LIVE: Bajeti Kuu ya Serikali ikisomwa bungeni Dodoma
Dar es Salaam. Matumaini au maumivu zaidi kuhusu hatua za kupunguza gharama za maisha kwa wananchi yatajulikana leo, Serikali inapowasilisha bajeti yake kuu ambayo ni msingi wa utendaji wake kwa siku 365 za mwaka wa fedha 2026/27.
Bajeti hiyo inawasilishwa katikati ya mtihani wa kupanda kwa gharama za bidhaa muhimu kwa wananchi, kulikosababishwa na ongezeko la bei ya mafuta, ambalo ni matokeo ya vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati.
Ni bajeti inayowasilishwa katikati ya mtihani huo kwa sababu bei ya lita moja ya petroli imefikia Sh4,086 kutoka Sh2,864, huku dizeli ikiwa juu zaidi ikiuzwa kwa Sh4,115 kutoka Sh2,858 kwa lita, jambo linaloongeza gharama za uzalishaji viwandani na usafirishaji wa watu na bidhaa.
Ongezeko hilo limeathiri moja kwa moja usafirishaji, uzalishaji na usambazaji wa bidhaa, hivyo kuchochea kupanda kwa bei za vyakula na bidhaa nyingine muhimu.
Nauli zapanda nchini
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Latra), pamoja na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), tayari zimeongeza bei za nauli katika maeneo mbalimbali.
Safari fupi za hadi kilomita 10, nauli zimepanda kutoka Sh600 hadi Sh700, huku safari za kati zikifikia Sh1,500 kulingana na umbali. Nauli za mabasi ya masafa marefu zimeongezeka hadi wastani wa Sh57.93 kwa kilomita katika barabara za lami.
Safari ya Dar es Salaam–Arusha sasa inagharimu zaidi ya Sh36,000. Huduma za usafiri wa mtandaoni zimepanda kwa takriban asilimia 22, huku nauli za boti kati ya Dar es Salaam na Zanzibar zikifikia Sh40,000 hadi Sh80,000.
Athari kwa kaya
Kwa wananchi wa kawaida, hasa mijini, gharama za usafiri zimekuwa moja ya mizigo mikubwa zaidi ya kila mwezi. Kaya nyingi zimelazimika kupunguza matumizi ya msingi ili kumudu safari za kazi na shughuli za kila siku.
Mfumuko huo umeathiri moja kwa moja uwezo wa wananchi kununua chakula, kulipa kodi za nyumba na kugharamia mahitaji ya familia.
Aidha, kwa wazazi na walezi wanaosomesha watoto katika shule binafsi, gharama za ada na usafiri zimeanza kupanda na kuongeza maumivu.
Mfumuko wa bei wa mwaka kwa sasa ukiwa karibu asilimia 4.0, ongezeko hilo linachangiwa zaidi na kupanda kwa gharama za usafiri kwa asilimia 9.2 na chakula kwa asilimia 5.7.
Kwa kuwa mafuta yanaathiri kila hatua ya mnyororo wa uzalishaji, kuanzia kilimo hadi usambazaji, athari zake zinaenea haraka kwenye uchumi mzima.
Maoni ya wataalamu
Mhadhiri wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Daudi Ndaki, amesema misukosuko ya kisiasa duniani imechangia ongezeko la gharama za nishati na bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.
Amesema Tanzania imedhibiti sehemu ya athari hizo kutokana na uzalishaji wa chakula ndani ya nchi, lakini kuna haja ya mageuzi ya muda mrefu katika nishati, ajira na uzalishaji.
Meneja wa Uchambuzi wa Sera wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Mercy Philipo, amesema ukuaji wa uchumi unaweza kupatikana kwa kupanua wigo wa kodi badala ya kuongeza viwango vya kodi.
Amesema maboresho ya mifumo ya ukusanyaji kodi yataongeza mapato bila kuongeza shinikizo kwa wafanyabiashara.
Malalamiko ya wafanyabiashara
Wafanyabiashara wa Kariakoo jijini Dar es Salaam wamelalamikia kodi na tozo nyingi zinazotozwa na taasisi tofauti. Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa soko hilo, Severine Mushi, amesema mfumo wa sasa ni mgumu na unapaswa kurahisishwa.
Amependekeza kuwepo kwa mfumo mmoja wa malipo, ili kupunguza urasimu na gharama za uendeshaji wa biashara.
Aidha, ameeleza changamoto za miundombinu, kama msongamano na ukosefu wa maeneo ya maegesho, vinavyoathiri biashara.
Wito wa kuimarisha sekta isiyo rasmi
Mkurugenzi wa Chama cha Biashara Tanzania, Oscar Kisanga, amesisitiza haja ya kuhamasisha sekta isiyo rasmi kuingia kwenye mfumo rasmi wa kodi ili kupanua wigo wa mapato ya Serikali.
Amesema mazingira rafiki ya biashara na sera thabiti zitasaidia kuongeza usajili wa wafanyabiashara.
Amesisitiza kuwa mabadiliko ya mara kwa mara ya kodi yanadhoofisha mipango ya uwekezaji.
Viwanda na ushindani
Kwa upande wa Shirikisho la Wamiliki wa Viwanda Tanzania (CTI), limesema gharama kubwa za uzalishaji nchini bado ni changamoto.
Mwakilishi wa shirikisho hilo, Akida Mnyenyelwa, amesema bidhaa za ndani zinakabiliwa na ushindani kutoka kwa bidhaa za nje kutokana na gharama kubwa za uzalishaji.
Kilimo, nishati na vijana
Sekta ya kilimo, inayotegemewa na zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania, inaendelea kuathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa na gharama za pembejeo.
Serikali imepanga kuwekeza katika umwagiliaji, huduma za ugani na kilimo kinachozingatia mazingira ili kuongeza tija.
Sekta ya maji imetengewa Sh1.12 trilioni, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mabwawa kwa ajili ya umwagiliaji na usalama wa maji.
Sekta ya nishati nayo inatarajiwa kupewa kipaumbele, hasa katika upanuzi wa umeme vijijini na nishati safi ya kupikia.
Kwa upande wa ajira za vijana, licha ya kutengwa kwa Sh200 bilioni kwa miradi ya kujiajiri, wataalamu wanasema suluhisho la muda mrefu litategemea ukuaji wa viwanda na uwekezaji wa sekta binafsi.
Matarajio ya wengi ni kuona hatua za kupunguza mzigo wa maisha, kuimarisha uzalishaji, kupanua ajira na kuhakikisha uchumi unakua kwa njia shirikishi zaidi.
Alichosema waziri
Akitoa taarifa ya awali kuelekea kuwasilishwa kwa bajeti hiyo, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema imejikita kuwanufaisha zaidi wananchi kupitia vipaumbele vipya vya maendeleo na uboreshaji wa ukusanyaji mapato.
Amesema bajeti hiyo imezingatia mikakati ya muda mrefu ya maendeleo pamoja na mazingira ya uchumi wa ndani na kimataifa.
Balozi Omar amesema uwasilishaji wa bajeti hiyo unakwenda sambamba na makubaliano ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki yanayowataka mawaziri wa fedha kuwasilisha mapendekezo ya bajeti kwa siku na muda mmoja, kila Alhamisi ya pili ya mwezi Juni.
Pia, amesema mchakato huo unalenga kutimiza matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Amesema Bajeti ya 2026/27 ni ya kipekee kwa kuwa inaanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2026/27–2030/31), pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025.
Akizungumzia utekelezaji wa bajeti inayoendelea, Balozi Omar amesema Serikali imepata mafanikio katika ukusanyaji wa mapato ya ndani yaliyofikia lengo, huku akibainisha kuwa matumizi yamekabiliwa na changamoto zilizohitaji uangalizi wa karibu.
Kwa mwaka 2026/27, amesema sehemu kubwa ya matumizi itagharamiwa na mapato ya ndani yanayokadiriwa kufikia Sh46.8 trilioni.
Amesema kipaumbele kimewekwa katika miradi ya kimkakati, ikiwemo ujenzi wa Reli ya SGR, miundombinu ya barabara, sekta ya maji, nishati na maendeleo ya rasilimali watu.
Katika hatua ya kuimarisha mfumo wa kodi, amesema Serikali ilipokea jumla ya mapendekezo 727 kutoka kwa wadau mbalimbali, ikiwemo sekta binafsi, taasisi za elimu ya juu, asasi za kiraia na wananchi. Mapendekezo hayo yalihusu maboresho ya kodi, ada na tozo mbalimbali.
Kati ya mapendekezo hayo, amesema 125 yalikubaliwa kama yalivyowasilishwa, 121 yakaboreshwa kabla ya kupitishwa, 295 yakakataliwa, 107 yakapelekwa kwa taasisi husika kwa uchambuzi zaidi, 47 yakabaki bila uamuzi kutokana na upungufu wa takwimu, huku 32 yakiwa katika hatua za utekelezaji.