Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bavicha nao wajitosa sakata la Basata kufungia nyimbo

Bavicha nao wajitosa sakata la Basata kufungia nyimbo

Muktasari:

  • Siku chache baada ya Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kuufungia wimbo wa Mama wa msanii Emmanuel Elibariki maarufu Ney wa Mitego, Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) limelaani kitendo hicho kwa madai kuwa ni kuvunja katiba kwa kuingilia uhuru wa msanii huyo katika kutoa maoni yake.

Dar es Salaam. Siku chache baada ya Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kuufungia wimbo wa Mama wa msanii Emmanuel Elibariki maarufu Ney wa Mitego, Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) limelaani kitendo hicho kwa madai kuwa ni kuvunja katiba kwa kuingilia uhuru wa msanii huyo katika kutoa maoni yake.

Mei 3, 2021 Basata ilizuia wimbo huo kwenda hewani hadi ufanyiwe marekebisho katika baadhi ya mashairi kwa madai kuwa ina ukakasi, hata hivyo, Ney amesema hataubadilisha wimbo huo kwa sababu tayari ametumia gharama kubwa.

Leo Alhamisi Mei 6, 2021, Bavicha wameibuka na kudai kwamba baada ya kuusikiliza wimbo huo hawajaona uongo, uchochezi wala kashfa zozote zinazodaiwa na Basata kuwa sababu za kuufungia wimbo huo.

Pia, wamedai  wimbo huo haudhoofishi umoja, ushirikiano na ustawi bora wa jamii ya Tanzania kama ambavyo Basata wameeleza kabla ya kuufungia.

Kwa mujibu wa taarifa ya mratibu wa uhamasishaji wa Bavicha, Twaha Mwaipaya iliyotolewa leo inaeleza kuwa kitendo hicho cha Basata ni mwendelezo wa Serikali kuweka taratibu za kisheria kwa makusudi ili kuminya uhuru wa maoni, fikra, mawazo ya sanaa.

“Uamuzi wa Basata umevunja haki hiyo ya katiba na umeingilia haki na uhuru wa msanii Ney wa Mitego kutoa maoni yake,” inaeleza taarifa hiyo ya vijana wa Chadema ikisisitiza kwamba madai ya Basata hayana mashiko.

Inafafanua kuwa katiba imeruhusu uhuru wa mawazo huku ikinukuu Ibara ya 18 (1) ambayo inaeleza bayana kwamba:

“Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.”

Bavicha imewataka wasanii washikamane na kuwa wamoja katika suala hilo na kupinga matumizi ya kanuni hizo mbovu ambazo zitaua vipaji vya sanaa, kuua ndoto za vijana wengi, kuhatarisha ajira za vijana wengi na mapato yanayotokana na kazi za sanaa.

Jana Basata ilieleza kuwa utaratibu huo ni kwa mujibu wa sheria na lengo ni kutoa madaraja ya nyimbo husika si kuzifungia.

katibu mtendaji wa baraza hilo, Matiko Mniko amesema suala hilo si jipya bali ni utekelezaji wa sheria namba 23 ya mwaka 1984 ya Baraza la Sanaa la Taifa pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2019.

Amesema kanuni za sheria hiyo zimetoa ufafanuzi kupitia kanuni namba 25 kifungu (1)-(8) kuhusu masharti mahususi  juu ya masuala ya maadili ya kazi za sanaa na utoaji wa ithibati katika kazi za sanaa.

Katika maelezo yake Mniko amesema wameamua kufanya hivyo kama moja ya njia ya kulinda maadili na kuhakikisha kazi hizo zinaangaliwa au kusikilizwa kutegemea na rika la watu na kuhakikisha zinazingatia maadili, mila na desturi.

Mniko amesema sheria hiyo imeweka bayana nini msanii anapaswa kufanya katika kazi yake kabla hajaiwasilisha kwa walaji na wanachofanya Basata ni kuwakumbusha wasanii na vyombo vya habari kuhusu kanuni hizo.

 “Hii sheria sio ngeni katika kuitekeleza tumeanza nayo tangu mwaka 2018  lakini watu wanaiona kama ni ngeni, tunachokifanya ni kuwakumbusha tu,” amesema.

Alipoulizwa kwa nini msisitizo huo umefanyika sasa na si miaka iliyopita wakati sheria hiyo ilikuwepo amesema, “kitu chochote kikishatungiwa sheria na kutengenezewa  kanuni, ukiona kunalegalega katika utekelezaji mnakaa kama menejimenti kukazia kwa kuwa tayari kanuni zipo.”

Amewatoa wasiwasi  wasanii kuhusu ukaguzi wa kazi zao na kueleza kuwa wamejipanga na wana watu wa kutosha kukagua nyimbo, “wimbo mmoja unaweza kukaguliwa kwa dakika tano.

Huenda wasanii wakawa na wasiwasi kama kazi hii tunaweza kuitekeleza kwa wakati ukizingatia wasanii ni wengi na nyimbo mpya zinatoka kila siku, naomba niwaondoe shaka katika hili.”

 “Pia katika ukaguzi huo tunatarajia kutumia njia mbalimbali ikiwemo  kutoa namba ya Whatsapp ambapo msanii hatalazimika kufika ofisini kwake na badala yake atatuma wimbo na kutumiwa majibu kupitia mtandao huo.”