Zanzibar, Msumbiji kuimarisha ushirikiano katika sekta za utalii, uvuvi na nishati

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi (kulia) na Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo walipokutana na kufanya mazungumzo Ikulu ya Zanzibar.
Muktasari:
- Ushirikiano huu mpya unalenga si tu kukuza maendeleo ya pamoja, bali pia kuimarisha uchumi wa buluu kupitia sekta muhimu kama utalii, uvuvi wa bahari kuu, pamoja na mafuta na gesi.
Unguja. Ziara ya Rais Daniel Chapo wa Msumbuji visiwani Zanzibar imefungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kimkakati kati ya Zanzibar na Msumbiji, ambao unalenga kuimarisha mahusiano ya kijirani kwa kuzingatia masilahi ya pamoja ya kiuchumi, kijamii na kitamaduni.
Ziara ya siku tatu ya Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo nchini Tanzania, iliyomalizika leo Mei 9, 2025, imeweka msingi wa ushirikiano mpya na wa karibu kati ya Zanzibar na Msumbiji.
Katika ziara hiyo, Rais Chapo amekutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, na baadaye kufanya mazungumzo rasmi na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi katika Ikulu ya Zanzibar.

Katika mazungumzo yao, Dk Mwinyi na Rais Chapo wamekubaliana kushirikiana katika maeneo matatu muhimu ya kiuchumi: utalii, uvuvi wa bahari kuu, pamoja na mafuta na gesi.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza mazungumzo yao Ikulu Zanzibar leo Mei 9, 2025 Rais Mwinyi amesema ziara hiyo italeta chachu ya kuendeleza ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili.
“Katika mazungumzo yetu ya leo ni kwamba tumeonyesha maeneo yenye fursa kati yetu bila shaka kuna maeneo mengi lakini kwa hapa Zanzibar fursa zipo katika maeneo kama tulivyoyataja matatu makuu, utalii, uvuvi na mafuta na gesi,” amesema.
Rais Mwinyi alieleza kuwa sekta hizo zina fursa kubwa za kukuza uchumi wa Zanzibar na Msumbiji, hasa kutokana na mazingira ya kihistoria na kijiografia ya mataifa hayo mawili ya Pwani ya Bahari ya Hindi.
Katika sekta ya utalii, Msumbiji imeonyesha nia ya kujifunza kutoka Zanzibar, ambayo imepiga hatua kubwa katika kuendeleza sekta hiyo.
Ikiwa na fukwe nyingi kama Zanzibar, Msumbiji imevutiwa na jinsi Zanzibar ilivyofanikiwa kuimarisha utalii kama chanzo kikuu cha mapato ya uchumi wa visiwa hivyo.
Kuhusu mafuta na gesi, Zanzibar inatazamia kunufaika na uzoefu wa Msumbiji ambao umejikita katika uchimbaji wa rasilimali hizo kwa zaidi ya miaka 20.
Viongozi hao walijadili uwezekano wa kununua gesi kutoka Msumbiji kwa matumizi ya ndani, jambo ambalo linaweza kusaidia kukuza sekta ya nishati Zanzibar na kuboresha maisha ya wananchi.
Katika sekta ya uvuvi wa bahari kuu, Rais Chapo alitembelea Taasisi ya Uvuvi wa Bahari Kuu huko Fumba, Zanzibar, na kueleza kuvutiwa kwake na maendeleo yaliyofikiwa na Zanzibar katika uchumi wa buluu.
Ameeleza kuwa Zanzibar imeweza kufaidika na samaki wa gharama kubwa wanaopatikana katika bahari zake, ambao wanasafirishwa kwenda masoko ya Asia na Ulaya.

Msumbiji imeonyesha nia ya kushirikiana katika teknolojia ya uvuvi, mafunzo, na uwekezaji katika miundombinu ya sekta hiyo muhimu.
Pia, viongozi hao pia walizungumzia kubadilishana wataalamu wa lugha ambapo walimu wa Kiswahili kutoka Tanzania kwenda Msumbiji, na wa Kireno kuja Zanzibar.
Rais Mwinyi amesisitiza kuwa, mbali na masuala ya kiuchumi, ushirikiano huu umejengwa pia juu ya msingi wa kihistoria na kindugu.
Amesema kuwa, mbali na masuala ya diplomasia na ushirikiano wa kiuchumi, Zanzibar na Msumbiji zina uhusiano wa karibu wa kihistoria na kindugu uliojengwa juu ya msingi wa harakati za ukombozi wa Afrika.
Amebainisha kuwa vyama vyao vya siasa CCM, ambacho awali kilikuwa TANU, na FRELIMO cha Msumbiji vimekuwa na uhusiano wa muda mrefu na wa kihistoria, kwani FRELIMO kilianzishwa na kupata hifadhi na msaada mkubwa kutoka Tanzania wakati wa mapambano ya ukombozi wa taifa hilo.
Amesema, ni dhihirisho la undugu wa kweli uliopo baina ya mataifa hayo mawili tangu enzi za harakati za kujikomboa kutoka kwa ukoloni, na ambao unaendelea kudumu hadi leo.
Kwa upande wake, Rais Chapo ameeleza kufurahishwa na maendeleo yaliyofikiwa na Zanzibar na kusisitiza kuwa makubaliano waliyoafikiana yatatekelezwa kwa vitendo.
Ameeleza kuwa ushirikiano huu unaashiria urafiki wa dhati kati ya nchi hizo, akisema kuwa kama samaki wa baharini ni marafiki, basi hakuna sababu kwa binadamu kushindwa kuwa marafiki.