Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bongo Fleva ilivyopishana na kina Oliver Mtukudzi

Muktasari:

  • Eneo hilo dogo ni kukosekana kwa video za nyimbo husika walizoshirikiana, kuna nyimbo za Bongo Fleva ambazo ndani yake zina majina ya wasanii wakubwa kutoka nje ila ladha yake inapungua kutokana na hilo. Miongoni mwa hizo ni hizi zifuatazo.

Dar es Salaam, Haikuwa bahati kuuza nao sura, ndivyo tunavyoweza kusema kufuatia baadhi ya wasanii wa Bongo Fleva kushirikiana na wenzao wa kimataifa kama Oliver Mtukudzi lakini wakapishana katika eneo moja dogo tu ambalo lingeweza kupeleka mbali zaidi kazi hizo.

Eneo hilo dogo ni kukosekana kwa video za nyimbo husika walizoshirikiana, kuna nyimbo za Bongo Fleva ambazo ndani yake zina majina ya wasanii wakubwa kutoka nje ila ladha yake inapungua kutokana na hilo. Miongoni mwa hizo ni hizi zifuatazo.

Diamond Platnumz & Papa Wemba

Akiwa kwenye ziara yake barani Ulaya, Diamond Platnumz  alienda Paris, Ufaransa na kuingia studio na Papa Wemba kutoka Congo na kurekodi wimbo, Chacun Pour Soi (2016) ambao ulifanya vizuri pindi ulipotoka.

Licha ya kuwa ni wimbo wa Papa Wemba lakini kwa hapa nchini unachukuliwa kama wa Diamond kutokana umeshirikisha wasanii wawili kutoka nchi mbili tofauti.

Utakumbuka Papa Wemba alifariki Aprili 24, 2016 akiwa na umri wa miaka 66 baada ya kuanguka jukwaani alipokuwa akitumbuiza kwenye tamasha kubwa la FEMUA huko Abidjan, Ivory Coast, hivyo kuondoa uwezekano wa video ya wimbo huo kufanyika.

Desemba 2016, Shirika la Habari la Ujerumani, Deutsche Welle (DW) liliripoti kuwa ‘Chacun Pour Soi’ ndiyo wimbo bora na namba moja wa kufungia mwaka nchini DR Congo.

Na Juni 2017, Diamond aliachia dokumentari fupi ambayo inaonesha walivyokuwa studio wakirekodi na gwiji huyo wa muziki wa  Soukous barani Afrika. Studio kulikuwepo watu mbalimbali wa Papa Wemba, huku Diamond akiwa na Meneja wake, Sallam SK.

AY & P-Square
Rapa AY alitoa wimbo wake, Freeze (2008) akilishirikisha kundi la P-Square kutoka Nigeria ambao kwa wakati huo walikuwa juu sana kimuziki Afrika na hata walikuja nchini kufanya shoo iliyowakosha wengi.

Wimbo huo ulirekodiwa ndani ya studio za B’Hitz  na Prodyuza Hermy B, mipango yao ilikuwa baada ya kumaliza kurekodi, AY angeenda Lagos, Nigeria kwa ajili ya kufanya video yake, lakini hilo halikuweza kufanikiwa hadi wimbo unatoka.

AY kwenye mahojiano na kipindi cha Mkasi alisema kulifanyika makosa ya kutoa wimbo huu bila video kufanyika ila amekuwa akihakikisha kosa hilo halijirudii tena kwenye maisha yake ya muziki.

Ikumbukwe AY ndiye msanii wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kufanya wimbo na kundi la P-Square kisha wakafuata wengine kama Cindy Sanyu kutoka Uganda na Diamond Platnumz wa Tanzania.

P-Square, wakali wa miondoko ya Afrobeat, R&B na Dancehall, walifanya vizuri na nyimbo zao kama Temptation, Do Me, Bizzy Body, Personally, Chop My Money, Alingo, Beautiful Onyinye, Shekini, Bring it On, Gimme Dat, Roll It, Ifunanya.

Harmonize & Morgan Heritage

Katika albamu ya kwanza ya Harmonize, Afro East (2020) yenye nyimbo 18, kuna wimbo unaitwa ‘Malaika’ ambao amelishirikisha kundi la muziki wa Rege kutoka Jamaica, Morgan Heritage.
Kundi la Morgan Heritage linafahamika duniani kwa kipindi kirefu, lilianzishwa mwaka 1994 na watoto watano wa msanii wa

Reggae Jamaica, Denroy Morgan.  

Harmonize ni msanii wa pili Bongo kufanya kazi na Morgan Heritage baada ya Diamond aliyewashirikisha kwenye wimbo wake ‘Hallelujah kutoka kwenye albamu yake ya tatu, A Boy Froma Tandale (2018).

Na hadi sasa video ya wimbo ‘Malaika’ haijatoka huku Harmonize akiwa tayari ameachia albamu nyingine nne ambazo ni High School (2021), Made For Us (2022), Visit Bongo (2023) na Muziki wa Samia (2024).

Utakumbuka Morgan Heritage  kupitia albamu yao, Strictly Roots (2015) walishinda tuzo yao ya kwanza ya Grammy kwenye kipengele cha Albamu Bora ya Rege, kisha wakaja kushinda tuzo hiyo kwa mara ya pili kupitia albamu yao, Avrakedabra (2017).

Ibra Da Hustler & Loon

Baada ya Loon kutokea Marekani kuja Tanzania alikutana na Ibra Da Hustler ambaye kwa wakati huo alikuwa akifanya vizuri na kundi la Nako 2 Nako Soldiers na wakarekodi wimbo, Worldwide Bachelor (2006).

Loon alikuja Tanzania kwa ajili ya kufanya video ya wimbo wake mpya kwa wakati huo ‘Distracted’, katika video ya hiyo alishirikisha warembo wa Tanzania akiwemo Miss Tanzania na Miss World Africa 2005, Nancy Sumari.

Pia katika wimbo huo alisikika msanii mwingine kutokea Marekani, Humurak D Gritty ambaye aliongozana na Loon, huyu ndiye aliachana vesi ya mwisho ya wimbo huo.

Mikono ya Prodyuza kutoka Kenya, Ambrose Dunga wa Mandugu Digital ndiyo iliyosika kukamilisha wimbo huo uliofanya vizuri kwa kukutanisha mahadhi ya muziki wa rap na ule wa kiafrika ila kwa bahati mbaya video yake ndiyo haikutoka hadi sasa.

Ikumbukwe Ibra Da Hustler ndiyo msanii wa mwisho kujiunga Nako 2 Nako baada ya Lord Eyes kuona uwezo wake, na Ibra ndiyo aliwapa wazo la kwenda Kenya kurekodi ndipo wakakutana na Chezan Brain.

Lady Jaydee & Oliver Mtukudzi

Mwimbaji Lady Jaydee aliamua kuchanganya muziki wa Bongo Fleva na wa gwiji huyo kutoka Zimbabwe, Oliver Mtukudzi ambaye alikuwa akisifika Afrika na duniani kwa kufanya miondoko ya Afro Jazz.

Walirekodi wimbo wao, Mimi ni Mimi (2011) baada ya Oliver Mtukudzi kuja nchini kutumbuiza ambapo Jide alipata nafasi ya kuimba naye jukwaani wimbo wake wake maarufu, Neria (1991) lakini walikuwa wanafahamiana kwa miaka mingi.

Ni wazi kama ingefanyika video ya wimbo huo, Lady Jaydee angejitengezea historia kubwa zaidi kwenye Bongo Fleva kutokana uzito wa jina la Oliver Mtukudzi barani Afrika.

Utakumbuka Oliver Mtukudzi alifariki dunia hapo Januari 23, 2019 akiwa na umri wa miaka 66, hivyo kuondoa hata uwezekano wa video ya wimbo huo kuja kufanyika hapo baadaye.

Miongoni mwa nyimbo maarufu za Oliver ni ‘Neria’ ambao aliuandika kwa ajili ya kutumika katika filamu inayokwenda kwa jina hilo iliyotoka mwaka 1991 na hadi sasa inatajwa kama filamu iliyoingiza fedha nyingi zaidi nchini Zimbabwe kwa muda wote.