Mbinu za kibunifu Sabasaba zavutia watembeleaji

Muktasari:
- Maonyesho ya 49 ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maarufu Sabasaba yalianza Juni 28 mwaka huu na yanatarajia kukamilika Julai 13 mwaka huu.
Dar es Salaam. Wakati kilele cha Maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba, kikitarajiwa kufanyika kesho Julai 7, mabanda yameongeza kasi ya kuvutia wageni kwa mbinu mbalimbali za kibunifu.
Idadi ya watembeleaji imeendelea kuongezeka tangu siku ya kwanza huku wapigangoma, matarumbeta, wachekeshaji, mangongoti, bendi, wanenguaji na wasanii ni miongoni mwa watu waliopo katika kila banda.
Watu waliovalia mavazi yanayowakilisha wanyama fulani kama sokwe mbali na kuvutia wateja wa mabanda waliyowekwa, nao walikuwa wakiendelea kujipatia kipato kwa watu waliotaka kupiga picha kwa kulipia Sh1,000.
Maonyesho haya yaliyoanza Juni 28, 2025 yana jumla ya washiriki 3,887 wa ndani na nje huku kampuni 386 za kimataifa zikishiriki kutoka nchi 23.
Yanatarajiwa kuzinduliwa Julai 7 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Muungano, Dk Hussein Ali Mwinyi.
Pia, ipo siku maalumu kwa ajili ya uzinduzi wa nembo ya ‘Made in Tanzania’ unaotarajiwa kufanywa na Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko.
Katika kitu cha tofauti mwaka huu ni Tamasha la Sabasaba linaloratibiwa na Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo ambalo kwa sasa huenda ndiyo eneo linaloongoza kukusanya watembeleaji wengi.
Ndani ya kijiji hicho cha wizara, wadau mbalimbali wamekusanywa wakiwamo wasanii wa filamu wenye biashara mbalimbali, washonaji, makundi mbalimbali ya burudani ikiwemo wachekeshaji, vyombo vya habari.
Mbali na uwepo wao, eneo hilo muda wote linatoa burudani za wasanii wa muziki ikiwamo Singeli, bongo fleva, hiphop jambo ambalo limefanya watembeleaji kukaa muda mrefu wakishuhudia burudani za wasanii wanaowapenda.
Hali hiyo imefanya viti vinavyowekwa eneo hilo kutotosha hali inayofanya watu wengi kuendelea kusimama na kufurahia burudani wanayoitaka.
Tofauti na maeneo mengine ambayo shughuli zinafanyika hadi saa mbili za usiku, eneo hili ni kati ya lile lililopewa kibali cha kufanya shughuli zake hadi saa sita usiku, hivyo kutoa nafasi ya watu ambao hawakupata nafasi ya kufika mchana kufika usiku.
“Natamani usiku ndiyo wasanii wangekuwa wanapanda jukwaani ili kuwapa watu sababu ya kutembelea eneo hili si mchana tu hadi usiku, hii utasaidia watu kujua kuwa maonyesho si mchana tu hadi usiki,” amesema Kaisiki Mkinga.
Maneno yake yaliungwa mkono na Mussa Hassan aliyetaka tamasha hilo kufanywa kuwa moyo wa Maonyesho ya Sabasaba litafanya wasanii wa ndani kutambulika zaidi kimataifa kupitia nchi wanachama zinazoshiriki.
“Litangazwe kwa nguvu zote, watu wanapenda wasanii, kadri idadi ya watu watakavyotaka kuwaona wasanii itakavyokiwa kubwa ndiyo maonyesho yatapata watembeleaji wengi zaidi, watu wakija pia watalipa kiingilio na hawatatoka mikono mitupu kwani watanunua bidhaa,” amesema Hassan.
Wakati kuletwa kwa usafiri wa pikipiki za magurudumu matatu na magari ya kutembeza wageni yanayotumia umeme yakifanyika kwa mara ya kwanza, gari kubwa mfano wa basi linazungusha wageni lageuka kivutio.
Basi hilo linalobeba zaidi ya watu 20 limekuwa likizungusha wageni uwanja mzima kwa nauli ya Sh5,000 kwa wale wasiopenda kutembea au wanaotamani kulipanda.
Basi hilo la utalii, limegeuka kuwa lulu kwa kuwa, kila linapopita watu wanalitazama na waliokuwa ndani yake walirekodi kile kinachoendelea nje.
Mmoja wa waliopanda gari hilo, Shabaha Khamis amesema ni uzoefu ambao hakuwahi kuupata.
“Mabasi kama haya huwa tunayaona nchi za wenzetu kama wakiwazungusha watalii kuangalia mji wao, ni mwanzo mzuri kulitumia hapa Sabasaba nadhani ifike wakati litumike kwa utalii wa Dar es Salaam na sehemu kama Zanzibar linaweza kutumika,” amesema Shabaha.