Wataalamu waeleza chanzo sumu ya kasa

Muktasari:
Wakati watu wa familia moja wakipoteza maisha na wengine 47 kulazwa hospitalini baada ya kula nyama ya kasa huko Zanzibar, imebainika kuwa kuna uwezekano vimelea anavyokula samaki huyo vikachangia kutengeneza sumu kwenye mwili wake ambayo ni hatari kwa afya ya binadamu.
Dar es Salaam. Wakati watu wa familia moja wakipoteza maisha na wengine 47 kulazwa hospitalini baada ya kula nyama ya kasa huko Zanzibar, imebainika kuwa kuna uwezekano vimelea anavyokula samaki huyo vikachangia kutengeneza sumu kwenye mwili wake ambayo ni hatari kwa afya ya binadamu.
Hata hivyo, hilo huwa halitokei mara kwa mara na msisitizo wa Serikali unawekwa kwenye kuzuia samaki hao kuvuliwa na kuliwa kwa kuwa wapo hatarini kutoweka.
Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (Tafiri), Dk Ismael Kimirei alisema kasa anakula vimelea vya kwenye maji na inaweza kutokea akawa amekula kimelea ambacho kinaweza kusababisha sumu kwenye nyama yake.
“Sijui nini hasa kilichotokea kwa hao waliokula, siwezi kuzungumzia kwa undani lakini sijawahi kukutana na utafiti uliowahi kuonyesha kuwa nyama ya kasa haitakiwi kuliwa, ila tunazuia asiliwe kwa sababu za uhifadhi.
“Kasa hafai kuliwa kwa kuwa yupo kwenye kundi la viumbe ambao wako hatarini kutoweka, hivyo si sahihi kuacha watu waendelee kuvua na kuwala, ingawa hilo la sumu inaweza kutokea kutokana na kilichoingia mwilini mwake,” alisema Dk Kimirei.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Emmanuel Bulayi alisema wapo kasa wenye sumu na wasio na sumu na hii hutokana na namna walivyoumbwa.
“Kama ilivyo kwa nyoka, wapo wenye sumu na wasio na sumu basi hata kasa iko hivyo. Sumu hii inaweza ikawa kutokana na walivyoumbwa au hata miili yao kuwa na uwezo wa kuhifadhi sumu inayotengenezwa kutokana na vimelea wanavyokula,” alisema Bulayi.
Sumu ya kasa
Kulingana na Daktari Mkuu wa Hospitali ya Kivunge mkoa wa Kaskazini Unguja, Tamim Said, samaki huyo ana aina ya sumu ambayo kwake haina madhara ila inaweza kumdhuru binadamu.
“Ile sumu kwa kasa mwenyewe inakuwa si tatizo, lakini kwa binadamu ni tatizo kubwa na inategemea kiwango cha nyama kilicholiwa kina sumu kiasi gani, na sumu hii huwaathiri zaidi watoto kwa sababu uwezo wao wa kinga mwili kuhimili unakuwa bado mdogo,” alisema Dk Said.
Mjue kasa
Wataalamu wanasema kuna aina kuu nane za kasa duniani ambao ni Green Turtle (kasa wa kijani au kawaida), Hawksbill Turtle (ng’amba) loggerhead Turtle (kasa duvi), Atlantic Ridley, Pacific Ridley, Scute covered shell Turtle, Leatherback (kasa ngozi) na Olive Ride (kasa muanzi).
Licha ya kasa kufanana sana na kobe, yeye hawezi kurudisha kichwa chake ndani ya gamba lake kwa kuwa ni laini na miguu ya wavuti inayomsaidia kuogelea kwa kasi majini.
Kasa anao uwezo wa kubana pumzi takribani saa tano akiwa majini. Chakula chao kikubwa ni mimea ya baharini kama vile plankton, yavuyavu, mwani, kaa, kamba na matumbawe.
Kasa ni viumbe wa baharini walio katika kundi la ‘reptilian’ na ametajwa kuwa ndio kiumbe mwenye kumbukumbu kubwa katika kundi lake.
Kasa jike anao uwezo wa kurudi katika fukwe za bahari ileile aliyototolewa, licha ya kuwa husafiri bahari moja hadi nyingine ila muda wa kuzaliana unapofika, hurudi kwenye fukwe aliyotokea awali kusudi atage mayai.
Kama ilivyo kwa reptilia wengi, kasa hawezi kuatamia mayai yake, bali huchimba kiota na kufukia mayai yake mpaka yatakapototolewa.
Uwiano wa joto katika kiota ndiyo hufanya jinsia fulani ya kasa wanapototolewa.
Inaelezwa kuwa nyuzi joto 31 kushuka chini, huwezesha kuanguliwa kwa madume na nyuzi joto 34 kwenda juu huwezesha kuanguliwa kwa majike.
Kasa hutaga mayai 7,000 katika maisha yake na kwa kila msimu anaweza kuwa na viota vinne mpaka sita na huwa na mayai 80 mpaka 180.
Pamoja na kutaga mayai mengi kiasi hicho, kasa wachache sana wanaweza kuanguliwa, na wakakua na kuzaliana tena, kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kuwindwa na binadamu.
Viumbe hivi pia huathiriwa na uchafuzi wa mazingira unaofanyika baharini kama vile utupaji wa taka kama za plastiki. Kasa wanapojaribu kuzila, ndiyo huwa mwisho wa maisha yao.