BoT yakamilisha utafiti uanzishwaji fedha ya kidijitali

Muktasari:

  • Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeweka wazi hatua za mafanikio katika uanzishaji wa fedha za kidijitali ya Benki Kuu (CBDC) baada ya kukamilisha shughuli za utafiti.

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeweka wazi hatua za mafanikio katika uanzishaji wa fedha za kidijitali ya Benki Kuu (CBDC) baada ya kukamilisha shughuli za utafiti.

Taarifa iliyotolewa jana na BoT imesema kwa kuwa CBDC inaweza kutolewa na benki hiyo na hivyo kuwa chini ya mamlaka yake, iliamua kufanya utafiti wa kutoa fedha aina hiyo.

Hatua hiyo imekuja kufuatia mijadala ya kisiasa na kisera kuhusu sarafu hiyo inayotokana na mageuzi ya teknolojia inayowezesha mchakato wa kurekodi miamala na mali katika mtandao wa biashara, kupitia matumizi ya mali za kidijitali, ikijumlisha sarafu kama Bitcoin, Ethereum, Tether na kadhalika. Akitoa maoni kuhusu hatua hiyo ya BoT, Dk Donald Mmari, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Repoa alishauri elimu zaidi itolewe kwa wananchi ili kutambua faida, hasara na viashiria hatarishi vya sarafu hiyo. “Kwa sababu elimu ya fedha bado iko chini, sasa hii ya kidijitali ni changamoto.”

Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa BoT, zaidi ya nchi 100 duniani ziko katika hatua za kutaka kutumia fedha za kidijitali ya benki kuu, nchi 88 zikiwa katika utafiti, 20 katika uthibitisho wa dhamana, 13 katika majaribio na tatu katika uzinduzi.

Aidha, matokeo ya utafiti huo yameonyesha pia benki kuu nyingi duniani zinakwenda kwa tahadhari katika utekelezaji wa mpango wa matumizi ya fedha hiyo, ili kuepuka kuvuruga utulivu na usalama wa uchumi wao.

“Nchi sita zilikataa kutumia sarafu hiyo (CBDC) kutokana na changamoto za kimuundo na teknolojia, zikiwamo katika hatua za utekelezaji, zikiwamo kutumia fedha taslimu kufanya miamala, mifumo isiyofaa ya malipo na gharama za utekelezaji,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.