Anko Kitime: Wanamuziki wameanza zamani kudai sheria ya hakimiliki

Muktasari:
- Nchi yetu sasa inatimiza miaka 101 tangu kuanza kutumika sheria ya hakimiliki nchini.
Dar es Salaam. Mei 21 ilikuwa siku ya Miliki Ubunifu Duniani na kauli mbiu yake ilikuwa, ‘MILIKI UBUNIFU NA MUZIKI:SIKILIZA MDUNDO WA MILIKI UBUNIFU’ Hakimiliki ni sehemu Miliki Ubunifu, hebu tuonje historia ya mapambano ya wanamuziki kudai utekelezaji bora wa sheria ya Hakimiliki.
Nchi yetu sasa inatimiza miaka 101 tangu kuanza kutumika sheria ya hakimiliki nchini.
Kwa kuwa tulikuwa chini ya utawala wa Uingereza, kuanzia muda mfupi baada ya vita ya kwanza ya dunia na sheria zilizoanza kutumika zikawa za Uingereza na hivyo basi kuanzia mwaka 1924 tulianza kutumia sheria iliyoitwa the Imperial Copyright Act 1911. Hivyo kinadharia nchi yetu imekuwa na sheria ya Hakimiliki toka ilipoanza kuwa nchi.
Kwa miaka ya awali ya ukoloni, wanamuziki wa nchini mwetu hawakuwa na shida sana ya sheria hiyo kwani teknolojia ya kurekodi muziki na kuusambaza au kuutumia kwa ajili ya biashara kwa njia nyingine yoyote ile ilikuwa bado haijaingia nchini.
Mwaka 1954 ndipo kilipozinduliwa kituo cha redio kilichoweza kusikika nchi nzima na kikaitwa TBC hiki kilikuwa kifupi cha Tanganyika Broadcasting Corporation.
Kituo hiki kilianza kufuata sheria ya hakimiliki kwa kutayarisha maelezo ya kila wimbo uliopigwa na kulipia kwa kupeleka malipo Performing Rights Society ya Uingereza.
Hali hii ilifanya wanamuziki wa hapa kutopata mafao yao sahihi kwani hakukuwa na utaratibu wa vyama vya kukusanya mirabaha ya wanamuziki wakati huo. Lakini baadhi walilipwa akiwemo baba yangu aliyelipwa shilingi 60 baada ya nyimbo alizorekodi kwenye studio za redio hiyo kupigwa kwenye moja ya vipindi wakati huo.
Utaratibu wa kuweka kumbukumbu na kulipa uliendela mpaka mwaka 1966, nchi yetu ilipopata sheria yake na kuachana na sheria ya Uingereza. Sheria hiyo mpya iliitwa Copyright and Neighbouring rights act No. 61 ya mwaka huo 1966.
Baada ya kutengenezwa sheria hii, ulipaji wa matumizi ya muziki wa redio pekee wakati huo ambayo ilikuwa ni kituo cha Taifa ulisimama na hakika ndicho chanzo cha utamaduni wa vituo vya utangazaji mpaka leo kupata kigugumizi cha kulipia matumizi ya kazi za muziki.
Katikati ya miaka ya 70 kukaingia teknolojia ya kanda za kaseti, teknolojia hii iliwezesha watu binafsi kurufu muziki na kuanza kuuza. Awali muziki uliokuwa ukipatikana ulikuwa wa wanamuziki wa nchi za nje lakini miaka ya 80 kukaanza utamaduni wa kuuza muziki wa wanamuziki wa nchini na hapo ndipo wanamuziki wakaanza kudai sheria bora za ulinzi wa hakimiliki.
Chama cha Muziki wa Dansi (CHAMUDATA) chini ya Marehemu Mzee Kasim Mapili wakishirikiana na katibu wake Farahani Mzee walianza kuongea na ofisi ya Rais mwaka 1987 kudai haki hii.
Mwaka 1992, BASATA ikiwa chini ya Mtendaji Mkuu, Shogolo Challi iliweza kutengeneza rasimu ya sheria mpya ya Hakimiliki.
Januari 1993, ulifanyika uchaguzi wa viongozi wa CHAMUDATA na nilichaguliwa uenyekiti na uongozi mpya tukaendeleza ajenda kuu ya kudai sheria mpya Hakimili na hatimaye miaka sita baadaye Bunge likapitisha sheria mpya iliyoitwa Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ya 1999.
Ni miaka 26 sasa toka kupitishwa kwa sheria hiyo, lakini bado haijaweza kufanya kazi inayotegemewa, tulioanza kuipigania tukitegemea tutaifaidi sasa tumezeeka na bado matunda yako mbali, nini tatizo?
Kumekuwa na awamu mbalimbali za matatizo ya kutekeleza vizuri sheria hii. Wakati wanamuziki wakianza kudai sheria bora tatizo lao lilikuwa ni biashara ya kanda za muziki zilizokuwa zikishasambazwa na kuuzwa bila wao kupata mgao wa mauzo ya kazi zao hizo.
Biashara ilikuwa ni kubwa sana na Tanzania kilikuwa ndio kituo kikubwa cha utengenezaji na usambazaji wa kanda hizo. Kanda hizo zilisambazwa si Tanzania tu bali hata nchi zilizojirani zikiwemo, Zambia, Malawi, Burundi, Congo, Msumbiji, na hata visiwa vya Comoro.
Ilikuwa biashara kubwa na ilikuwa biashara ambayo ilikuwa rahisi kukwepa kodi, kwani kilichokuwa kikiuzwa hakikuwa halali wala hakina daftari.Rushwa kubwa zilisambazwa kwa watu waliokuwa wakiheshimika katika jamii. Biashara hii ikabadilika ilipoingia teknolojia ya CD na VCD.
Hizi zikaanza kuingia nchini awali kutoka Pakistani, taarifa iliyotolewa kwenye mtandao wa International Federation of Phonographic Industries (IFPI) ulitaja Tanzania kama ni moja ya nchi zinazosambaza kazi kutoka Pakistan ambazo mapato yake yalikuwa yakitukia kulifadhili kundi la Al Khaida.
Hivyo basi wanamuziki wa Tanzania wasio na chochote ilikuwa ngumu sana kushinda katika mazingira haya.Biashara ya kurudufu kanda ikasambaa karibu katika kila tarafa hapa nchini. Katika kujaribu kurekibisha hali hii COSOTA ilitengeneza kanuni iliyolazimisha kila kanda, CD, VCD, DVD inayouzwa nchini lazima iwe na stika ya COSOTA iliyoitwa Hakigram, mkakati ukatengenezwa na mamlaka ya kodi nao wakaja na stika kama hiyohiyo, matokeo yakawa ni mwanzo wa kifo cha biashara halali ya kuuza kand, CD na DVD. Je kilifuata nini? Tukutane toleo lijalo.