Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fedha za kuagiza mafuta nje ya nchi zapungua, sababu yatajwa

Muktasari:

  • Kati ya mwaka 2022 na 2024 fedha zilizotumika kuagiza mafuta nje ya nchi zimepungua kutoka Sh9.57 trilioni hadi Sh7.62 trilioni mtawaliwa, bei katika soko la dunia na matumizi ya gesi asilia nchi zikitajwa kuwa sababu.

Dar es Salaam. Wakati fedha zilizotumika kuagiza mafuta nje ya nchi zikishuka kwa miaka miwili mfululizo kati ya mwaka 2022 hadi 2024, wadau wamesema huenda matumizi ya gesi asilimia ikawa sababu.

Pamoja na kupungua, lakini bidhaa hizo bado ndiyo zinazoongoza kwa kutafuna fedha nyingi za nchi jambo ambalo limefanya watu kupaza sauti kutaka gharama za ufungaji wa mifumo ya gesi kwenye vyombo vya moto kupitiwa upya, ili kuhakikisha jitihada zinazofanyika sasa zinaendana na kile kilichopo mtaani.

Ripoti ya Hali ya Uchumi ya Tanzania 2024, inaonyesha mafuta yalitumia Sh7.62 trilioni katika mwaka 2024 pekee ikiwa ni pungufu kutoka Sh9.574 trilioni mwaka 2022 na Sh8.04 trilioni mwaka 2023.

Hata hivyo, huenda fedha hizo zilipungua kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia kwani ripoti hiyo inaonyesha kuwa kati ya mwaka 2023 na 2024 bei za jumla za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa zilipungua kwa wastani wa asilimia 9.5, 6.2 na 9.8.

Mafuta yalifuatiwa kwa karibu na uingizaji wa mitambo ambao uligharimu Sh6.63 trilioni katika mwaka 2024.

Wadau wanasema kutopitiwa kwa gharama hizo kutafanya kundi dogo la watu kumudu gharama jambo litakalofanya ununuzi wa mafuta kuendelea kuongezeka, kadri vyombo vya moto vinapoongezeka sambamba na shughuli za kiuchumi kukua.

Bidhaa nyingine zilizotumia fedha lukuki ni vifaa vya usafirishaji vilivyogharimu Sh5.13 trilioni, vifaa kwa ajili ya majengo na ujenzi viligharimu Sh4.5 trilioni, malighafi za viwanda zikigharimu Sh3.28 trilioni, mbolea ilitumia Sh926.3 bilioni, bidhaa za vyakula Sh2.597 trilioni.

Mmoja wa madereva wa taksi ameiambia Mwananchi matumizi ya gesi kwenye magari ni rahisi lakini ufungaji mifumo ndiyo changamoto kwa watu wengi.

“Wengi tunatamani, tatizo ni gharama, wengine wanatoza hadi Sh1.2 kwenye gari, sasa utajikusanya kiasi gani ili ufikishe hela hiyo,” amesema Rajab Rajab, dereva eneo la Upanga.

Maneno yake yaliungwa mkono na Vicent Kipeta ambaye pia ni dereva aliyeshauri jitihada zaidi kufanyika ili kuhamasisha matumizi ya gesi asilia katika maeneo mengi yanayotegemea umeme na mafuta ili kurahisisha maisha.

“Mafuta ni bei na umeme bado haujawa ule wa uhakika saa 24 siku saba za wiki, sasa tukirahisisha gesi ikapatikana kwa wingi watu wakanunua kwa bei rahisi uchumi wetu utakuwa sana kwani vitu vitashuka bei watu watakuwa na uwezo wa kumudu na fedha nyingine wataelekeza kwenye maendeleo.

“Sasa hata ile fedha ya kuagiza mafuta itapungua zaidi na itaelekezwa kwenye huduma nyingine za kijamii ambazo watu wanazihitaji zaidi kama afya, maji, elimu.”

Akizungumzia namna ambavyo fedha za kuagiza mafuta zinaweza kupunguzwa zaidi, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kuondoa Umaskini (Repoa), Dk Donald Mmari amesema jitihada za makusudi zinahitajika ikiwemo katika ujenzi wa miundombinu ya kujaza gesi kwenye magari katika maeneo mengi nchini.

“Hii itasaidia kufanya watu wengi wahame katika matumizi ya mafuta, nchini Malysia ilipitishwa sheria iliyoyataka magari yote ya abiria na mizigo kutumia gesi lakini hili haliwezi kutekelezwa ikiwa miundombinu haijatosheleza nchi nzima,” amesema Dk Mmari.

Amesema njia nyingine inayoweza kutumika ni kuharakisha utekelezaji wa ujenzi wa kusindika gesi ili iweze kusafirishwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo nje ya nchi.

Hili amesema litasaidia kuifanya nchi kupata fedha nyingi za kigeni ambazo zitapunguza matumizi ya fedha za ndani katika kuagiza bidhaa hizo.


Mtazamo wa kiuchumi

Mhadhiri na mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Lutengano Mwinuka amesema zinahitajika jitihada za kikodi kutoka serikalini katika upande wa vifaa vinavyotumika kutengeneza mfumo wa gesi katika vyombo vya moto, ili kusaidia kushusha gharama na watu wengi kumudu.

Amesema hilo linaweza kwenda sambamba na kupunguza kodi kwa magari yote yanayotumia gesi yanayoletwa nchini ikiwa ni moja ya hatua kuelekea kupunguza utegemezi wa mafuta.

“Lakini pia hata Dar es Salaam yenyewe, vituo bado si vingi, hivyo ni muhimu kuweka miundombinu ya kujaza gesi kwenye vyombo vya moto ili kusaidia gesi kupatikana kwa urahisi kwa wale watakaoamua kuhamia huko,” amesema.

Amesema hayo yote yaende sambamba na nchi kuongeza uwezo wake wa kifedha hususan za kigeni ili iweze kumudu kufanya manunuzi mbalimbali pale inapohitajika.

Haya yanaelezwa wakati ambao taarifa ya Wizara ya Nishati inaeleza hadi Aprili, 2025 vituo tisa vya kujazia gesi asilia kwenye magari (CNG) vilikuwa vimekamilika na vinatoa huduma ikilinganishwa na vituo viwili vilivyokuwapo mwaka 2020/21.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko alipokuwa akiwasilisha bajeti ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 alisema mwelekeo wa Serikali ni kuwa na vituo 20 ifikapo Juni, 2026.

Pia, matumizi ya CNG katika vyombo vya moto yameendelea kuongezeka nchini huku akisema kuimarika kwa matumizi ya gesi katika vyombo vya moto hususan magari na bajaji kumekuwa na manufaa makubwa, ikiwemo kuwapa wananchi unafuu wa gharama katika uendeshaji wa vyombo hivyo pamoja na kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni katika uagizaji wa mafuta.

“Ili kuendelea kuweka urahisi, Serikali kupitia TPDC (Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania) linaendelea na taratibu za ununuzi wa vituo sita vya CNG vinavyohamishika ambapo vitatu vitakuwa katika jijini Dar es Salaam, kimoja Morogoro na viwili Dodoma,” amesema Dk Biteko.

Amesema kwa sasa TPDC inakamilisha taratibu za upatikanaji wa maeneo yatakayosimikwa vituo hivyo jitihada zinazoenda sambamba na kuvutia sekta binafsi kuwekeza katika shughuli za mafuta na gesi asilia, ambapo kampuni 61 zimeruhusiwa kufanya biashara ya CNG nchini.

“Hatua hii itaongeza upatikanaji wa CNG kwa ajili ya vyombo vya moto katika mikoa mbalimbali nchini,” amesema.

Katika upande wa usindikaji wa gesi asilia, Dk Biteko amesema maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo yameendelea na hadi Aprili 2025, kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kuendelea na hatua za mwisho za majadiliano na wawekezaji katika vitalu husika.

Kwa ujumla, mtandao wa usambazaji wa gesi asilia nchini umeongezeka kutoka kilomita 102.54 mwaka 2020/21 hadi kilomita 241.58 Aprili, 2025 ambao umewezesha kuunganishwa kwa jumla ya nyumba 1,514, taasisi 13 na viwanda 57.

Pia, zaidi ya vyombo vya moto 15,000 vinatumia gesi asilia (CNG), hivyo kupunguza mahitaji ya petroli na dizeli katika uendeshaji wa vyombo vya moto nchini.