Wanane wafariki dunia, 78 walazwa wakidaiwa kula kasa

Pemba. Watoto wanane wamefariki dunia na watu wengine 78 wamelazwa hospitali kwa madai ya kula samaki aina ya kasa kisiwani Panza, Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba.
Hata hivyo, Daktari wa Wilaya ya Mkoani, Haji Bakari Haji alisema jana kuwa, awali alipowauliza wagonjwa kinachowasibu hawakuweka wazi, hivyo walichukua sampuli na kuzipeleka maabara kwa ajili ya uchunguzi zaidi kufahamu chanzo cha tatizo hilo.
Alisema jumla ya wagonjwa 86 waliofikishwa hospitali wanane wamepoteza maisha.
Dk Haji alisema tukio hilo lilitokea Machi 5 mwaka huu kisiwani hapo.
“Tuliwapeleka Hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani watu 86, kati yao wanane ambao ni watoto walikuwa wameshapoteza maisha, lakini wengine hali zao zinaendelea vizuri, tunasubiri majibu ya uchunguzi wa maabara ili kuthibitisha chanzo cha tukio hilo,’’alisema.
Awali, Sheha wa Shehia ya Panza, Haji Ali Shaali alisema walipata taarifa kutoka kwa baadhi ya wananchi wakidai watu hao wamekula kasa lakini hawajapata uthibitisho, kwa hiyo wanasubiri majibu ya wataalamu.
“Baadhi ya watu walitoa taarifa ya kwamba tatizo hilo limesababishwa na kasa, lakini bado tunasubiri majibu ya wataalamu,” alisema.
Akizungumzia hilo, Miza Kombo Bakari ambaye amepoteza watoto wake wawili, mmoja wa miaka miwili na nusu na mwengine wa miezi mitano alisema tukio hilo limetokea Machi 5 mwaka huu.
Alisema hakufahamu chanzo cha kifo cha watoto wake kilisababishwa na nini, bali aliona mabadiliko na kuanza kutapika ndipo waliwakimbiza kituo cha afya kilichopo karibu naye.
Alisema watoto wake hao mmoja alikuwa na umri wa miaka miwili na mwingine miezi sita ambao walikuwa wameshapatiwa matibabu, lakini muda mfupi wakapoteza maisha.
“Nilikuwa sipo nyumbani nikapata taarifa watoto wangu wanaumwa wanatapika, tukawapeleka hospitali wakapatiwa matibabu lakini baada ya muda mfupi walipoteza maisha,” alisema Bakari.
Mkazi wa kisiwa hicho, Hadiya Abasi Othman alisema alishawahi kula samaki wa aina hiyo na watoto wake lakini hawakudhurika.
Alisema wamepata wasiwasi kutokana taharuki watoto hao kufariki dunia na wengine wakiendelea kupatiwa matibabu.
“Mimi nilishawahi kula na watoto wangu, nilimpata kwa dada yangu lakini tunashukuru hatujaathirika,’’alisema Hadia.
Mhudumu wa Afya, Harub Makame Ali alisema baada ya kupokea taarifa za misiba na watoto wengine kuumwa, walianza kufuatialia kujua chanzo nini lakini wakati wanauliza wananchi wanadai hawafahamu juu ya suala hilo.
“Nilipokea taarifa juzi asubuhi kwamba kumetokea msiba watoto wawili wa familia moja, tukajiandaa na mazishi ya watoto wale, lakini kabla hatujamaliza kuwazika, tukapokea habari kuna wengine tayari walishakufa na wengine wanaumwa,” alisema Ali.