya uagizaji mafuta kutoka nje ya nchi na hilo litafanywa baada ya kujiridhisha kuhusu uwekezaji na uzalishaji wa mbegu za alizeti, pamba na machikichi chini ya kanuni ya Copra (Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mengine) za mwaka 2026.

Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, amesema Serikali itaendelea kutoa ruzuku ya mbegu za alizeti, pamba na miche milioni mbili kila mwaka kwa lengo la kukuza uzalishaji wa mbegu zinazotumika kuzalisha mafuta ya kupikia na kuondoa uagizaji mafuta.