BoT yaziwekea Saccos mtego

Dar es Salaam. Kama wewe ni mwanachama wa Saccos, unafahamu ni kwa kiwango gani michango ya fedha zako iko salama?

Basi unapaswa kuchukua tahadhari, kwani huenda ukawa miongoni mwa zaidi ya wanachama milioni moja wenye akiba zilizo hatarini kupotea katika vyama hivi vya akiba na mikopo (Saccos) vilivyothibitishwa na Kamisheni ya Maendeleo ya Ushirika nchini (TCDC) kutokuwa na sifa ya kuendesha huduma hiyo.

Hadi Februari, kamisheni hiyo imesema ni Saccos 779 pekee ndizo zilikuwa zimepata leseni kati ya 2,400 zilizosajiliwa nchini, sawa na asilimia 43.

Kati ya mwaka 2018 hadi 2019, ukaguzi maalumu uliofanyika ulibaini kuwepo kwa Saccos 6,178 kabla ya Mrajis kuzifuta 2,554 mwaka 2020 na mwaka jana akazifuta nyingine zaidi ya 1,000.

“Hizo Sacoss tumezipa muda wa kurekebisha kasoro zilizopo ili kukidhi vigezo vya kuwa na leseni. Lakini kwa mwanachama aliyepo kwenye Saccos isiyo na leseni, pesa zake ziko hatarini,” alisema Joseph Kasamalala, Mrajis Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Saccos alipozungumza na gazeti hili.

Kutokana na mazingira hayo, baadhi ya wanachama wa vyama hivyo wameitaka Serikali kuchukua hatua zitakazoimarisha usalama wa akiba zao, huku wabobezi wa masuala ya fedha wakishauri kuongeza utoaji elimu ya usalama wa fedha.

Pia, wameshauri Serikali iangalie uwezekano wa kuwa na mfumo mpya utakaosaidia kuvikuza vyama hivyo kutoka ngazi moja hadi nyingine kwa kusaidiwa na wataalamu wa fedha watakaopelekwa kila kata kabla ya kuingizwa kwenye masharti ya kisheria.

Utoaji wa leseni unazingatia Kifungu cha 16(1) cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018 pamoja na kanuni zake za mwaka 2019 kinachozitaka Saccos zote zilizosajiliwa kuomba leseni kabla ya kufanya biashara ya huduma ndogo za fedha.

Kamisheni ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), imesema imeshawasiliana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kufuatilia mwenendo wa akaunti za Saccos zinazojiendesha bila leseni.

“Tulichokifanya ni kushirikisha BoT ili kufuatilia kwa ukaribu akaunti za Saccos hizo kwenye benki walizopo. Hata benki zenyewe zinaelewa namna ya kudhibiti risks (vihatarishi) hizo,” alisema Kasamalala.

Angalizo la kamisheni hiyo kwa wanachama wa Saccos nchini ni sawa na taarifa ya Muungano wa Vyama vya Akiba na Mikopo (SCCULT) ulioshauri wanachama wa vyama hivyo kufuatilia na kuhoji uhalali wa vyama vyao kama unakidhi matakwa ya kisheria.

Ofisa Mawasiliano na Masoko wa SCCULT, Irene Magambo alisema “Saccos ikifutwa itakuwa changamoto kwa mwanachama ambaye atapoteza fedha zake, kwa hiyo tunashauri wanachama kujenga utamaduni wa kufuatilia na kuhoji mwenendo wa vyama vyao mikutanoni sio kuuachia uongozi kila kitu.”


Maboresho ya mfumo

Ili kupata leseni, Saccos inatakiwa kuonyesha vielelezo vya ajira ya mkaguzi wa ndani na mtaji wa daraja husika. Kwa A mtaji ni Sh10 milioni na daraja B ni Sh200 milioni.

Vilevile kunatakiwa iwepo katiba na sera ya mikopo, ajira ya meneja mwenye sifa zinazohitajika kikanuni, bodi ya usimamizi na taarifa ya mkaguzi wa nje. Saccos pia inatakiwa kuambatanisha muhtasari wa mkutano mkuu wenye saini za wajumbe husika na barua ya kuomba leseni hiyo.

Kwa mujibu wa TCDC, Saccos nyingi za daraja B zimepewa leseni hizo isipokuwa Saccos ndogo daraja A. Idadi ya wanachama wa Saccos zilizosajiliwa kumbukumbu zinaonyesha mwaka 2021 walikuwa milioni 1.5 ambao waliongezeka hadi wastani wa milioni mbili mwaka huu kutokana na ongezeko la Saccos zilizopata leseni.

Profesa Abel Kinyondo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anasema dhamira ni njema ya Serikali kuanzisha usimamizi na uratibu wa kisheria lakini haitakuwa na msaada katika vyama hivyo katika ukuaji wake.

“Hao ni mfumo usio rasmi ambao ni zaidi ya asilimia 80 wasiokuwa na akaunti benki lakini wamekubaliana kuanzisha Saccos hizo baada ya kushindwa masharti ya benki. Kwa hiyo ukiwaondoa kwenye mfumo huo kwa masharti magumu ya kisheria unawaua na utawarudisha kwenye umaskini,” alisema na kuongeza:

“Unawezaje kurasimisha kundi lisiloweza kupata msaada kwenye mfumo rasmi? Nadhani wangejengewa uwezo maofisa biashara wa wilaya washuke kwenye vyama hivyo kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha na namna ya kutunza kumbukumbu, kutoa na kuweka fedha pamoja na namna ya kuchukua tahadhari ili wakue taratibu.”


BoT yaangaliza

Wakati TCDC ikiangaliza hivyo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa raia kwa wanachama na Watanzania kwa ujumla kutoa taarifa za Saccos zinazojiendesha bila kukidhi vigezo.

“Watanzania wanatakiwa kuwa makini sana, ili pesa zako ziwe salama unatakiwa kujihakikishia kama Saccos hiyo imepata leseni baada ya usajili kwa sababu kesho na keshokutwa ukitapeliwa utaenda kudai wapi?” alihoji Mary Ngassa, ofisa katika kurugenzi ya usimamizi wa sekta ya fedha ya BoT.

“Kwa wanaotoa mikopo chini ya leseni, hawatakiwi kisheria kutoza riba inayozidi asilimia 3.5 kwa mwezi, hatua zitakazochukuliwa ni pamoja na faini isiyopungua Sh20 milioni au kifungo kwa muda usiopungua miaka miwili,” alisema Mary kwenye mkutano na wahariri wa vyombo vya habari.

Hata hivyo, Irene wa SCCULT alisema vyama hivyo vinao uhuru wa kupanga viwango vya riba. “Saccos zinaweza kutoza riba kati ya asilimia tisa hadi 20.”

Idadi ya wanaojiunga na Saccos inazidi kuongezeka nchini kutoka na faida kadhaa zilizopo ambazo wanachama hunufaika nazo tofauti na wale walio nje.

Faida hizo ni pamoja na kuhifadhi akiba, kununua hisa, mikopo kwa riba nafuu chini ya miongozo na kanuni za kawaida zinazokubalika kwa wanachama. Pili ni kuongeza udhibiti wa matumizi ya pesa, kunufaika na gawio la kila mwaka na fursa ya uwekezaji.

Katibu Mtendaji wa Mwananchi Communications Saccos, Herri Basil anasema katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, zaidi ya wanachama 70 wamekopa na kujenga makazi, 56 wamenunua viwanja, 30 wamenunua magari na wengine wamechukua mikopo kujiendeleza kielimu au kusomesha wategemezi.

“Sisi tumeshapata hati mpya ya usajili iliyoanza kutoka kabla ya mwaka 2021 na leseni mpya iliyoanza kutolewa kielektroniki mwaka huu. Kwa hiyo nashauri Saccos kujenga imani kwa wanachama wao, siku ikitokea changamoto kubwa hakuna atakayekuelewa,” alisema na kuongeza:

“Changamoto ni sheria hiyo ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018 haiwabani wadaiwa sugu kuorodheshwa majina yao katika kituo cha kumbukumbu za mkopaji, kwa hiyo inakwamisha ukuaji.”