Mfahamu binti pekee wa Eminem aliyeolewa

Rapa Eminem, 51, wikiendi iliyopita alishuhudia ndoa ya binti yake wa pekee, Hailie Jade, 28, ambaye ameolewa na mchumba wake wa siku nyingi, Evan McClintock, 27, waliyekutana tangu wanasoma chuo.
Harusi hiyo ya watu wachache iliyohudhuriwa na familia na marafiki wa karibu ilifanyika ndani ya jumba la kifahari la Greencrest Manor huko Battle Creek nchini Marekani, huku mastaa kama 50 Cent, Dr. Dre na Jimmy Iovine wakihudhuria.
"Machozi mengi ya furaha yalimwagika, vicheko na tabasamu vilikuwepo, na upendo mwingi ulisikika. Mimi na Evan tunatoa shukrani kwa familia na marafiki wote waliosafiri na kuwa sehemu ya sura hii mpya ya maisha yetu kama mume na mke," amesema Hailie.
Utakumbuka wawili hao walichumbiana mnamo Februari 2023, baada ya kukutana kwa mara ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Michigan mnamo 2016.
Hailie alizaliwa Desemba 25, 1995, huko Detroit, Michigan, kipindi hicho Eminem alikuwa na uhusiano na mkewe, Kimberly 'Kim' Scott ambaye walikutana shule mwaka 1989 na walikuja kuachana 2001, na tangu kuzaliwa kwa Hailie Eminem hajapata mtoto mwingine.
Lakini Hailie ni mtu wa namna gani hasa?, binti huyo amehitimu Chuo Kikuu cha Michigan na kupata shahada ya Saikolojia kwa ufaulu wa GPA ya 3.9, alikuwa mwanafunzi bora tangu shule ya sekondari ya Chippewa Valley.
"Hailie amenifanya nijivunie kwa hakika, hana watoto bali mpenzi tu, yupo bize na kazi zake," alisema Eminem mnamo 2020 katika kipindi cha Hotboxin akiwa na Mike Tyson.
Kwa zaidi ya miaka miwili Hailie amekuwa akiendesha Podcast yake, Just A Little Shady, hufanya mazungumzo na rafiki na wageni. Kipindi chake cha kwanza kiliruka mwaka 2022 ambapo kilimzungumzia kama mtoto wa msanii maarufu wa Hip Hop.
Katika mahojiano yake na The Daily Mail mwaka 2018, Hailie alisema kwamba yeye na Eminem wanazungumza mara kwa mara na wako karibu sana, ila yuko karibu sana na mama yake, Kim ambaye wakati huo aliishi naye kufuatia kutengana na baba yake.
McClintock katika Podcast ya Hailie, alisema kilikuwa kipindi cha mwishoni mwa mwaka alipokutana na Eminem na kumueleza kuhusu nia yake ya kumuoa Hailie, alitaka kuweka wazi jambo hilo.
"Nilimuona baba yako akishuka katika ngazi na kuwaza kama napaswa kufanya hili sasa hivi au kupanga muda mwingine, nilimfuata tu pale chini na nashukuru nilimkuta hapo akinunua keki," alisema McClintock.
Utakumbuka Eminem ambaye alivuma zaidi kimuziki baada ya kusainiwa Aftermath Entertainment (1998) na Dr. Dre, ni miongoni mwa wasanii waliuza zaidi duniani kwa muda wote akiwa ameuza rekodi takribani milioni 220 na kushinda tuzo 15 za Grammy.