Anko Kitime: Wanamuziki wameanza zamani kudai sheria ya hakimiliki-3

Muktasari:
- Kwa kawaida vyama vya Hakimiliki huanzishwa na kuendeshwa na wadau katika sekta mbalimbali za ubunifu. Mfano vyama vya hakimiliki vya kukusanya mirabaha ya watunzi wa muziki, vyama vya watunzi wa muziki, vyama vya watunzi wa maandishi, vyama vya hakimiliki katika filamu na kadhalika.
Dar es Salaam. Katika makala ya leo nitaendeleza mlolongo wa historia ya Hakimiliki, na nitaanzia pale ilipoanzishwa COSOTA. Chama cha Hakimiliki nchini, Copyright Society of Tanzania (COSOTA) kilianzishwa kwa mamlaka ya kisheria chini ya kifungu 51(1) cha sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ya mwaka 1999.
Kwa kawaida vyama vya Hakimiliki huanzishwa na kuendeshwa na wadau katika sekta mbalimbali za ubunifu. Mfano vyama vya hakimiliki vya kukusanya mirabaha ya watunzi wa muziki, vyama vya watunzi wa muziki, vyama vya watunzi wa maandishi, vyama vya hakimiliki katika filamu na kadhalika.
Mwaka 1997 katika moja ya semina za kuelimishwa mambo ya hakimiliki iliyofanyika Lilongwe Malawi, ushauri wa mambo mawili ulitolewa na taasisi ya Hakimiliki ya Miliki Ubunifu Duniani (WIPO).
Ilishauriwa kuwa katika kuunda sheria mpya ya Hakimiliki ya Tanzania, sheria iruhusu kuundwa kwa chama kimoja tu cha Hakimiliki, na pili chama hicho kianzishwe kwa msaada wa serikali mpaka kitakapokuwa na nguvu za kujiendesha chenyewe ndipo kikabidhiwe wadau.
Mfumo huo wa chama kimoja cha Hakimiliki katika nchi haukuwa mgeni na ulionyesha mafanikio katika sehemu nyingi. Katika kipindi hicho hicho kulikuwa na mgogoro mkubwa nchini Nigeria ambako sheria iliruhusu vyama huria vya hakimiliki, vyama vikawa vingi mno na hivyo kukawa na fujo badala ya utaratibu mzuri wa kukusanya mirabaha, ikalazimika mambo yaende mahakamani na shughuli za kukusanya na kugawa mirabaha zikasimama kwa muda mrefu.
Ilikuwa ni kwa sababu hii sheria ya hakimiliki ya Tanzania ilipotoka ikaagiza kuundwa chama kimoja cha hakimiliki.
Katika sheria hiyo, baadhi ya mambo yaliyotajwa katika uundaji wa chama hicho ni kuwa kitakuwa na bodi ambayo wajumbe wake wangebadilishwa baada ya kila miaka mitatu. Bodi ya kwanza ilielekezwa kuwa na wajumbe kutoka sehemu zifuatazo;
(a) Ofisi ya kamishna wa utamaduni;
(b) BASATA
(c) Ofisi iliyoshughulika na na Industrial
(d) Cahama cha watengeneza filamu;
(e) Makumbusho ya taifa
(f) Idara ya sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;
(g) Ofisi ya Mwanasheria Mkuu;
(h) Chama cha watunzi wa vitabu Tanzania.
(i) Tume ya utangazaji
(j) Idara ya forodha
Sheria ikaendelea kusema, theluthi ya wajumbe ambao wako katika bodi kutokana na nafasi za ofisi zao, watapunguzwa kwenye bodi kila miaka miwili na nafasi zao kuchukuliwa na wadau. Nia ya kipengele hiki ilikuwa kuhakikisha kuwa baada ya awamu tatu za bodi, wajumbe wote wa bodi wangekuwa ni wadau na serikali ingekuwa imemaliza kazi yake ya kukilea chama.
Waziri muhusika alikuwa anauwezo wa kuteuwa wajumbe wasiozidi watatu alioona wanafaa kukisaidia chama katika kazi zake, japo kuwa wajumbe hao wasingekuwa na turufu ya kupiga kura katika mikutano ya bodi. Bodi ya kwanza ya COSOTA ilikuwa chini ya uenyekiti wa Mheshimiwa Harrison Mwakyembe.
Na mtendaji wake mkuu alikuwa Mzee Steven Mtetewaunga, ambaye hakika ndiye muhimiri wa kufanikiwa kupatikana kwa sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ya 1999.
Kanuni kadhaa ziliandaliwa ikiwemo kanuni iliyoitwa Copyright Licencing of Public Performance and broadcasting Regulation , 2003.
Kanuni hii ilielekeza kuwa ni marufuku kutumia kazi ya mtu hadharani bila kupewa mamlaka ya muhusika kupitia COSOTA, ndio kanuni iliyokuwa ikilazimisha vyombo vya utangazaji kulipia matumizi ya muziki katika vipindi vyake. Ni mwaka wa 22 toka kanuni hiyo itolewa na mambo mengi ya ajabu yamepita katika kupinga kutekeleza kanuni hii.
Jambo la ajabu ni kuwa wanamuziki wengi maarufu wametumika kupinga kanuni hii na hivyo kudhoofisha vita ya utekelezaji wake.
Mwaka 2002, COSOTA iliunda kamati iliyoitwa National Antipiracy Committee, kamati hii ilitakiwa kutayarisha kanuni ili kuzuia uharamia wa kazi za sanaa ikiwemo usambazaji wa kanda za kaseti, CD, DVD bila ruksa ya mwenye mali. Hatimaye kanuni iliyoitwa The Copyright and neighbouring Rights(Production and distribution of sound and audiovisual recordings) Regulation.
Hadithi ya ajabu sana ilitokea kuhusu kanuni hii. Katika kikao cha bodi kilichofanyika katikati ya mwaka 2005, ilionekana kanuni hii haijaridhiwa na Waziri kama ilivyotakiwa, waziri muhusika tayari alikuwa ameelekea kwenye jimbo lake la uchaguzi kwani muda wa uchaguzi ulikuwa umekaribia.
Bodi ilimuagiza Mtendaji Mkuu wa COSOTA kumfuata waziri hukohuko jimboni ili kutia saini kanuni ile ianze kutumika. Baada ya Waziri kutia saini kanuni ile ilipotea katika mazingira ya ajabu. Hivyo basi baada ya uchaguzi wa 2005, waziri mpya alikuja kutia saini kanuni hiyo na inajulikana kama The Copyright and neighbouring Rights (Production and distribution of sound and audiovisual recordings) Regulation, 2006.
Kwa kanuni hii kazi zote za muziki na filamu kabla ya kuuzwa zilitakiwa kuwa zimebandikwa stika ya COSOTA iliyoitwa Hakigram. COSOTA ilianza kutafuta mtaji wa kutekeleza kanuni hii, huku pembeni zikaanza mbinu mpya za kuja na stika aina nyingine, mwaka 2013 kukatengenezwa kanuni za sheria ya The Exice ( Management and Tarrif Act), kanuni zilizoitwa The film and music products (Tax Stamps) Regulations, 2013.
Kisheria kila kaseti, CD , VCD, au DVD ingetakiwa iwe na stika ya Hakigram na stika ya TRA. Hapo ndipo kengele ya mwisho wa maduka halali ya kuuza kanda za muziki na DVD. Katika mlolongo huu si wasanii tu waliopata hasara, serikali ilikosa mabilioni ya mapato kutokana na biashara hiyo.