Prime
Haya hapa maeneo ya kuwekeza Arusha

Muktasari:
- Jukwaa la kiuchumi Arusha limeibua fursa za uwekezaji katika utalii, michezo, kilimo na madini. Viongozi wa kitaifa wasisitiza umuhimu wa kujiandaa kwa mashindano ya Afcon 2027 kwa kuboresha miundombinu na huduma.
Arusha. Wawekezaji wameitwa kuwekeza katika sekta ya utalii, michezo, kilimo na uchimbaji madini katika Mkoa wa Arusha.
Wameitwa wakati wa Jukwaa la Kiuchumi la Mkoa wa Arusha lililofanyika leo, likilenga kujadili fursa za kiuchumi kwa wawekezaji na wananchi katika mkoa huo.
Jukwaa hilo, lililofanyika katika ukumbi wa AICC, lilikutanisha wadau zaidi ya 1,000. Liliongozwa na viongozi mbalimbali ambao ni Mwanajumui wa Afrika, Profesa Patrick Lumumba, Profesa Kitila Mkumbo (Waziri wa Mipango na Uwekezaji), Dk Selemani Jafo (Waziri wa Viwanda na Biashara).

Baadhi ya washiriki wa Jukwaa la Kiuchumi mkoa wa Arusha,wakifuatilia jukwaa hilo leo Jumamosi Mei 3,2025 katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha (AICC).
Wengine ni Mohamed Mchengerwa (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), David Kafulila, jukwaa lililoandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.
Akizungumza na wadau hao, Waziri Mkumbo amewataka wakazi wa Arusha na mikoa ya jirani kutambua kuwa mashindano ya Afcon mkoani humo ni fursa ya kupata fedha na kuinua vipato vyao.
Amesema fursa za uwekezaji wa nyumba za kukodisha (Airbnb), hoteli, na kuwataka wenyeji wenye nyumba zilizopo kwenye mazingira mazuri kuandaa nyumba hizo kwa ajili ya kuzikodisha kwa watakaofika nchini kufuatilia michuano hiyo.
“Afcon inakuja na fursa za wageni, lazima tuweke miundombinu ya kutosha ya malazi, hivyo Airbnb tunazihitaji. Tunahitaji kubadilisha mitazamo ya watu wetu na suala la kuhudumia watoa huduma wetu. Unakuta watu wakiongezeka wanakasirika, kwa hiyo Arusha mjipange kuhudumia watu wa matabaka ya kati, wekeni vizuri miundombinu,” amesema.
Kwa upande wake, Kafulila amesema wakati mataifa ya Tanzania, Kenya na Uganda yakijipanga kwa ajili ya kuandaa fainali za mashindano hayo, ni fursa kwa Watanzania kupitia PPP, na kuwa maandalizi ya mashindano hayo kabla, wakati na baada yataacha alama kwa Tanzania kunufaika kiuchumi.

Baadhi ya washiriki wa Jukwaa la Kiuchumi mkoa wa Arusha, wakifuatilia jukwaa hilo leo Jumamosi Mei 3,2025 katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha (AICC).
Amesema mwaka 2027 mashindano yatakapofanyika, Kenya itakuwa kwenye uchaguzi, hivyo Tanzania itakuwa na nafasi nzuri ya kujipanga kuvuna fursa za kiuchumi.
“Mwaka 2027 Kenya kutakuwa na uchaguzi, na sote tunatambua uchaguzi wa Kenya huwa na hekaheka, hivyo Tanzania ina nafasi nzuri ya kufanya vizuri na kukua kiuchumi katika mashindano hayo. Pia Arusha inaweza kutumia fursa ya kilimo, ikiwemo cha parachichi, kujiinua kiuchumi kupitia PPP,” amesema.
Aidha, Kafulila ametaja fursa nyingine ni pamoja na utalii (ukiwepo wa mikutano, michezo na matibabu), na kuwa katika maeneo mengine mamlaka za Serikali hazipaswi kusubiri bajeti kutoka Ofisi ya Hazina, bali zinaweza kutumia PPP kufanya miradi mbalimbali.
Kwa upande wake, Waziri Jafo amewataka wakazi wa Arusha, hasa eneo la Engaruka kunakotekelezwa mradi huo, kutumia fursa za uwekezaji kuanzia mradi unapoanza kutekelezwa.
“Tutumie fursa kuhakikisha mradi unapotekelezwa wakati wa ujenzi wake tunanufaika nao. Kunahitajika hoteli, wafanyabiashara changamkieni hiyo fursa. Kuna fursa ya utalii kwani wengine wanaweza kutembelea Mlima Oldonyolengai, ukitengeneza nyumba za kulala wageni utapata wateja.”
Akizungumzia jukwaa hilo, Makonda amesema kuwa lengo kuu ni kuwapa fursa wananchi wa Arusha kupata taarifa sahihi juu ya fursa za uwekezaji na biashara kwa ajili ya kuzichangamkia.
Amesema kuwa lengo lingine ni kuwapa nafasi wananchi wa Arusha na Tanzania kwa ujumla kuzijua fursa za uwekezaji zilizotengenezwa na Serikali katika sekta mbalimbali, ili kuchangamkia kwa kujinufaisha kiuchumi
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri, amesema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha inarahisisha mazingira ya uwekezaji nchini, hasa kwa Watanzania wanaoona fursa na kutaka kuzichangamkia.
Profesa Lumumba
Mwanasheria nguli, Profesa Patrick Lumumba, amezitaka nchi za Afrika kujitafakari juu ya hatua za kuchukua ili kuhakikisha zinakuwa nchi zilizoendelea kiuchumi.
Amesema nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikijipongeza kwa hatua za maendeleo ya kiuchumi walizopiga, lakini hatua hizo ni ndogo mithili ya mwendo wa kinyonga na kobe.
Akitolea mfano, amesema nchi kama Vietnam iliyopigana vita hadi mwaka 1975, ambayo kwa sasa ina wananchi wasiozidi milioni 50, ila uchumi wao ni mkubwa kuliko nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
“Tujiulize Wakorea walifanya nini wamepiga hatua? Vietnam hakuna jeshi la malaika waliotua kule kujenga Vietnam ila walifanya kazi. Lazima tutafute fursa na kuziangalia kwa jicho chanya.
“Mfano, nchi za EAC tukipata wageni milioni mbili, iwe Kenya au Tanzania, tunasheherekea kwa nderemo na vifijo, ila nchi ya Singapore inapata wageni kwa mwaka wasiopungua milioni 30.”
Ameongeza,“Hapa kwetu kuna nafasi nyingi. Ni nafasi ya kujiuliza ni hatua zipi tunazozichukua ili Taifa la Tanzania na Afrika zipige hatua.”