BET kutolewa kesho Megan, Will Smith ndani

Muktasari:
- Baadhi ya wasanii kutoka Afrika wanaowania tuzo hizo ni Burna Boy, Ayra Starr, Tems, Seyi Vibes Asake, Tyla, Focalistic, Tyler ICU, huku Drake akiwa msanii aliyetajwa kuwania vipengele vingi zaidi ambavyo ni saba.
Tuzo za BET 2024 zinatarajiwa kutolewa hapo kesho Juni 30 huko Los Angeles, California katika ukumbi wa Peacock Theater, huku Taraji P. Henson akirejea tena katika jukwaa hilo kama mshehereshaji wa shughuli nzima.
Baadhi ya wasanii kutoka Afrika wanaowania tuzo hizo ni Burna Boy, Ayra Starr, Tems, Seyi Vibes Asake, Tyla, Focalistic, Tyler ICU, huku Drake akiwa msanii aliyetajwa kuwania vipengele vingi zaidi ambavyo ni saba.
Mwaka 2010 ndipo BET walianza kujumuisha wasanii kutoka Afrika katika tuzo zao kupitia kipengele cha 'Best International Act; Africa' ambacho 2018 kilifanyiwa mabadiliko na kuwa 'Best International Act' kikihusisha wasanii wote kutoka nje ya Marekani.
Wiki hii Megan Thee Stallion ametangazwa kuwa ndiye atatumbuiza katika ufunguzi wa hafla hiyo ambayo itarushwa mubashara na Black Entertainment Television (BET) na baadhi ya mitandao.
Megan ambaye anaendelea na ziara yake ya Hot Girl Summer Tour, atapanda jukwaa la BET zikiwa ni siku mbili baada ya kuachia albamu yake tatu, MEGAN (2024) ambayo ilitoka Juni 28 ikiwa na nyimbo 18.
Wasanii wengine watakaotumbuiza ni pamoja na Will Smith, GloRilla, Ice Spice, Latto, Muni Long, Sexyy Red, Shaboozey, Mone na Tyla, mshindi wa Grammy 2024 kutokea Afrika Kusini.
Naye Usher Raymond IV anatarajiwa kupewa tuzo ya heshima ya mafanikio ya kazi yake ya sanaa (lifetime achievement), akiungana na mastaa wengine kama Mary J. Blige, Busta Rhymes na Diddy ambao wamewahi kupokea tuzo hiyo.
Usher aliyepata umaarufu mwishoni mwa miaka ya 1990 kufuatia kuachia albamu yake ya pili, My Way (1997), pia anawania tuzo nne; Albamu Bora ya Mwaka, Wimbo Bora wa Kushirikiana, Msanii Bora wa Kiume R&B/Pop na Video Bora ya Mwaka.
Hadi sasa Beyonce ndiye msanii aliyeshinda tuzo nyingi za BET akiwa ameshinda 32 ukichanganya na zile alizoshinda akiwa na Destiny's Child na The Carters (Beyonce & Jay Z). Anafuatiwa na Chris Brown (19), Drake (17), Nicki Minaj (12) na Lil Wayne (11).
Kwa Afrika, Wizkid na Burna Boy kutoka Nigeria ndio vinara wa tuzo za BET ambapo kila mmoja ameshinda mara nne ila Wizkid kuna moja alishinda kupitia kolabo yake na Beyonce, Brown Skin Girl (2019) iliyoshinda kipengele cha HER Award 2020.