Hili hapa vazi lililoshinda Tamasha Samia Festival

Muktasari:
- Tamasha hilo lilikuwa na majaji watatu wakiogozwa na Jaji Mkuu Millen Magese, Jokate Mwegelo na Idrisa Sultan, likiwashirikisha wabunifu tisa na kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, mabalozi na wasanii.
Unguja. Wakati Tamasha la Samia Fashion likifanyika Zanzibar, serikali imesema licha ya sekta ya fasheni kuwa muhimu lakini ilikuwa haijaitambua hivyo imeamka na kuanza kuchangamkia fursa zilizopo sio tu kuwaendeleza wabunifu, bali kukuza uchumi wa taifa hilo.
Tamasha hilo ambalo limeandaliwa na Khadija Mlimboka limefanyika usiku wa kumkia leo Desemba Mosi, 2024 Mjini Unguja likiwashirikisha wabunifu tisa kutoka Zanzibar na kuhudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali, mabalozi, wasanii maigizo na wabunifu.
Akizungumza katika tamasha hilo, Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo, Tabia Mwita Maulid ameweka wazi kwamba serikali ilikuwa bado imeyaweka kando masuala hayo licha ya kuwa na fursa na mchango kwenye uchumi.
“Wizara ilikuwa haijafanya kitu katika hili , lakini tumeona umuhimu wake na sisi tunajipanga sasa, wabunifu wote walioshiriki katika tamasha hili watachukuliwa na kuwaangalia namna ya kuwawezesha zaidi,” amesema na kuongeza.
“Kwa kweli hili ni jambo zuri tumeona namna ambavyo linaweza kuleta mabadiliko makubwa, tunaomba waandaaji wakati mwingine mtushirikishe mapema na serikali itaweka bajeti maalumu kwa ajili ya kugharamia tamasha hili,” amesema.
Naye Waziri Nchi Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff amesema sekta ya fasheni ni muhimu lakini Zanzibar walikuwa hawajaitambua.
“Leo tunaona mambo makubwa katika sekta hii, kuna ajira, ubunifu na kuna fursa kubwa za kukuza uchumi wetu, tunaenda kulichukulia jambo hili kwa umakini mkubwa sana,” amesema.
Amesema kupitia wizara yake chini ya Wakala wa Kuwezesha Wananchi Kiuchumi kuna mikopo inayotolewa hivyo kuwataka wabunifu hao wajitokeze kupata mikopo hiyo kuendeleza vipaji vyao.
Naye Jaji Mkuu wa tamasha hilo, Milleni Magese pamoja na mambo mengine, amempa mshindi wa tamasha hilo Sh 3 milioni huku akimuahidi kumuendeleza zaidi.
Amesema amebaini Zanzibar kuna vipaji vya ubunifu na kuiomba serikali iwatumie vijana hao katika matangazo na mambo mengine ya kuitangaza nchi badala ya kutumia watu kutoka nje.
Akizungumzia tamasha hilo, Mwanamitindo huyo amesema tukio hilo sio tu ni sherehe ya mitindo lakini ni safari ya ushindi, heshima, ubunifu na urithi kwa Watanzania.
“Hii inachangia alama inaacha historia, hili vazi la Samia ni zaidi ya vazi ni ishara ya utumishi, stara na inayobeba maana kubwa ya mwanamke wa kwanza kuwa Rais nchini Tanzania ikiwa ni utambulisho kamili, amesema.
Amesema vazi hilo linawakilisha mchanganyiko wa kipekee kuonesha Watanzania ufahari wetu kwamba tunaweza kuwa wabunifu bila kupoteza asili, maadili na utamaduni wetu, vazi hili linaonyesha jinsi tunaweza kuvuka mipaka ya nchi lakini bado tukaendelea kuwa na utamaduni wetu na ubunifu wa wanamitindo.
Hii sio tamasha bali ni fursa ya kuandika historia, tunajivunia kua sehemu ya tukio ambalo litatoa mabalozi wataiwakilisha Tanzania duniani.
Naye mwanzilishi na muandaaji wa tamasha hilo, Khadija Mwanamboka amesema lilianza Oktoba Dar es Salaam kwa vijana wakiwashikisha watoto lakini wakaona washirikishe wabunifu kutoka Zanzibar lengo la tamasha hilo ni kusherehekea na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupenda tasnia ya michezo.Amesema mchakato ulikuwa mkubwa lakini mwishowe walipata watu watakaoshiriki.
“Tamasha lingine litafanyika Desemba ambapo litawashirikisha wabunifu kutoka Zanzibar maeneo mengine ili kuwashindanisha kwa pamoja,” amesema
Elizabert Petro ambaye ni mshindi wa shindano hilo amesema “namshukuru Rais Samia kuanzisha fursa hii mimi ni mara yangu ya kwanza kushiriki lakini nimeshinda, sikutegemea kwa sababu watu walikuwa wengi lakini bahati imekuja kwangu,”