Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Anko Kitime: Wanamuziki walianza zamani kudai hakimiliki-7

Muktasari:

  • Wanamuziki wa Tanzania walianza kudai Hakimiliki mwishoni mwa miaka ya 80. Hali hii ilijitokeza baada ya teknolojia ya kanda za kaseti kuanza kuenea, teknolojia hiyo  iliwezesha kwa mara ya kwanza kazi za wanamuziki kuwa rahisi kurudufu na kuanza kuuzwa bila ruksa yao

Dar es Salaam. Wiki hii ninamalizia makala za hakimiliki kwa andiko hili nililoandika  Aprili 20, 2017, ili liwe kama muktasari wa makala 6 mfululizo zilizoelezea kwanini hakimiliki Tanzania haijatoa matunda.

Wanamuziki wa Tanzania walianza kudai Hakimiliki mwishoni mwa miaka ya 80. Hali hii ilijitokeza baada ya teknolojia ya kanda za kaseti kuanza kuenea, teknolojia hiyo  iliwezesha kwa mara ya kwanza kazi za wanamuziki kuwa rahisi kurudufu na kuanza kuuzwa bila ruksa yao. 

Kabla ya kipindi hicho, wanamuziki waliotaka kuuza nakala ya nyimbo zao walilazimika kuvuka mpaka na kuingia Kenya ambako kulikuwa na kampuni kadhaa ambazo zilikuwa na viwanda vya kutengeneza santuri. 

Ujio wa kanda za kaseti uligongana na kipindi ambacho mpaka wa Tanzania na Kenya ulikuwa umefungwa kutokana na migongano ya kisiasa kati ya nchi mbili hizi, na kwa kuwa santuri zilikuwa zikitengenezwa Kenya ikawa ni vigumu kupata santuri hizo nchini kwetu, santuri chache zilikuwa zikiingia nchini kupitia njia za panya na nyingine chache kupitia maduka ya umma ya Regional Trading Company (RTC), kwa ujumla kulikuwa na uhaba wa kazi za muziki. 

Hivyo basi wafanyabiashara wenye akili za haraka wakaanza kurudufu nyimbo maarufu na kuziuza kwa njia ya kaseti. Biashara hiyo iliweza kukuwa na kufikia nchi hii kuwa na mitambo iliyoweza kutoa maelfu ya kanda kwa muda mfupi, kanda ambazo zilisambazwa kote nchini na hata nchi jirani, kwa kuwa nyingi za kanda hizi zilikuwa zimerudufiwa bila ruksa ya wenye nyimbo hata nchi jirani zilianza kulalamika kuhusu biashara hii haramu ambayo Tanzania ilikuwa kinara.

Kwa vile miaka hiyo kulikuwa na wimbi la wanamuziki wakubwa kutoka Kongo kukaribishwa kufanya maonesho nchini, kukaanza kutokea mikasa baada ya wanamuziki hao kukuta kanda za nyimbo zao zikiwa zinauzwa bila idhini yao, marehemu Defao alianguka kilio baada ya kuingia kwenye duka moja na kukuta kazi zake zikiuzwa bila yeye kujua, marehemu Fan Fan wa Orchestra Somosomo alimlamba kibao mfanyabiashara mmoja maarufu wa kuuza kanda baada ya yeye kukuta kanda zake zikiuzwa bila idhini yake,  Mbilia Bel alifanya ziara ya kuzurura kwenye maduka na kudai malipo ya papo kwa papo na hadithi hizi ziliandikwa hata kwenye magazeti wakati huo. 

Harakati za wanamuziki kudai sheria bora ya Hakimiliki zilizaa matunda mwaka 1999, ambapo sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki no 7 ya 1999 ilipitishwa na Bunge.
 
Mwanzoni mwa 2000, Chama cha Hakimiliki cha Tanzania (COSOTA) kilizaliwa na aliyewahi kuwa Waziri  wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe akawa mwenyekiti wa kwanza wa Bodi ya  chama hicho. Pamoja na juhudi hizi za kwanza kuna kila dalili kuwa serikali na jamii kwa ujumla haijawahi kuona umuhimu wa ulinzi wa hakimiliki.  

Inawezekana jambo kubwa linalofanya serikali kutokuona umuhimu wa hakimiliki ni kwa sababu ya kutokujua faida za hakimili kwa wasanii, sanaa, utamaduni, jamii na serikali yenyewe, na hivyo kuziba masikio hata ya kupewa elimu kuhusu suala hili. 

Wabunge pia wanastahili kubeba lawama kwa hili kwani nao miaka yote  wamekuwa wagumu kutaka kuelewa kwa undani kuhusu sheria hii, kiasi cha kwamba wanapokuwa na nia ya kusaidia ‘wasanii’ huishia  kuongea kwa wepesi sana hoja zao kuhusu hakimiliki.

Nitoe mfano rahisi wa kuonesha umuhimu wa ulinzi wa hakimiliki. Katika ripoti ya World Intellectual Property (WIPO) ya Mchango wa Tasnia ya Hakimiliki katika Uchumi wa Taifa la Tanzania (2012) (The Economic Contribution of Copyright-Based Industries in Tanzania), ilionesha kuwa katika mwaka 2009, himaya ya hakimiliki iliingiza jumla ya shilingi 676,458,324,498.

 Ripoti ilionesha pia kuwa mapato yatokanayo na hakimiliki, yalichangia asilimia 4.6 ya pato la Taifa, na katika  mwaka huohuo pato la Taifa kutokana na madini lilikuwa ni asilimia 2.5,  hakika wote tunajua jinsi shughuli za madini zinavyoangaliwa kwa jicho makini, na kila siku tunasikia ripoti za kuboresha mikataba yake, serikali, Bunge, wananchi wote wako makini sana na madini lakini hesabu ndio hizo, zilionesha kilichokuwa kinaingiza zaidi. 

Hizo zilikuwa hesabu za 2009, ni miaka 15 imepita sasa hakika ripoti ingefanyika sasa lazima ingeonesha hesabu kubwa zaidi.

 Mwaka 2006 Wizara ya Viwanda na Biashara ilipitisha  kanuni iliyolazimisha kazi zote za muziki na filamu kuwa na stika zilizoitwa Hakigram, serikali haijawahi kutoa fedha za kuwezesha stika hizo zianze kufanya kazi.

Lakini mwaka 2007 ikatungwa kanuni nyingine ya Wizara ya Fedha ikilazimisha kazi za muziki na filamu kuwa na stika za TRA, kanuni hii ya pili ilikuja pitishwa bila utafiti wowote, japo kila mara kumekuwa na taarifa kuwa ‘Ikulu’ ilitoa shilingi milioni 20 kwa mtafiti kutoka ‘Chuo Kikuu’ ili kufanya utafiti uliopelekea kutungwa kwa kanuni hizo, hakika mtafiti huyo’ kama alikuweko’ angejua kuwa kuna stika tayari hivyo cha kufanya pengine ingekuwa kuiboresha stika hiyo, kimsingi kwa sasa kisheria kila kazi ya muziki na filamu inatakiwa iwe na stika mbili!!.

Mheshimiwa Rais wa awamu ya nne alirudia zaidi ya mara moja taarifa ya Ikulu kutoa fedha kwa ajili ya mtafiti. Lakini mpaka leo, hiyo ripoti haionekani, mtafiti hajulikani na hakika stika za TRA utekelezaji wake ulishayeyukia hewani.

 Katika nchi zilizoendelea hakimiliki ni moja ya misingi  ya maendeleo na eneo kubwa la pato la Taifa. Katika zama hizi ambazo Tanzania inataka kuwa nchi ya viwanda, ni muhimu sana misingi ya kulinda ubunifu kuimarishwa, labda kama nia ya viwanda vyetu ni kutengeneza mali ambazo zina hakimiliki za wabunifu kutoka nje ya nchi tu. 

 Tanzania ilisaini mkataba wa Berne Convention mwaka 1994 ambao unailazimu kulinda hakimiliki za wabunifu wa nje kwa nguvu sawa na wabunifu wa ndani. Ulinzi wa hakimiliki ni muhimu katika kulinda na kuendeleza kazi za sanaa za jamii na ni nguzo muhimu katika kulinda na kuendeleza utamaduni wa Taifa. Na hakika ni chanzo muhimu sana cha pato la Taifa.