Wanafunzi 100 walazwa baada ya kula chakula chenye nyoka

Picha na Mtandao
Muktasari:
- Wapishi walimuona nyoka lakini walimuondoa na kuendelea kuwapatia chakula wanafunzi.
India. Zaidi ya wanafunzi 100 wamelazwa hospitalini baada ya kula chakula kilichodaiwa kuwa na nyoka mfu mwishoni mwa juma, wakiwa shuleni nchini India.
Kwa mujibu wa CBS News, Tume ya Haki za Kibinadamu ya India (NHRC) imesema inaendelea kuchunguza taarifa hiyo ingawa inaelezwa mpishi aliendelea kuwapatia chakula wanafunzi hata baada ya kumtoa nyoka huyo.
Tukio hilo limetokea katika shule ya Serikali katika kijiji cha Mekra, wilaya ya Patna, jimbo la Bihar mji wa Mokama nchini India, mojawapo ya majimbo maskini zaidi nchini humo.
Inaripotiwa karibu watoto 500 walikula chakula hicho, na tukio hilo lilichochea maandamano ya hasira kutoka kwa familia za watoto hao, kwa mujibu wa taarifa ya tume.
Business Standard imesema shule hiyo ya Msingi ya Upkramit Madhya Vidyalaya, kwa mujibu wa wakazi wa eneo hilo nyoka aliingia kwa bahati mbaya ndani ya chombo cha kupikia wakati wa maandalizi ya chakula.
Mara baada ya kula chakula hicho, watoto wengi walianza kutapika na walilalamika kuhisi kizunguzungu, hali iliyosababisha taharuki kijijini.
Zaidi ya wanafunzi 24 waliwahishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mokama, na wawili kuhamishiwa Hospitali ya Barh. Hata hivyo, madaktari walithibitisha kutokuwa na sumu kwenye miili yao.
Nchini humo, chakula cha bure hutolewa kwa mamilioni ya watoto katika shule zote za serikali, ikiwa ni jitihada ya kuwahamasisha kuendelea na masomo yao.
Mpango huo wa chakula cha mchana, unaojulikana kama Mid-Day Meal, ulianzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1925 katika jiji la Chennai (zamani Madras) kwa ajili ya watoto kutoka familia maskini, kwa mujibu wa BBC. Hata hivyo, kumekuwa na malalamiko ya mara kwa mara kuhusu usafi duni wa chakula hicho.
Business Standard inaeleza mnamo mwaka 2013, watoto 23 walifariki baada ya kula chakula kilichochafuliwa na dawa ya sumu ya kuua wadudu katika jimbo hilohilo la Bihar.
Ikiwa taarifa hizo zitathibitishwa, tume inasema tukio hilo linazua suala kubwa la ukiukaji wa haki za binadamu za wanafunzi.