Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Anko Kitime: Wanaume kuimba matatizo ya wanawake siyo kosa

Muktasari:

  • Wiki hii nilipata bahati ya kuongea na wanamuziki chipukizi kuhusu mambo mengi yaliyopita katika ulimwengu wa muziki wa dansi Tanzania.

Dar es Salaam. Wiki hii nilipata bahati ya kuongea na wanamuziki chipukizi kuhusu mambo mengi yaliyopita katika ulimwengu wa muziki wa dansi Tanzania.

Kati ya swali nililoulizwa ni kwanini waimbaji wa kiume walikuwa wakiimba ujumbe wa wanawake? Nilianza kukumbuka nyimbo nyingi zilizoimbwa na wanaume enzi hizo, kwa mfano Mume Wangu Jerry – Mlimani Park Orchestra, Mfaume Waniliza – Mlimani Park Orchestra, Mfaume- Orchestra Makassy, Nimemkaribisha Nyoka- Tancut Almasi Orchestra,  Mabruki- Maquis, Mke Mkubwa – Vijana Jazz, Rehani-Oss Ndekule, Kalubandika- Maquis, Ndoa ya Mateso – Dar es Salaam International Orchestra.

Hii ni orodha ndogo sana kati ya nyimbo nyingi za bendi tofauti, waimbaji  walikuwa wanaume, walikuwa wakiimba nafasi za wanawake. Hebu tuangalie baadhi ya maneno katika nyimbo hizi.  Wimbo Mfaume wa Orchestra Makassy uliimbwa na Issa Nundu na Kyanga Songa ulikuwa na maneno haya;

Ewe Mfaume umefika nyumbani kwetu, Mimi bado nasoma mama, Ukanieleza kwamba unataka tufunge pingu za maisha pamoja nami, Nikakweleza subiri nikimaliza shule ewe Mfaume, Kwa kuwa siwezi kuolewa bado ningali mwanafunzi oyoo.
Sehemu ya wimbo wa Tancut Almasi Orchestra ulioitwa Nimemkaribisha Nyoka ulioimbwa na Kasaloo Kyanga  ulikuwa na maneno yafuatayo;

Mume wangu alipotoka kazini, Nikamuelezea mambo yote mama, Naye pia akakubali  kama ni dada yake ambaye wamezaliwa tumbo moja, Basi tukaendelea kuishi kama mtu na wifi yake ndani ya nyumba.

Marijani Rajabu, jabali la muziki akiwa na Dar es salaam International Orchestra naye aliimba maneno haya katika wimbo Ndoa ya Mateso;

Niulizieni enyi walimwengu, huyu mwanaume anavyonitesa, Hii ndio haki au ni mateso, hii ndio haki au ni mateso,
Kanitoa kwetu kwa baba na mama kwa vigelegele na heshima nyingi, Tizameni sasa anavyonigeuka, Tizameni sasa anavyonigeuka, Ananipa mateso huku ugenini sina hata ndugu wa kunisaidia, Nami nina watoto jamani tabu gani, Nami nina watoto jamani tabu gani, Kwani kuolewa ni jambo la ajabu au kuolewa sawa na utumwa, Kama ndivyo hivyo mimi nimeshindwa, Kama ndio hivyo mimi nimeshindwa, Natoa ushahidi kwako we mjumbe, mwambie huyo bwana anipe talaka yangu, Nisije kuondoka ikawa maneno, nisije kuondoka ikawa maneno.
Wimbo ulioitwa Masikitiko wa Tancut Almasi Orchestra ulikuwa na kibwagizo hiki;

Kinachonisikitisha ni kuona kwamba nakosa mume wa kunioa mama, Nami nijisikie kama wenzangu waliobahatika kuolewa iyooo iyoo.
Nyimbo hizi zilitungwa na kuimbwa na wanaume na ni nyimbo ambazo bado hazijapoteza umaarufu  japo nyingine zina zaidi ya miaka 30 toka zilipoanza kusikika. Haikuwa kitu cha ajabu kwa wanaume kuimba kuhusu matatizo na maisha ya wanawake hapo zamani. Moja ya sababu ilikuwa ni kukosekana kwa waimbaji wa kike katika muziki wa bendi za dansi, lakini hata pale bendi zilikuwa na waimbaji wa kike bado nyimbo zilizohusu wanawake zilitungwa na kuimbwa na wanaume bila kuweko na shida yoyote. Ulikuwa usanii wa kiwango cha juu sana. Siku hizi ni nadra sana kusikia sanaa ya aina hii, na hakika ilipigwa vita na hata viongozi kadhaa ambao waliona ni kosa wanaume kuimba nafasi za wanawake.

Lakini jambo hili si geni kabisa katika sanaa, Tyler Perry ni muigizaji maarufu ambaye moja ya sifa yake kubwa ni kuigiza nafasi ya mwanamke  Mabel ‘Madea’ Simmons, na ameweza kutengeneza sinema nyingi akiigiza kama mwanamke Madea, na hakika ukiangalia sinema hizo utaona jinsi aliyoweza kuvaa nafasi yake anayoigiza.

Hata hapa kwetu msanii Joti amekuwa na mafanikio makubwa katika kuigiza nafasi ya mwanamke katika vichekesho vyake vingi, na ndivyo ilivyokuwa kwa watunzi na waimbaji wengi wa bendi wa zamani. Siku hizi kuna waimbaji wengi sana wa kike lakini je wanazungumza matatizo ya wanawake kwa uzito uliokuwa unabebwa na wanaume katika nyimbo za dansi zilizotajwa? 

Kuna waimbaji wa kike mashuhuri kwa ‘mipasho’, hizi ni tungo ambazo mara nyingi ni kuwasema wanawake wengine na hasa katika kugombea penzi la wanaume. Kundi jingine la waimbaji wa kike wamejikita zaidi katika kuimba nyimbo za mapenzi, hivyo pengo la nyimbo zinazoongelea matatizo ya wanawake limerudi japo waimbaji wanawake wako wengi sana siku hizi, pengine inasubiriwa wanaume waanze tena kutunga na kuimba nyimbo kwa kuvaa  matatizo ya wanawake. Katika kuongea na baadhi ya waimbaji wa kiume wa siku hizi wengi walisema wanaona aibu kuimba nyimbo ambazo wanaimba kama ‘mke wa mtu’, kubwa likiwa ni kuogopa kuhisiwa kuwa si mwanaume kamili, jambo ambalo halikujitokeza kabisa zamani.


 Ila hakika hapa nalazimika kushangaa kidogo, kwani mwanamuziki huyohuyo ambaye ameamua kutoga masikio na kuvaa hereni na kutinda nyusi huku amesuka vizuri nywele zake, na suruali kashusha kuonyesha nguo yake ya ndani anasema anaona aibu kuimba nyimbo zenye maneno ya wanawake kwani atahisiwa vibaya..!

Nadhani usanii huu wa wanaume kuimba nyimbo zenye ujumbe kwa wanawake, bado una nafasi katika sehemu kubwa ya jamii yetu ambayo haina hisia mbaya, na pia kwa kuwa waimbaji wa kike wenyewe hawataki kubeba jukumu lao la kuelimisha matatizo yao na ya wanawake wenzao. Nimalize kwa kuandika maneno ya wimbo Nirudishe Kwetu uliopigwa na Msondo miaka ya 70, na kuimbwa na akina Hassan Rehani Bitchuka na Mzee Muhidini Gurumo..

Mume wangu nirudishe kwetu, Nyumba yako imekwisha nishinda, Sababu watoto wako sielewani nao, kila nisemalo wasema mimi mama wa kambo, Kumbuka nilikueleza usimuache mama watoto wako, Kumbuka nilikueleza usimuache mama watoto wako, Watoto wengi mmekwisha zaa nae mmrudishe mama watoto wako.