Aliyetarajia kujifungua ‘pacha’ watatu ajifungua wanne, aomba msaada
Rachel Simba (kushoto), aliyejifungua watoto wanne kwa mpigo katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), akiwa na mume wake, Paschal Wilbroad katika wodi ya wazazi ya Hospitali hiyo mkoani Kilimanjaro.
Muktasari:
- Mama mkazi wa Kilimanjaro, Rachael Simba (28), amejifungua watoto wanne njiti katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC). Watoto wanaendelea vizuri chini ya uangalizi maalumu, huku mama akiomba msaada wa gharama za matibabu kutokana na changamoto za uzazi huo nadra.
Moshi. Mama mkazi wa Newland TPC, mkoani Kilimanjaro, Rachael Simba (28), amejifungua watoto wanne waliozaliwa kabla ya muda (njiti) katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), tukio linalotajwa kuwa nadra kitaalamu.
Rachel alijifungua watoto hao Aprili 22, 2026 kwa njia ya upasuaji. Amesema hakutarajia kupata watoto wanne kwa mpigo, kwani awali alielezwa kuwa alikuwa na ujauzito wa watoto watatu.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Ijumaa, Aprili 24, 2026, hospitalini hapo, Rachael amesema watoto hao wanaendelea vizuri chini ya uangalizi maalumu katika chumba cha watoto njiti (Nicu), kutokana na kuzaliwa na uzito pungufu.
Mama huyo, ambaye pia ana mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka miwili na nusu, amesema safari ya ujauzito wake ilianza Septemba 2025 na ilikumbwa na changamoto nyingi, ikiwamo kulazimika kupumzika kitandani tangu alipofikisha miezi mitatu ya ujauzito.
Ameeleza kuwa aligundua ana ujauzito wa mapacha alipokuwa na miezi sita, ambapo alithibitishiwa kuwa ni watatu, kabla ya hali kubadilika ghafla siku ya kujifungua.
“Siku hiyo nilifika kliniki bila dalili zozote za kujifungua, lakini baadaye nikaanza kupata uchungu ghafla na kupelekwa chumba cha upasuaji. Ndipo madaktari walipogundua kuwa watoto ni wanne,” amesema Rachael.
Amesema taarifa hiyo ilimshtua, lakini alimshukuru Mungu baada ya yeye na watoto wake wote kutoka salama.
Kutokana na ukubwa wa ujauzito huo, Rachael amesema alishindwa kufanya shughuli nyingi za kawaida, ikiwamo kutembea na kusimama bila msaada.
Kutokana na watoto wake kuzaliwa kabla ya muda, ameomba msaada kutoka kwa jamii ili kumudu gharama za matibabu, akitaja mahitaji kuwa ni pamoja na oksijeni, dawa za kukomaza mapafu, maziwa na vipimo mbalimbali.
“Gharama ni kubwa sana na tunaambiwa tunaweza kukaa hapa hospitalini kwa zaidi ya mwezi mmoja kulingana na maendeleo ya watoto,” amesema.
Kwa sasa Rachael ana jumla ya watoto watano, akiwamo mtoto wake wa kwanza, huku watoto aliowajifungua sasa wakiwa wanne mmoja wa kiume na watatu wa kike.
Kwa upande wake, daktari wa magonjwa ya kinamama na uzazi katika Hospitali hiyo, Dk Gedion Edward amesema mama huyo alipokelewa Aprili 22, 2026 akiwa na ujauzito wa wiki 31 na siku mbili, baada ya kufika kliniki akiwa na maumivu ya tumbo yasiyo makali.
Amesema baada ya kufanyiwa vipimo vya awali ikiwamo damu, mkojo na ultrasound, walibaini kuwa alikuwa na ujauzito wa zaidi ya watoto wawili, hali ambayo si ya kawaida kwa ujauzito uliotungwa kwa njia ya kawaida.
“Tulipomchunguza zaidi tulibaini ana viashiria vya hatari, hivyo tukamlaza wodini kwa uangalizi wa karibu kabla ya kufanyika kwa upasuaji,” amesema.
Dk Edward amesema kwa kawaida hospitali hiyo hupokea mama mmoja au wawili kwa mwaka wanaojifungua watoto zaidi ya watatu, huku idadi kubwa ya wajawazito hujifungua mtoto mmoja au mapacha.
Ameeleza kuwa kitabibu, uwezekano wa mwanamke kupata ujauzito wa watoto wanne ni mdogo, ukikadiriwa kuwa ni mama mmoja kati ya 6,000.
Amesema ujauzito wa aina hiyo unaweza kusababishwa na uchavushaji wa mayai zaidi ya moja au mgawanyiko wa yai moja lililorutubishwa, hali inayoweza kusababisha mapacha wawili au zaidi.
Akizungumzia hali ya watoto, amesema walizaliwa wakiwa na mifumo tofauti ya ukuaji tumboni, ambapo wawili walikuwa katika mfuko mmoja na wengine wawili katika mifuko tofauti.
Amesema watoto wawili wa kike waliokuwa katika mfuko mmoja kila mmoja ana uzito wa kilo moja, huku mtoto wa kiume akiwa na uzito wa kilo 1.6 na mtoto mwingine wa kike kilo 1.3.
Kwa upande wake, muuguzi wa idara ya akina mama aliyekuwa zamu siku hiyo katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), Secilia Jonathan, amesema alimpokea mama huyo Aprili 22, 2026 akiwa amelazwa wodini na tayari akiwa na maumivu.
“Wakati anapokelewa alikuwa amegundulika kuwa na ujauzito wa mapacha zaidi ya wawili na alikuwa na maumivu makali,” amesema.
Amesema alipofika hospitalini hapo alikuwa na ujauzito wa wiki 31 na siku mbili, na alilazimika kuchomwa sindano za kukomaza mapafu ya watoto.
“Tayari alikuwa ameanza uchungu, hivyo nilimpima na kubaini kuwa mlango wa uzazi ulikuwa umefunguka kwa sentimita tatu. Niliwasiliana na daktari aliyekuwa zamu kwa sababu kwa kawaida mama mwenye ujauzito wa mapacha zaidi ya wawili katika hospitali yetu ya kanda huzalishwa kwa njia ya upasuaji,” amesema.
Secilia amesema wakati wa maandalizi ya upasuaji ndipo ilibainika kuwa si mapacha watatu kama ilivyodhaniwa awali, bali ni watoto wanne.
Amesema kutokana na hali hiyo, wanashauri wanawake wajawazito kuwahi kliniki ndani ya wiki nane za mwanzo wa ujauzito ili matatizo yaweze kugundulika mapema na kupatiwa huduma stahiki.