Bodi ya Korosho kutembelea maghala mikoa ya kusini

Wakulima wa zao la korosho waliopata mafunzo wakiwa kwenye picha ya pamoja na wataalamu wa kilimo. Picha na Bahati Mwatesa
Muktasari:
- Bodi ya Korosho Tanzania imesema kuwa itapita kwenye Amcos zote zilizopo mikoani ya Kusini pamoja na maghala makuu ili kukagua korosho zote zenye ubora.
Lindi. Tafiti zilizofanywa na Bodi ya Korosho nchini kwenye soko la dunia, zimebaini kuwa kuna uhitaji mkubwa wa korosho ghafi ambazo zinatakiwa kuwa na ubora wahali ya juu, korosho zinazotakiwa ubora wake kuanzia paundi hamsini na kuendelea.
Akizungumza jana Jumamosi Oktoba 21, 2023 kwenye mnada wa kwanza wa ununuzi wa zao la korosho, Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho nchini, Francis Alfred amesema kuwa kutokana na uhitaji wa korosho ghafi kupitia soko la dunia, Bodi ya Korosho nchini imeamua kukagua Amcos zote zilizopo mikoa ya Kusini na vyama pamoja na maghala makuu ilikuweza kuhakiki ubora wa korosho kutokana na soko lililopo.
Alfred amesema kuwa korosho zinazotakiwa ubora wake kuanzia paundi hamsini, ambapo Chama Kikuu cha Lindi Mwambao korosho zake zipo kwenye wastani huo wa paundi hamsini, ambapo amesema kuwa Amcos ambayo haitazingatia ubora wa korosho wataifungia.
"Tunaanza kutembelea na kukagua Amcos zote zilizopo mikoa ya Kusini ili kuangalia ubora wa korosho, kupitia kwenye maghala ili kuhakikisha korosho zote zinazoingia sokoni zinakuwa na ubora na endapo Amcos yoyote itakiuka maagizo hayo tutaifungia," amesema Alfred.
Mkuu wa Wilaya ya Kilwa akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Christopher Ngubiagai amewataka wakulima kuwa makini katika kuandaa korosho kuanzia shambani na kuzikausha ili korosho iwe na ubora na kupata bei nzuri. Pia amewataka wakulima wasibabaishwe na banki ndogo ndogo zinazojitokeza wakati wa msimu wa korosho ambapo kumekuwa na benki ambazo siyo waaminifu na kuwadhulumu wakulima fedha zao.
"Wakulima niwaombe mjitahidi kuwa na korosho zenye ubora ilikuweza kupata bei nzuri ya soko, pia kuna benki ambazo zinajitokeza wakati wa msimu niwaombe msibabaishwe nazo kwani benki zingine siyo waaminifu wanawaibia wakulima,” amesema.
Mkulima wa zao la korosho, Hadija Mwamba amesema kuwa bei walizopata leo zinatia moyo tofauti na mwaka jana, ambapo amesema bei inapokuwa nzuri, na wao wanapata nguvu ya kulima ila bei zinaposhuka wanakatishwa tamaa ya kulima tena.
"Bei izidi kupanda kwani bei ya mwaka jana ilikatisha tamaa, lakini kwa mwaka huu inaleta matumaini, maana bei inapokuwa nzuri hata mkulima unapata matumaini ya kuendelea kulima,” amesema Hadija.
Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Lindi Mwambao kinachojumuisha Wilaya tatu, ikiwemo Wilaya ya Lindi, Wilaya ya Kilwa pamoja na Halmashauri ya Mtama Nurdin Swallaa amesema kuwa zaidi ya tani 1,889 zimeuzwa katika mnada wa kwanza ambapo bei ya juu ikiwa Sh2,000 na bei ya chini Sh1,900.
Mkoa wa Lindi umefanya Mnada wake wa kwanza kupitia Chama Kikuu cha Ushirika Lindi Mwambao katika Kata ya Tulieni, Manispaa ya Lindi na jumla ya wanunuzi 30 walijitokeza kununua korosho hizo.