Mtoto akatwa mkono baada ya kupigwa shoti ya umeme Dodoma
Muktasari:
- Mtoto mwenye umri wa miaka 11 kutoka Kijiji cha Kongogo, Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma amekatwa mkono wa kulia baada ya kuunguzwa na waya wa umeme uliokuwa umeanguka.
Dodoma. Mtoto, Mgulumi Saning'o (11), mkazi wa Kijiji cha Kongogo Kata ya Babayu wilayani Bahi, Mkoa wa Dodoma, amekatwa mkono wa kulia baada ya kujeruhiwa na waya wa umeme uliokuwa uliokuwa unaning'inia eneo la kijiji hicho.
Mbali na kupoteza mkono, mtoto huyo ameungua sehemu mbalimbali za mwili kuanzia miguuni hadi mikononi baada ya kupigwa shoti ya umeme katika tukio lililotokea Mei 4, 2026.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Mei 31, 2026 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, baba wa mtoto huyo, Mlewa Saning'o amesema ajali hiyo ilitokea wakati mtoto wake alipokuwa akicheza pamoja na wenzake karibu na eneo ambalo waya huo ulikuwa ukining’inia.
Amesema mtoto huyo alipokuwa akipita eneo hilo aligusa waya wa umeme uliokuwa unaning'inia kwenye nguzo na kupigwa shoti iliyomsababishia majeraha makubwa.
Mtoto Mgulumi Saning'o (11) akiwa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma baada ya kupigwa shoti na umeme iliyosababisha kukatwa mkono wake wa kulia.
Saning'o amesema baada ya tukio hilo mtoto alipelekwa Zahanati ya Kijiji cha Kongogo, lakini kutokana na ukubwa wa majeraha alipatiwa rufaa kwenda Hospitali ya Wilaya ya Bahi na baadaye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
“Walimfanyia upasuaji wa kwanza ili kuruhusu damu ipite kwenye mishipa ya mkono wa kulia ambao ulikuwa umeathirika sana. Baadaye aliruhusiwa kurudi nyumbani, lakini mkono huo uliendelea kuoza na tuliporudi hospitali Mei 29, 2026 madaktari walilazimika kuukata,” amesema Saning'o.
Amesema katika hatua za awali, Ofisi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Wilaya ya Bahi ilitoa usafiri wa kumpeleka mtoto hospitalini na wafanyakazi wake walichanga Sh200,000 kusaidia matibabu.
Hata hivyo, amesema kwa sasa amebaki na deni la matibabu la Sh308,000 ambalo hana uwezo wa kulilipa.
“Naona kama nimetelekezwa. Sina uwezo wa kugharamia matibabu haya na nilitarajia kupata ushirikiano zaidi kutokana na mazingira ya tukio lenyewe,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kongogo, Frank Liberati, amesema taarifa alizozipata zinaonyesha mtoto huyo alikuwa akicheza na wenzake karibu na eneo ambalo waya wa umeme ulikuwa umeanguka.
Amesema baada ya mtoto huyo kunaswa na umeme, watoto wengine walikimbia kwa hofu, huku mkazi mmoja akitumia mti kumtoa kwenye waya huo.
“Tulimkuta ameungua vibaya na kupoteza fahamu. Tulimkimbiza zahanati kwa matibabu ya awali kabla ya kupelekwa hospitali,” amesema Liberati.
Amesema viongozi wa kijiji waliwasiliana na Tanesco na baadaye waliombwa kuandika taarifa ya tukio hilo.
Liberati amesema majibu yaliyotolewa baadaye yalieleza shirika hilo halikuhusika na tukio hilo kwa kuwa mtoto ndiye aliyegusa waya huo.
Tanesco yajibu
Akizungumzia tukio hilo, Meneja wa Tanesco Mkoa wa Dodoma, Donasiano Shamba amesema shirika hilo linafahamu kuhusu ajali hiyo lakini halioni kuwa lina wajibu wa kubeba gharama za matibabu.
Kwa mujibu wa Shamba, tukio hilo lilitokana na uharibifu wa miundombinu ya umeme baada ya watu wasiojulikana kuiba vifaa vinavyosaidia kushikilia nguzo na nyaya za umeme.
Amesema hali hiyo ilisababisha baadhi ya nyaya kulegea na kuning'inia katika eneo lisilo na makazi ya watu.
“Watoto walikuwa wanachezea waya huo uliokuwa umening'inia na ndipo walipogusa nyaya zenye umeme. Eneo hilo ni porini na hatukuwa tumepata taarifa kuwa nyaya hizo zilikuwa zimeanguka,” amesema Shamba.
Ameongeza kuwa Tanesco imekuwa ikitoa elimu ya tahadhari kuhusu hatari za umeme kwa wananchi na kwamba watu wanapaswa kuepuka kugusa nyaya za umeme zinapoonekana zimeanguka au kuning'inia.
“Kwa mtazamo wetu, gharama za matibabu si jukumu la Tanesco. Hata hivyo, wafanyakazi wetu walichanga fedha na kumsaidia mzazi wakati mtoto alipokuwa akipatiwa matibabu ya awali,” amesema.