Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Teknolojia mpya ya upasuaji, wagonjwa kuruhusiwa siku hiyohiyo

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akizungumza katika Mkutano wa 31 wa Kisayansi wa Chama cha Madaktari wa Upasuaji Tanzania (TSA) unaofanyika jijini Mwanza.

Muktasari:

  • Wataalamu wanasema kuendelea kwa matumizi ya kamera ndogo katika upasuaji (laparoscopic surgery) kutasaidia kupunguza mateso kwa wagonjwa, kuongeza ufanisi wa huduma za afya na kuimarisha mfumo wa afya nchini.

Mwanza. Wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji nchini, wanatarajiwa kuanza kunufaika na teknolojia ya upasuaji kwa kutumia kamera ndogo utakaopunguza maumivu, kuharakisha kupona na hata kuwawezesha kuruhusiwa hospitalini siku hiyohiyo baada ya kufanyiwa upasuaji.

Mbinu hiyo ya kisasa inayojulikana kama ‘minimal invasive surgery’ inahusisha kufanya upasuaji kupitia matundu madogo ya sentimita chache kwa kutumia kamera maalumu, tofauti na upasuaji wa zamani uliokuwa ukihitaji kuchana sehemu husika kwa kiwango kikubwa.

Kwa mujibu wa wataalamu, upasuaji wa zamani ulihusisha kukata mwili kwa urefu wa takribani sentimita 10 hadi 20 au zaidi kulingana na aina ya operesheni hali iliyosababisha maumivu makali, hatari ya maambukizi na muda mrefu wa kupona.

Hatahivyo, kwa teknolojia ya sasa madaktari hutumia matundu ya sentimita 0.5 hadi 3 pekee kufanya upasuaji mkubwa bila kuchana mwili kwa kiwango kikubwa, mabadiliko yanayotokana na matumizi ya mbinu za kisasa za upasuaji kwa kutumia kamera na vifaa maalumu zinazopunguza ukubwa wa jeraha na muda wa matibabu.

Akizungumza leo Alhamisi, Juni 11, 2026, katika Mkutano wa 31 wa Kisayansi wa Chama cha Madaktari wa Upasuaji Tanzania (TSA) jijini Mwanza, Rais wa chama hicho, Dk Olivia Kimario amesema teknolojia hizo zimeleta mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma za upasuaji.

Rais wa Chama cha Madaktari wa Upasuaji Tanzania (TSA) akizungumza katika Mkutano wa 31 wa Kisayansi wa chama hicho uliofanyika jijini Mwanza.

“Kuna vifaa vinavyoendelea kuvumbuliwa kila siku vinavyorahisisha upasuaji na kufanya uwe na mafanikio makubwa zaidi, huku vikimpunguzia mgonjwa maumivu na muda wa kupona,” amesema Dk Kimario.

Amesema tofauti na zamani ambapo wagonjwa walikuwa wanapata makovu makubwa na maumivu ya muda mrefu, sasa wanapata nafuu haraka kutokana na mbinu hizo mpya.

“Watanzania watarajie kwamba unaweza kwenda hospitali leo asubuhi jioni unatoka…maana yake hiyo inakwepesha mtu analala hospitali siku tano, wiki hospitali au mwezi saa nyingine..kwahiyo muda utakwenda kupungua na hata ukishafanyiwa operesheni hata kama ni siku moja hali ya maumivu itakuwa tofauti,”amesema Dk Kimario.

Daktari wa mifupa kutoka Hospitali ya Paragon Medical, Dk Taha Karimjee amesema kwa sasa madaktari wanaweza kufanya upasuaji mkubwa kupitia matundu madogo ya sentimita chache kwa kutumia kamera.

“Tunachana sentimita mbili au tatu tu na kufanya upasuaji wote…zamani ulikuwa unafungua mwili kwa kiwango kikubwa, jambo lililosababisha mgonjwa kutumia muda mrefu kupona,” amesema Dk Karimjee.

Amesema kwa upasuaji wa zamani, mgonjwa alihitaji siku 3 hadi 7 au zaidi kuanza kusimama na wakati mwingine alilazimika kukaa hospitalini kwa wiki moja hadi mbili kulingana na hali yake tofauti na sasa wengine wakisimama baada ya saa sita za upasuaji.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akizungumza katika Mkutano wa 31 wa Kisayansi wa Chama cha Madaktari wa Upasuaji Tanzania (TSA) unaofanyika jijini Mwanza.

Akifungua mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema Serikali inaunga mkono matumizi ya teknolojia hizo ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

“Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya kisasa na kuhakikisha teknolojia kama Akili Hunde inatumika ili huduma ziwe bora, nafuu na zinapatikana kwa wote,” amesema Mtanda.

Amesema bila kuimarisha huduma za upasuaji, malengo ya kufikia huduma ya afya kwa wote hayawezi kufikiwa akisisitiza ushirikiano kati ya wataalamu na Serikali.

“Tunatambua changamoto zilizopo mbele yetu iwe ni miundombinu, maadili, au gharama lakini kwa pamoja kupitia ushirikiano imara kati ya Serikali, vyama vya kitaaluma na washirika wa kimataifa tunaweza kuzishinda,”amesema.

Mkazi wa jijini Mwanza, Juliana Faustine amesema mbinu hiyo itawarahisishia wagonjwa kupona haraka na kurejea kwenye majukumu yao ya kila siku.

Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa 31 wa Kisayansi wa Chama cha Madaktari wa Upasuaji Tanzania (TSA) unaofanyika jijini Mwanza.

“Kama mtu anaweza kufanyiwa operesheni na akatoka siku hiyo hiyo, itatusaidia sana sisi wanawake ambao tuna majukumu mengi ya kufanya ujasiriamali na kuhudumia familia,” amesema.

Naye, Rutta Musa amesema kupungua kwa muda wa kulazwa kutokana na kufanyiwa upasuaji kutapunguza gharama na hofu kwa wagonjwa wengi hasa wenye kipato kidogo.

“Watu wengi wanaogopa operesheni kwa sababu ya maumivu na muda mrefu wa kupona…lakini hii teknolojia itabadilisha hilo na kuwapa ujasiri wa kutafuta matibabu mapema,” ameeleza.