Siku 1,902 za Prof Luoga BoT

Dar es Salaam. Januari 9, 2023 gazeti hili lilichapisha habari iliyoeleza kazi na matarajio ya wadau kwa gavana mpya wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba aliyeteuliwa Januari 7, leo tutaangazia mambo makubwa yaliyojiri wakati wa uongozi wa mtangulizi wake, Profesa Florens Luoga.

Tutuba aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Januari 7 kurithi nafasi ya Profesa Luoga, ambaye amemaliza muda wake.

Profesa Luoga aliteuliwa na Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli Oktoba 23, 2017 na amehudumu katika nafasi hiyo hadi Januari 7, 2023.

Katika kipindi cha siku 1,902 alizodumu Profesa Luoga akiwa gavana mambo mengi yalitokea, lakini kuna baadhi yameacha kumbukumbu ya muda mrefu, likiwemo suala la kufungwa kwa maduka ya kubadilishia fedha, hatua iliyohusishwa na udhibiti wa vitendo vya utakatishaji fedha.

Katika sakata hilo lililosababisha kufungiwa kwa maduka zaidi ya 100, Gavana Luoga alisema kati ya maduka ya kubadilishia fedha za kigeni 87 yaliyofanyiwa ukaguzi jijini Dar es Salaam, 82 yalikutwa na viashiria vya utakatishaji fedha.

“Hatuwezi tukasema ni maduka mangapi, lakini kwa kuangalia ni maduka mengi yalihusika katika utakatishaji huo wa fedha kwasababu Dar es Salaam ilihusisha maduka 87.

“Kwa mfano maduka yaligundulika kutumia fedha nyingi za Tanzania kununua fedha za kigeni, lakini fedha ndogo za kigeni kulikuwa hakuna taarifa ya fedha za kigeni zilizobaki,” alisema.

Jambo lingine lililotikisa ni BoT kuzifutia leseni ya kufanya biashara benki tano na kuziweka chini ya ufilisi.

Taarifa ya Mei, 2018 iliyotolewa na BoT ilizitaja benki hizo kuwa ni Covenant Bank For Women (Tanzania) Limited, Efatha Bank Limited, Njombe Community Bank Limited, Kagera Farmers’ Cooperative Bank Limited na Meru Community Bank Limited.

Hatua nyingine ambayo ilichukuliwa na BoT wakati wa uongozi wa Profesa Luoga ni kutangaza nia ya Serikali kuhakikisha sekta ya benki nchini inakuwa na benki chache zinazofanya vizuri katika kipindi chake cha miezi 62, benki nyingi zimewekwa chini ya uangalizi wa Benki Kuu na nyingine ziliunganishwa na benki nyingine ili kuongeza ufanisi.

Miongoni mwa mifano hiyo ni Novemba 2020, BoT ilichukua usimamizi wa China Commercial Bank Limited, Profesa Florens Luhoga alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya kubaini benki hiyo ina upungufu mkubwa wa mtaji kinyume na matakwa ya sheria ya mabenki na taasisi za fedha ya mwaka 2006 na kanuni zake.

Katika kipindi hichohicho benki nyingi ziliunganishwa, Benki M na Azania, Twiga na Posta, lakini pia wakati wa utawala wake Luoga Benki ya Exim ilifanikiwa kuzinunua benki mbili ambazo ni FNB na UBL na mifano mingine mingi.

Hatua ya hivi karibuni kabla ya kuondoka ofisini ni Desemba 12, 2022 BoT ilipotangaza kusimamisha menejimenti na kuivunja bodi ya wakurugenzi wa Benki ya Yetu Microfinance kwa kile ilichoeleza kuwa ni sababu ya upungufu mkubwa wa mtaji wa ukwasi.

BoT ilisema imeiweka benki hiyo chini ya uangalizi wake, ili kulinda haki za wateja na wadau wengine, hatua ambayo ilianza mara moja na kutarajiwa kudumu kwa siku zisizozidi 90 kabla ya kutoa majumuisho.

Miongoni mwa masuala ambayo mtaalamu huyo wa sheria za kodi anaweza kupongezwa ni kusimamia lengo la Serikali la kuhakikisha riba za mikopo inayotolewa na benki za kibiashara na taasisi za fedha inapungua na kuwa tarakimu moja, ameondoka bila kufanikiwa hilo lakini hatua kubwa ilipigwa.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imekuwa ikisisitiza lengo lake ni kuona taasisi za kifedha, ikiwemo benki zinatoa mkopo kwa wananchi kwa riba isiyozidi asilimia 9.

Ili kufanikisha hilo, BoT ilichukua hatua mbalimbali kwa kupunguza riba zake kwa benki za kibiashara, hatua ya mwisho iliyochukuliwa ilikuwa ni kupunguza riba kutoka asilimia tisa hadi saba, lengo ni wafanyabiashara wadogo, wananchi wa kawaida, wafanyakazi na sekta binafsi za biashara zitapata fursa ya kukopa.

Julai 2021 BoT ilianzisha mfuko maalumu wenye thamani ya Sh1 trilioni wa kukopesha benki na taasisi za fedha, ili ziweze kuikopesha sekta binafsi. Mfuko huu uliweka riba ya asilimia tatu, ili nazo zikopeshe sekta binafsi kwa riba isiyozidi asilimia 10 kwa mwaka.

Vilevile Profesa Luoga katika kipindi cha uongozi wake ameweka rekodi ya mfuko wa akiba ya fedha ya kigeni kutuna zaidi na kupungua zaidi.

Oktoba 2021, akiba ya fedha za kigeni ilifikiwa kiwango cha kuweza kuagiza bidhaa za nje kwa kipindi cha miezi 7, kiwango ambacho hakijafikiwa kwa zaidi ya miaka 17 iliyopita, kiwango hicho kilifikia dola bilioni 6.7 (Sh15.6 trilioni).

Oktoba 2022, kiwango cha akiba ya fedha za kigeni kiliweka rekodi nyingine ya kufikia kiwango cha chini ambacho kilifikia Dola bilioni 4.96 (Sh11.5 trilioni) ambazo zinatosha kuagiza bidhaaa za nje kwa kipindi cha miezi 4.2.

Kulingana na uchambuzi uliofanywa na gazeti hili kwa kuzingatia takwimu za BoT, ulibaini kiwango hicho kilikuwa cha chini kuwahi kufikiwa kwa kipindi cha miaka mitano nyuma, kipindi cha miezi 4.2 ni chini ya kiwango cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) cha miezi 4.5 na SADC cha asilimia 6.

Jambo jingine ni kukosa uadilifu na upungufu wa udhibiti ndani ya BoT ambako kulisababisha hasara ya Sh3.99 bilioni kwa noti ambazo hazikuwa na vigezo vya kuwa chakavu kati ya Januari 2019 hadi Septemba 2019.