Anko Kitime: Wanamuziki wameanza zamani kudai sheria ya hakimiliki

Muktasari:
- WanaTeknolojia ya kanda na kaseti iliingia na kupokelewa vizuri sana. Kulikuwa na viwanda vikubwa viwili nchini vilivyokuwa vikitengeneza mashine za kupigia kanda zilizoitwa ‘radio cassette player’, zilikuwa ni mashine ambazo zilikuwa na redio iliyounganishwa na mashine ya kupiga kanda za kaseti.muziki wameanza zamani kudai sheria ya hakimiliki
Dar es Salaam. Kama nilivyozungumza katika makala iliyopita biashara ya kanda za muziki ilianza miaka ya 70 mwishoni mwishoni.
Teknolojia ya kanda na kaseti iliingia na kupokelewa vizuri sana. Kulikuwa na viwanda vikubwa viwili nchini vilivyokuwa vikitengeneza mashine za kupigia kanda zilizoitwa ‘radio cassette player’, zilikuwa ni mashine ambazo zilikuwa na redio iliyounganishwa na mashine ya kupiga kanda za kaseti.
Kiwanda cha Matsushita kilichokuwa kikitengeneza ‘radio cassette’ za aina ya National, kilikuwa Dar es Salaam na kiwanda cha Philips kilichokuwa kikitengeneza radio cassette aina ya Philips kilikuwa Arusha.
Kiwanda cha Arusha pia kikawa kinatengeneza kanda za kaseti. Biashara ya muziki kupitia kanda za kaseti taratibu ikaanza kukua. Kufikia miaka ya 80, kukawa na viwanda vikubwa vilivyokuwa na uwezo wa kurudufu maelfu ya kanda kwa siku, viwanda hivyo vilikuwa hasa Dar es Salaam.
Kukua kwa viwanda hivi kulitokana pia na kuboreshwa kwa ulinzi wa Hakimiliki katika baadhi ya nchi huko Mashariki ya Kati, wafanyabiashara haramu kutoka huko wakahamishia nguvu zao huku kwetu ambako sheria zilikuwa hafifu na pia wengine walihamishia biashara zao katika nchi kadhaa Afrika ya Magharibi, ikiwemo Sierra Leon.
Kutokana na kutokuweko na sheria zilizoeleweka za Hakimiliki, biashara iliyoingiza mamilioni bila kulipa kodi stahiki ikakomaa, Tanzania ikawa chanzo cha kazi za muziki haramu kwa sehemu kubwa ya Afrika Kusini mwa Ikweta.
Mapambano ya kutaka kuweko kwa sheria madhubuti pia kukapamba moto hasa upande wa wanamuziki. CHAMUDATA kwa upande wake wakati wa uongozi wa marehemu Kassim Mapili na Farahani Mzee wakaweza kuingia makubaliano na chama cha Music Copyright of Kenya ili kuweza kuwa na umoja wa nchi hizi mbili kulinda pamoja hakimiliki za wanamuziki na walifanikiwa kuanzisha kitu kilichoitwa East Africa Company.
Kama nilivyoeleza katika makala iliyopita BASATA ilikuwa ndio chombo cha kwanza kutengeneza rasimu ya sheria mpya ya Hakimiliki mwaka 1992, lakini katika kipindi hichohicho mambo yote yaliyo chini ya sheria za Miliki Ubunifu yakawa chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara.
Na mwaka mmoja baadaye, kuanzia siku ya Jumatano, Mei 5 hadi 8, ulifanyika mkutano mkubwa wa kuzungumzia Hakimiliki katika Hoteli ya Kilimanjaro Dar es Salaam, mkutano huo ndio ulikuwa mbegu ya kupatikana kwa sheria ya Hakimiliki iliyopo leo.
Mkutano ule ulifunguliwa na Waziri Mkuu wakati huo Mzee John Malecela, na mwenyekiti wa mkutano huo alikuwa Jaji Mkuu Francis Nyalali, tulijua serikali imetuelewa na kuchukulia jambo lile kwa uzito mkubwa sana. Kwa wanamuziki ambao tulikuwa tukilalamikia ukosefu wa sheria ya hakimiliki, mkutano huo ulikuwa na maana kubwa kwetu.
Baada ya mkutano huo, kupitia Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) zikaanza taratibu za kupata sheria bora ya Hakimiliki. Lakini uharamia wa kazi za sanaa ukawa unaendelea, mwanaharakati Francis Kaswahili akaanzisha chama cha kulinda hakimiliki alichokiita Tanzania Music Copyright Association, Kaswahili akiwa mwenyekiti na katibu wake mkuu alikuwa Innocent Nganyagwa, nao kwa upande wao wakawa wanaendesha kampeni za kudhibiti uharamia wa kazi za muziki, ila wakawa wanakwamishwa na kukosekana kwa sheria ya kuwapa nguvu stahiki.
Katika kutafuta uzoefu wa nchi nyingine ili kupata sheria bora zaidi, binafsi niliweza kusindikizana na maafisa kutoka Brela na kuweza kupata mafunzo kutoka nchi kadhaa Afrika zikiwemo Ghana, Ivory Coast, Senegal, Malawi na Afrika ya Kusini.
Hatimaye mwaka 1999, Bunge likapitisha sheria ya hakimiliki na Hakishiriki ya Mwaka 1999. Nakumbuka tulisherehekea siku ile kwa kudhani sasa wanamuziki wa Tanzania nao watapata stahiki zao kutokana na kazi zao.
Haikuchukua muda mrefu tukagundua kuwa sheria ikishapitishwa mambo hayabadiliki kwa siku moja. Biashara ya uharamia ikaendela kama kawaida, waliokuwa wakipokea bakshishi kutoka kwa wafanyabiashara haramu wa kazi za muziki wakaendelea kupokea mgao wao, kuna kiongozi mmoja alikuwa akipokea bahasha kila mwezi kama vile ni mshahara.
Mabadiliko kidogo yakaanza kutokea kwa wanamuziki wa hapa Tanzania, wasambazaji wakaanza kuingia mikataba na wanamuziki wa Tanzania, badala ya kurudufu na kusambaza kazi bila ruksa. Bendi zikaanza kutoa ruksa ya kazi zao kusambazwa kwa kiwango cha shilingi elfu thelathini kwa ‘album’.
Kiwango hiki kilimruhusu msambazaji kusambaza kanda popote duniani bila mipaka.
Kufikia mwaka 1995, mwanamuziki aliweza kuingia mkataba wa kusambaziwa kanda zake kwa kupewa shilingi mia moja kwa kila kanda, na mkataba ulikuwa wa kusambaza kanda 1000, kisha kuingia mkataba mwingine.
Kwa kawaida baada ya kupewa shilingi laki moja, kama malipo ya kanda hizo elfu moja ukawa ndio mwisho kwani hadithi ilikuwa, ‘ Samahani kanda zako hazitoki’
Ili sheria ifanye kazi inahitaji kuwa na kanuni na mwaka 2001, miaka miwili baada ya kupitishwa kwa sheria ya Hakimiliki, chama cha kwanza cha kisheria cha hakimiliki kikaanzishwa na kikaitwa COSOTA.
Kati ya vyama vya hakimiliki vilivyokuwa na mafanikio mazuri katika Afrika vilikuwa ni chama cha COSGHA cha Ghana na chama cha COSOMA cha Malawi, na ndio hasa msingi wa chama kipya cha hakimiliki Tanzania kupewa jina lililofanana. Mabadiliko yakawaje? Tukutane makala ijayo