Lil Ommy na rekodi zake katika utangazaji

Muktasari:
Ameshinda tuzo kama African Entertainment Awards USA (AEAUSA) 2019 (Marekani) kama Mtangazaji Bora wa Mwaka, Star QT Awards 2020 (Afrika Kusini) kama Mtangazaji Bora Afrika, Zikomo Awards 2021 (Zambia) kama Mtangazaji Bora Afrika n.k.
Kwa miaka sasa jina la Omary "Lil Ommy" Tambwe limekuwa maarufu nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla katika tasnia ya utangazaji huku akijinyakulia tuzo za kimataifa mara kwa mara. Hii inatokana na umahiri wake kwenye kazi hiyo.
Utakumbuka kabla ya kujiunga na Wasafi Media yake Diamond Platnumz hapo Machi 2020, Lil Ommy alikuwa Times FM ambapo alipata umaarufu kupitia kipindi chake cha ‘The Playlist’.
Lil Ommy anayetangaza vipindi vya ‘The Switch’ (Wasafi FM) na ‘Big Sunday Live’ (Wasafi TV), ana rekodi nzuri ya kushinda tuzo za kimataifa katika kazi yake.
Ameshinda tuzo kama African Entertainment Awards USA (AEAUSA) 2019 (Marekani) kama Mtangazaji Bora wa Mwaka, Star QT Awards 2020 (Afrika Kusini) kama Mtangazaji Bora Afrika, Zikomo Awards 2021 (Zambia) kama Mtangazaji Bora Afrika n.k.
Diamond katika wimbo wake, Oka (2022) akimshirkisha Mbosso, Lil Ommy ni miongoni mwa watangazaji waliorushwa katika ngoma hiyo kutoka katika EP yake, ‘First of All’ (FOA).
Akizungumza na gazeti hili, Lil Ommy amesema ni vigumu kueleza ni kipi hasa kilichopo nyuma ya mafanikio hayo, Kwa sababu waandaji wenyewe wa tuzo hizo hasa AEAUSA ni mara chache wanaweka wazi vigezo zilivyopelekea kumchagua mshiriki.
"Wale jamaa hawakuambii kwa nini wamekupekesa na umeshinda kwa vigezo gani, unashangaa tu tuzo hii hapa.
“Ninachojua huwa wanafanya utafiti hasa kwenye mitandao, wakiangalia watu wanakuzungumziaje hasa wasanii na mashabiki." amesema Lil Ommy.
Hata hivyo, Lil Ommy amesema kufanya mahojiano na wasanii wakubwa wa kimataifa kunaweza kuwa kumechochea hilo kwa kiasi kikubwa.
“Pia kwenye kazi yangu nachanganya lugha kuna wakati analazimika kutumia Kiingereza iwapo staa ni wa nje na hajui Kiswahili.
Licha ya mafanikio hayo, bado anakumbuka kuikosa tuzo kutokea African Muzik Magazine Awards and Music Festival (AFRIMMA) (Marekani), iliyochukuliwa na mtangazaji wa Kenya, Willy M Tuva anayetangaza Citizen Radio katika kipindi cha ‘Mambo Mseto’.
"Na mimi mwaka 2019 kwa kweli nilitamani nichukue tuzo zote tatu, lakini unapopanga na Mungu naye anapanga, ila ni kuwa huwezi kupata na kukosa vyote." amesema Lil Ommy.
Ikumbukwe tuzo hiyo ya AFRIMMA, Lil Ommy na Tuva walikuwa wakichuana na watangazaji wengine wakali kutoka Afrika kama Do2dtun (Nigeria), Yaw na Afonso Quintas (Angola), Sammy Forson (Ghana), James Onen (Uganda), Dj Fresh (Afrika Kusini) na Konnie Toure (Ivory Coast).
Ukiachana na tuzo, Lil Ommy ana rekodi ya kuwa mtangazaji wa kwanza kutoka Tanzania kuachia Playlist yake ndani ya jarida la mtandao mkubwa wa kusikiliza muziki duniani, Apple Music.
Amesema kufanya mahojiano na Rapa wa Afrika Kusini, Nasty C na wakali wengine kulichochea hilo kwa kiwango fulani.
Mathalani, Nasty C anafanya kazi na Def Jam Recordings tawi la Afrika na Apple Music ya Afrika Kusini, hivyo ni rahisi kwa Apple Music kumuona yeye kwa sababu amefanya kazi na staa huyo.
"Kwa mfano Tiwa Savage kasainiwa Universal Music Group (UMG), na wasanii wakubwa wanaposaniwa lazima Apple Music wawepo, sasa wakikuta Tiwa ambaye wamemsaini kakuamini hadi mkafanya mahojiano ina maana una kitu.
"Wanaanza kukufuatilia. Je, mahojiano yalifanikiwa kiasi gani?, wakichunguza zaidi wanagundua wasanii wenyewe ndio wanakuwa wanaomba kufanyiwa mahojiano, hapo lazima wakutafute." amesema Lil Ommy.
Pia amesema kutokea kwenye majarida makubwa Afrika kama Tash Magazine kumemtangaza zaidi kimataifa.
Mwaka 2019 alikuwa mtangazaji pekee kutoka Tanzania kufanyiwa mahojiano na jarida hilo, huku msanii wa Bongofleva, Vanessa Mdee naye akitokea pia.
"Hayo majarida yana nguvu sana, unajua kule wenzetu wanadhamini sana majarida, na nililishikia sana bango hili jarida hadi Vanessa Mdee akaniuliza kwa sababu tulitokea mimi na yeye, na matokea yake yakawa makubwa." amesema Lil Ommy.
Katika playlist yake ndani ya Apple Music iliyoachia mwishoni mwa mwaka 2020 ilikuwa na nyimbo 30, na 13 kati hizo zilitokea Tanzania.
Nyimbo hizo ni ‘Cheche’ wa Zuchu, ‘Jeje’ wa Diamond, ‘Sina Nyota’ wa Mbosso, ‘Sexy Mama’ wa Lava Lava, ‘Tetema’ wa Rayvanny, ‘Gwiji’ wa Mwana FA, ‘Kata’ wa Ommy Dimpoz, ‘Gusanisha’ wa G Nako, ‘Sio Mbaya’ wa Jux, ‘Magical’ wa Navy Kenzo, ‘Tikisa’ wa Marioo, ‘Dangerous’ wa Joh Makini na ‘Till I Die’ wa Conboi.
Pia wasanii wa Afrika Mashariki ambao nyimbo zao ziliingia katika playlist hiyo ni Femi One, Sauti Soul, Willy Paul, Khaligraph Jones, Masuati na Nadia Mukami.