BoT ilivyopunguza athari vita vya Ukraine

Dar es Salaam. Mwaka mmoja wa vita vya Ukraine na Urusi umeathiri maeneo sita ya kiuchumi, lakini Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema haikufikia tishio walilotarajia kutokana na juhudi zilizochukuliwa ikilinganishwa na mataifa mengine.

Kwa mujibu wa BoT, vita hivyo vimeathiri dunia kutokana na uchechemuzi wake katika uzalishaji wa theluthi ya mahitaji ya ngano duniani, huku Urusi ikihudumia asilimia 40 ya nishati ya gesi na asilimia 30 ya mafuta katika masoko ya Ulaya. Pia huzalisha asilimia sita ya mahitaji ya makaa ya mawe duniani.

Baadhi ya athari hizo zilizoanza Machi 2022 ni pamoja na mataifa mengi kuporomoka kasi ya ukuaji wa uchumi, kupanda bei ya bidhaa kulikosababisha mfumuko wa bei, ongezeko la bajeti ya uagizaji bidhaa nje uliochochea uhaba wa fedha za kigeni na urari wa biashara na ukata wa taasisi za kifedha.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Tafiti na Sera za Kiuchumi kutoka BoT, Dk Suleiman Missango alitaja kitakwimu akisema pamoja na mfumuko wa bei kuongezeka hadi asilimia 4.8 Desemba mwaka jana, umeonekana kuwa chini ya makadirio ya asilimia 5.4 yaliyotarajiwa kwa mwaka 2022/23.

Tathmini ya athari hizo na mwelekeo wa uchumi wa Taifa ilitolewa jana na wataalamu wa masuala ya uchumi BoT na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari na tathmini ya miezi 11 ya athari za vita hizo.

Dk Missango alitaja baadhi ya hatua zilizofanyika chini ya taasisi hiyo ni pamoja na kuongezeka kwa udhibiti mfumuko wa bei, kulinda akiba ya fedha za kigeni, mikopo ya ndani, ruzuku ya bidhaa muhimu ya mafuta, mbolea, uchechemuzi bajeti sekta ya kilimo na kupunguza tozo mbalimbali katika uzalishaji.

Dk Donald Mmari, mchumi mwandamizi na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti Repoa alishauri maeneo matatu ya msingi yatakayoweka msingi wa kuondoa mshtuko wa uchumi pindi inapotokea mshtuko wa dunia, ikiwamo kuimarisha sekta ya kilimo kwa ajili ya uzalishaji wa chakula na viwandani.

“Pili, ni muhimu kuimarisha sekta muhimu za ukuaji uchumi ikiwamo usafirishaji, lakini pia tuangalie mwelekeo mpya wa masoko ya Afrika badala ya Ulaya pekee, itasaidia sana kuepuka hiyo mishtuko ya athari za kidunia,” alisema Dk Mmari.


Kuhusu athari

Kuna anguko la akiba ya fedha za kigeni kutoka dola 6,386 milioni (Sh14.6 bilioni) Desemba 2021 hadi dola 5,177 milioni (Sh12 bilioni) Desemba mwaka jana kutokana na matumizi mbalimbali, ikiwamo uagizaji bidhaa nje na ulipaji madeni. Uwezo wa fedha hizo kuhudumia Taifa ulishuka wastani wa miezi miwili.

Tatu, ukuaji wa uchumi mwaka 2021 ulikuwa umeanza kupanda kwa asilimia 5.5 lakini kutokana na vita hivyo vilivyoanza Februari mwaka jana, robo ya mwisho ya mwaka 2022, inatarajia ukuaji wa asilimia 4.7.

“Robo ya kwanza ya 2022 ukuaji asilimia 5.5, robo ya pili asilimia 4.8, robo ya tatu asilimia 5.2, nina uhakika robo ya mwisho tufikia kasi ya ukuaji uchumi kwa asilimia 4.7 kwa 2022,” alisema Dk Missanga.

Nne, thamani ya manunuzi ya nje iliongezeka kutoka dola 10 milioni (Sh23 bilioni) mwaka 2021 hadi dola 14.2 milioni (Sh32 bilioni) mwaka jana kutokana na kupanda kwa bei kwenye masoko ya dunia, huku tofauti ya urari wa biashara ikiongezeka kutoka dola 2,407 milioni hadi dola 5,347 milioni.


Mfumuko wa bei

Kuhusu mfumuko wa bei unaoathiri thamani ya Shilingi, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa alisema juhudi zilizofanyika kudhibiti bado zinatia matumaini kuimarika mfumuko huo.

Kwa mujibu wa NBS, mfumuko wa bei umeendelea kushuka hadi asilimia 4.8 Desemba mwaka jana, huku Dk Albina akisema utaendelea kuwa imara kutokana na makadirio yaliyofanyika katika mwenendo wa bidhaa za vyakula na vinywaji utashuka kutoka asilimia 9.7 hadi asilimia 8.4 ifikapo Machi.

Ukokotozi wa mfumuko wa bei hufanyika kwa kutumia bidhaa 383, ikiwamo vyakula na vinywaji pamoja na bidhaa zisizokuwa za vyakula. Ukokotozi huo hufanyika kwa kuangalia wastani wa bei ya bidhaa moja moja na kwa ujumla katika bidhaa hizo 383 na huzingatia utafiti wa kisayansi za kitakwimu kwenye kaya.

“Ninashauri wananchi tuanze utamaduni wa kuotesha mvua nyumbani kwa ajili ya kuendesha shughuli za kulima kwa wingi, tusipande maua tu, tupande pia mazao pale nyumbani, ili kuendelea kudhibiti mfumuko wa bei,” alisema Dk Albina.