Saa 16 kuwatenganishwa pacha wa Tanzania walioungana
Mama wa pacha walioungana wa Kitanzania Nancy na Nice Sospeter, Angerina Magori akitazama kwa hisia kali mabinti zake wakipelekwa chumba cha upasuaji mjini Riyadh, Saudi Arabia, kwa ajili ya upasuaji mgumu wa kuokoa maisha kwa kuwatenganisha, Mei 7, 2026.
Muktasari:
- Kabla ya kuondoka nchini Januari 26, 2026 kwenda nchini Saudi Arabia kwa matibabu hayo, pacha hao walikuwa chini ya uangalizi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja.
Dar es Salaam. Pacha walioungana wa Kitanzania, Nancy na Nice Sospeter leo Alhamisi, Mei 7, 2026 wanafanyiwa upasuaji mkubwa wa kuwatenganisha katika mji wa Riyadh, Saudi Arabia, katika operesheni ngumu na yenye hatari kubwa inayofanywa na Programu maarufu duniani ya Pacha Walioungana ya Saudi Arabia (Saudi Conjoined Twins Programme - SCTP).
Pacha hao waliozaliwa Julai 30, 2024, waliungana kuanzia kifuani, tumboni hadi nyongani, hali adimu kitabibu inayojulikana kama Thoraco-omphalopagus Ischiopagus Tripus.
Upasuaji huo unafanywa na jopo la wataalamu 34 wakiongozwa na Dk Abdullah Al Rabeeah, huku ukitarajiwa kuchukua takribani saa 16 na kupitia hatua 10 za upasuaji.
Nancy na Nice walizaliwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, jijini Mwanza kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam na baadaye kupelekwa Riyadh Januari 2026 kwa ajili ya uchunguzi maalumu na maandalizi ya matibabu.
Hii ni mara ya tatu kwa Tanzania kupeleka pacha walioungana katika Programu ya Saudi ya Kutenganisha Mapacha kupitia Hospitali ya Taifa Muhimbili, jambo linaloonyesha kuimarika kwa ushirikiano katika kushughulikia kesi adimu na ngumu za upasuaji wa watoto.
Mama wa pacha walioungana wa Kitanzania Nancy na Nice Sospeter, Angerina Magori akitazama kwa hisia kali mabinti zake wakipelekwa chumba cha upasuaji mjini Riyadh, Saudi Arabia, kwa ajili ya upasuaji mgumu wa kuokoa maisha kwa kuwatenganisha, Mei 7, 2026.
Awali, programu hiyo ilifanikiwa kuwatenganisha pacha wa Kitanzania Hassan na Hussein mwaka 2024.
Gharama zote za upasuaji huo, ikiwemo matibabu, usafiri na malazi, zinagharamiwa kikamilifu na Ufalme wa Saudi Arabia kupitia Kituo cha Misaada ya Kibinadamu na Huduma za Dharura cha Mfalme Salman (KSrelief), bila familia kubeba mzigo wowote wa kifedha.
Mama wa pacha hao, Angerina Magori, alisema familia imeendelea kuwa na matumaini katika safari hiyo ngumu.
“Tulipoelezwa kuwa upasuaji huo ungefadhiliwa kikamilifu na kufanywa na timu yenye uzoefu mkubwa, tulipata matumaini ambayo hatukuwahi kuyapata tangu siku mapacha walipozaliwa,” alisema.
Programu ya Saudi ya Kutenganisha Pacha Walioungana, iliyoanzishwa mwaka 1990, imepitia kesi 157 kutoka nchi 26 na imefanikiwa kuwatenganisha jozi 70 za mapacha walioungana kabla ya operesheni hii.
Taarifa za kitabibu kuhusu matokeo ya upasuaji huo zinatarajiwa kutolewa baada ya kukamilika kwa operesheni hiyo baadaye leo, Alhamisi Mei 7, 2026.
Mama wa pacha walioungana wa Kitanzania Nancy na Nice Sospeter, Angerina Magori akitazama kwa hisia kali mabinti zake wakipelekwa chumba cha upasuaji mjini Riyadh, Saudi Arabia, kwa ajili ya upasuaji mgumu wa kuokoa maisha kwa kuwatenganisha, Mei 7, 2026.
Jinsi walivyoungana
Kwa namna watoto hao walivyoungana, ilielezwa watahitaji matibabu yenye teknolojia ya hali ya juu pamoja na mabingwa wa upasuaji waliobobea.
Hayo yalisemwa Januari 26 mwaka huu na daktari bingwa mbobezi wa upasuaji watoto Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Zaituni Bokhari wakati wa kuwaaga watoto hao katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere.
“Watoto hawa sasa wana mwaka mmoja na miezi mitano, wao wameungana kwenye tumbo, mpaka kwenye nyonga, wana miguu mitatu na wanashirikiana pamoja njia ya haja kubwa,” alisema.
Dk Zaituni ambaye aliambatana na watoto hao kwenda kwenye matibabu Saudia, alikuwa karibu nao kwa kipindi chote walichokuwa Muhimbili.
Mama wa Nancy na Nice, Angelina George (38) kutoka Bunda Mara alisema alifikishwa Muhimbili Agosti 13 mwaka 2024 na wakati wote wamepokea huduma hospitalini hapo kwa gharama za Serikali.