Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Danadana kulipata vazi la Taifa mwisho lini?

Muktasari:

  • Utakumbuka mchakato wa kulipata vazi hilo ulinza mwaka 2004, na Desemba 22, 2011, kamati maalum ya kutafuta vazi hilo iliteuliwa rasmi na Dk Emmanuel Nchimbi akiwa ndiye Waziri mwenye dhamana kwa kipindi hicho.

Dar es Salaam. Tangu kuanzishwa kwa mchakato wa kulipata vazi la taifa hadi sasa ni mwaka wa 21, huku wakiwa tayari wamepita mawaziri 10 kwenye Wizara ya  Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, bila ya vazi hilo kupatikana.

Utakumbuka mchakato wa kulipata vazi hilo ulinza mwaka 2004, na Desemba 22, 2011, kamati maalum ya kutafuta vazi hilo iliteuliwa rasmi na Dk Emmanuel Nchimbi akiwa ndiye Waziri mwenye dhamana kwa kipindi hicho.

Kamati hiyo iliundwa ndani yake ikiwa na watu nane akiwemo Mwenyekiti Joseph Kusaga na Katibu wake Angela Ngowi na Wajumbe wakiwa Habib Gunze, Joice Mhaville, Mustafa Hassanali, Makwaia Kuhenga, Ndesambuka Merinyo na Absalom Kibanda ambaye baadaye alitangaza kukaa kando kwenye kamati hiyo.

Hata hivyo mwaka 2012 baada ya mabadiliko ya baraza la mawaziri kamati hiyo ikiongozwa na Angela Ngowi akiwa na Wajumbe Joyce Mhaville, Mustafa Hassanali na Ndesambuka Merinyo waliwasilisha ripoti ya vazi hilo kwa Waziri Mkangara akiwa na Naibu wake Amos Makalla. Ambapo Kamati ilikabidhi michoro sita kutoka katika 200 iliyowasilishwa na wasanii mbalimbali.

Licha ya hayo kamati hiyo ya awali ilivunjwa na kuundwa mpya Julai 20,2022 ikiwa chini ya mwenyekiti Profesa Hermas Mwansoko, Katibu akiwa Dk Emmanuel Temu, na Wajumbe Chifu Sangali, Hadija Mwanamboka, Mustafa Hasanali, Mrisho Mpoto, na Masoud Ally (Kipanya).

Januari 31,2023 neema ya kupatikana kwa vazi hilo ilianza kurudi tena kwa wananchi wanaosubiri kwa hamu, baada ya Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) Dk Kedmond Mapana aliposema Februari 3,2023 watakabidhi ripoti ya muundo wa vazi hilo kwa serikali baada ya mchakato wa kulitafuta uliofanyika kwa miaka kadhaa.

Si hivyo tu Februari 7, 2024, Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma wakati akijibu swali la Antipas Mgungusi Mbunge wa Malinyi, lililohoji juu ya upatikanaji wa vazi hilo, alisema Kamati ya Kitaifa ya Kuratibu upatikanaji wa vazi la taifa imefanikiwa kukukusanya maoni kutoka kwa wadau na wananchi 20452 kutoka mikoa yote ya Tanzania bara na visiwani.

Alisema hatua iliyofikiwa kwa sasa kamati itakutana na kuwashindanisha wabunifu wa mavazi kutoka pande zote mbili za muungano ili wale watakaokuwa washindi kwa upande wa wanaume na wanawake mavazi yao ndiyo yatapendekezwa kuwa vazi la Taifa.

“Wabunifu hao watafanya kazi kwa kutumia maoni na mapendekezo yaliyotolewa na wadau na wananchi ili kukamilisha mchakato wa vazi la taifa kwa ufanisi na haraka zaidi. 

Tumetumia njia hii ili kuharakisha mchakato na kupunguza uhitaji wa matumizi fedha nyingi za uratibu wa upatikanaji wa vazi la taifa,”alisema Hamis Mwinjuma.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kuratibu upatikanaji wa vazi la taifa Prof. Hermas Mwansoko, wakati akizungumza na Mwananchi ametoa maana ya vazi la taifa kwa kusema ni moja ya vitambulisho.

“Vazi la taifa ni moja ya vitambulisho vya taifa, kama likivaliwa, watu wengine hawatojiuliza huyu mtu ni wa taifa gani. Akivaa atajulikana kuwa ni Mtanzania popote alipo. Ni kama ilivyo kwa wanachama wa Chadema.

“Akivaa ‘kombati’ anajulikana moja kwa moja kuwa ni Chadema au kijani anatambulika kuwa ni CCM. Vitambulisho vya mtu ni vingi inaweza kuwa lugha, vazi, chakula kwa hiyo nalo ni kitambulisho,” anasema Mwansoko.

Hajaishia hapo, anasema vazi la taifa mara nyingi linakuwa mjadala kwa sababau watu wanapenda lifikie hatima, anasema wao kama kamati tayari wamefanya kazi yao.

“Wangi wanapeda lifikie hatima na kamati inafanya mchakato tu. Lakini uamuzi wa mwisho ni serikali, sisi tumeshafanya kazi yetu tumefanya mahojiano tutoe mapendekezo lakini bado hatujafika hatua ya mwisho ya mapendekezo hayo kukabidhi serikalini na ndicho kinachosubiriwa uamuzi ni wa serikali na siyo sisi,” anasema.

Kwa upande wake Mwanamitindo, Ally Remtullah anasema kwa sasa  ni ngumu kushawishi watu kuvaa vazi la taifa, lakini ni vyema kutumika kwenye shuguli kama bungeni au watu wakisafiri nje ya nchi kama timu ya taifa.

Anasema kwa upande wake anaona kanga ingefaa zaidi kuwa vazi la taifa sababu inatoka Tanzania 

“Vazi la Taifa kwa mimi nadhani kanga ipo na imetoka Tanzania ukiangalia msichana yeyote akienda kazini kwenye pochi yake unakuta ana kanga, mtoto akizaliwa anafungwa kanga na hata akifariki anafunikwa kanga, mimi nadhani ni kati ya vazi la taifa inabidi tuchague tu rangi iwe vazi la taifa,” anasema Remtullah.

Utakumbuka kutokana na danadana za kulipata vazi hilo  Machi 31, 2024, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alimtaka Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo wa kipindi hicho, Dk Damas Ndumbaro kuhakikisha vazi hilo linapatikana.

Agizo hilo alilitoa kwenye tamasha la Mtoko wa Pasaka akionyesha kushangazwa na kuchelewa kupatikana kwa vazi hilo, licha ya ahadi kadhaa zilizowahi kutolewa tangu mwaka 2017.

“Nilipomuona MC Eliud alipokuja hapa huwa namuona kwenye kipindi la Cheka, ni mchekeshaji wetu maarufu lakini leo ametoa ujumbe kwa Serikali, ametutaka tuanze kubuni vazi la kitaifa. Yeye amekuja alivyovaa, kavaa ameona hilo ndiyo vazi la kitaifa, nimemwambia Mheshimiwa Waziri ‘chalenji’ hiyo.

“Tulishafanya uamuzi toka mwaka 2017 kwa kuiagiza Wizara itafute Vazi la Taifa hili, na wakaahidi watatafuta katika kipindi kifupi. Toka 2017 hadi leo bado kipindi kifupi hicho? Eliud ametukumbusha tena kwamba tunahitaji kupata wazi la kitaifa, wanawake wavae vipi wanaume wavae vipi, kama umeshindwa kabisa basi tuchukue la Eliud, liwe vazi la kitaifa,” alisema Majaliwa.

Mbali na kauli hiyo iliyowahi kutolewa na Waziri Mkuu, imekuwa ikiibuka mijandala mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii. Kama ile iliyotokana na harusi ya Mwanamuziki Jux, ambapo wasanii walienda nchini Nigeria kumuunga mkono mwenzao wakiwa wamevalia mavazi ya tamaduni za Kinigeria.

Hali hiyo ilitokea awali Julai 3, 2024 baada ya wasanii wa Tanzania walipokwenda nchini Korea. Ambapo kutokana na kutokuwa na vazi la Taifa iliwalazimu kuvaa mavazi ya tamaduni za Kikorea.


Mchakato wa kulipata vazi hilo ulipofikia 

Akizungumza na Mwananchi, Afisa Utamaduni Mwandamizi, Tito Lulandala, kutoka  Kitengo cha Maadili ya Taifa, Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo anasema hakuna kilichokwamisha mchakato wa kulipata vazi hilo bali yanazingatiwa matakwa ya wananchi.

“Machakato ulianzia kwa wananchi. Serikali ilipeleka kwa wananchi katika nyakati mbili. Zoezi la kukusanya maoni kwa mara ya kwanza wadau walisema bado wanahitaji kuendelea na ukusanyaji wa maoni kwa sababu kama taifa tumebarikiwa makabila mengi.

“Kwa  hiyo tukaendelea tena kukusanya maoni kwa awamu ya pili. Awamu hiyo ilikamiliswa Januari 2025, ambapo kamati iliyokuwa ikikusanya maoni iliwasilisha kwa Waziri Palamagamba Kabudi akaipokea. Sasa serikali inachakata yale maoni yaliyowasilishwa kisha itakuja kusema nini imeamua baada ya hapo,” amesema.

Amesema serikali inaongozwa na wananchi na inasikiliza kile ambacho wananchi wanakipenda.

“Ukusanyaji wa maoni ulitumia njia kama tano,  kusambaza fomu za kutolea maoni kidijitali, kupitia mitandao ya kijamii ilifunguliwa mpaka ‘page’ ya kamati ya Vazi la Taifa, lakini kwa Zanzibar walifanya mpaka mihadhara kama mitano. Pia wameendesha mahojiano na wabunifu na wanazuoni wa utamaduni,” anasema.

Baadhi ya nchi za Afrika Mashariki zenye vazi la Taifa


Uganda

Vazi la taifa la Uganda ni “Gomesi” kwa wanawake na “Kanzu” kwa wanaume. Gomesi ni vazi la jadi la wanawake lenye muundo wa gauni na mara nyingine hupambwa kwa nakshi. Hivyo Gomesi na Kanzu ni sehemu ya utamaduni wa mavazi wa Uganda.


Burundi

Vazi la taifa la Burundi ni “Imvutano”  kwa wanawake na “Ikitenge” kwa wanaume. Imvutano hurembwa kwa rangi na michoro inayovutia. Huku Ikitenge linalofanana na vazi la kitenge pia huwa na mitindo na rangi mbalimbali. Mavazi haya umuhimu wa kipekee katika utamaduni wa Burundi na hutumiwa katika matukio maalum na sherehe nchini humo.


Rwanda

Vazi la taifa la Rwanda ni “Umushanana” kwa wanawake na “Ikitenge” kwa wanaume. Mavazi haya nchini Rwanda hutumiwa katika matukio muhimu na sherehe.