Rekodi zipo hivi Abigail Chams akiwania BET 2025

Muktasari:
- Abigail Chams anayefanya vizuri na wimbo wake, Me Too (2025) akishirikiana na Harmonize, ametajwa kuwania kipengele cha ‘Best New International Act’ akichuana na wenzake 10 kutoka mataifa matano tofauti.
HATIMAYE Tanzania imepata mwakilishi tena katika tuzo za BET baada ya kukosa kwa misimu mitatu mfululizo, Abigail Chams ndiye ametajwa kuwania tuzo hizo kubwa za muziki duniani kwa mwaka huu ikiwa ni mara yake ya kwanza.
Abigail Chams anayefanya vizuri na wimbo wake, Me Too (2025) akishirikiana na Harmonize, ametajwa kuwania kipengele cha ‘Best New International Act’ akichuana na wenzake 10 kutoka mataifa matano tofauti.
Washindani wake ni Ajulicosta, Amabbi (Brazil), Dlala Thukzin, Maglera Doe Boy, TxC (Afrika Kusini), Dr Yaro, Merveille (Ufaransa), kwn, Odeal (Uingereza) na Shallipopi (Nigeria).
Msanii wa mwisho wa Tanzania kuwania BET ni Diamond Platnumz ambaye 2021 alitajwa kipengele cha ‘Best International Act’ akichuana na Wizkid, Emicida, Headie, Aya Nakamura, Young T & Bugsey, Youssoupha na Burna Boy aliyeibuka mshindi.
Na Diamond, mwanzilishi wa WCB Wasafi, ndiye mwanamuziki Bongo aliyewania tuzo hizo mara nyingi zaidi (2014, 2016 & 2021) ila kwa bahati mbaya hajawahi kushinda hata mara moja!.
Rapa Kendrick Lamar aliyetikisa na ngoma yake, Not Like Us (2024) ndiye msanii aliyetajwa kuwania vipengele vingi msimu huu vikiwa ni 10, akifuatiwa na Doechii, Drake, Future na GloRilla ambao wote wamepata vipengele sita.

Tuzo zinatarajiwa kutolewa Juni 9, 2025 katika ukumbi wa Peacock huko Los Angeles, Marekani na kushereheshwa na mchekeshaji, Kevin Hart akipokea kijiti hicho kutoka kwa mwigizaji Taraji P. Henson ambaye amefanya hivyo misimu ya hivi karibuni.
Pia tuzo za mwaka huu zinaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 25 ya BET, tuzo zinazoandaliwa na Black Entertainment Television (BET) tangu Juni 19, 2001 zikilenga kusheherekea mafanikio ya watu weusi katika sanaa ya muziki, uigizaji na michezo.
Mwaka 2010 ndipo BET walianza kujumuisha wasanii kutoka Afrika katika tuzo zao kupitia kipengele cha ‘Best International Act; Africa’ ambacho 2018 kilifanyiwa mabadiliko na kuwa ‘Best International Act’ kikihusisha wasanii wote kutoka nje ya Marekani.
Abigail Chams anachaguliwa BET wakati wimbo wake, Mee Too (2025) ukiendelea kufanya vizuri, huu ndiyo wimbo pekee kutoka Tanzania ambao umesikilizwa mara nyingi zaidi (most streamed) katika mtandao wa Spotify kwa mwaka huu.
Video yake ambayo imeongozwa na Director Kenny, tayari imetazamwa zaidi ya mara milioni 10 YouTube ikiwa ni miezi miwili tangu itoke na ni video ya kwanza Tanzania iliyotoka mwaka huu kufikia namba hizo tena kwa kipindi kifupi.
“Kutoka kwa msichana anayeishi kwa ajili ya muziki, hii ni ndoto iliyogeuka kuwa kweli kwangu. Ningependa kuwashukuru wote mlioshiriki kwa ukaribu katika safari yangu. Me Too ni wimbo mkubwa zaidi nchini kwenye mitandao yote,” alisema Abigail Chams.

Mafanikio hayo ya Abigail Chams yanakuja ikiwa ni miaka mitatu tangu kusainiwa na menejimenti ya RockStar Africa na baadaye lebo kubwa duniani, Sony Music Entertainment Africa, dili ambalo limebadili muziki wake kwa sehemu kubwa.
“Malengo yangu ni kupeleka Bongo Fleva, muziki wa Kitanzania kimataifa zaidi na sasa hivi natazama tuzo za BET na Grammy, nawaza kuzipata kwa miaka ijayo, kwa sababu ziko hapo kwenye malengo na nina amini nitazipata,” alisema baada ya kusainiwa Sony Music.
Abigail Chams aliyevuma zaidi na wimbo, Nani? (2023), ukiachana uimbaji wake, ni kati ya wasanii wachache Bongo wenye uelewa mkubwa wa muziki, huyu alianza kujifunza kupiga piano akiwa na umri wa miaka mitano na hadi sasa anajua violini, gitaa n.k.
Ikiwa atashinda BET msimu huu, Abigail Chams atakuwa msanii wa pili kutoka Tanzania kufanya hivyo baada ya Rayvanny kushinda 2017 akiwa ni msanii wa pili kwa Afrika Mashariki baada ya Eddy Kenzo wa Uganda kushinda 2015.
Ikumbukwe msimu uliopita Tyla kutokea Afrika Kusini alishinda tuzo mbili za BET 2024 kama ‘Best New Artist’ na ‘Best International Act’ akiweka rekodi kama msanii wa kwanza Afrika kushinda vipengele viwili kwa usiku mmoja.
Vile vile mkali huyo wa kibao, Water (2023), alikuwa msanii wa tatu ambaye hakuzaliwa Marekani kushinda kipengele cha ‘Best New Artist’, wengine ni Nicki Minaj aliyezaliwa Trinidad na Sam Smith aliyezaliwa Uingereza.
Hadi sasa Wizkid na Burna Boy kutoka Nigeria ndio wasanii vinara Afrika kushinda tuzo nyingi za BET, wote wameshinda mara nne ila Wizkid kuna moja alishinda kupitia kolabo na Beyonce, Brown Skin Girl (2019) iliyoshinda kipengele cha HER Award 2020.

HER Award ni tuzo maalumu kwa nyimbo zinazotia moyo na kuwawezesha wanawake, ilianza kutolewa 2006 ikitambulika kama BET J Cool Like That, huku Beyonce na Mary J. Blige wakiwa ndio wasanii walioshinda mara nyingi kipengele hicho.
Mwanachama wa zamani wa kundi la Destiny’s Child lililotamba na nyimbo kama Say My Name (1999) na Survior (2001), Beyonce ndiye msanii aliyeshinda tuzo nyingi zaidi za BET kwa muda wote ambazo ni 33, huku akifuatiwa na Chris Brown aliyeshinda 19.