Wawakilishi wang'aka bajeti kiduchu ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais

Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Harusi Said Suleiman akiwasilisha Bajeti ya makadirio ya Mapato na Matumizi mwaka 2025/26 katika Baraza la Wawakilishi
Muktasari:
- Kwa mwaka wa fedha 2025/26 Baraza limeombwa kuhidhinisha Sh27.1 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa kazi za Idara tano zilizopo chini ya ofisi hiyo.
Unguja. Wakati Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, ikiomba Baraza la Wawakilishi kuhidhinisha Sh27 bilioni kutekeleza vipaumbele 11 katika idara tano, baadhi ya wawakilishi wamelalamika Serikali kutenga kiasi kidogo ikilinganishwa na ukubwa wa ofisi yenyewe na watu inaowahudumia.
Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ilitolewa kwa chama cha siasa kilichoshika nafasi ya pili kwa idadi ya kura za Urais. Katika muktadha huo, Othman Masoud Othman wa ACT-Wazalendo aliteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.
Akiwasilisha Bajeti ya Makadirio Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais leo Mei 9, 2025 Waziri mwenye dhamana, Harusi Said Suleiman ameomba baraza lijadili na kuhidhinisha Sh27.182 bilioni.
Katika bajeti hiyo, Sh12.4 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwa Sh10 bilioni kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Sh2.4 bilioni kutoka kwa washirika wa maendeleo.
Pia, Waziri ametaja moja ya changamoto zinazowakabili ni ufinyu wa bajeti na kutopata vifaa na vyombo vya usafiri.
Akichangia bajeti hiyo Mwakilishi wa Pandani Profesa Omar Fakih Hamad amesema licha ya wizara hiyo kushughulikia masuala muhimu ya watu wenye changamoto kubwa lakini kinachosikitisha serikali haitoi kipaumbele.
Amesema kwa kiasi kikubwa inagusa maslahi ya watu ambao ni rahisi kupata madhara, lakini hawajapewa kipaumbele.
“Ukiangalia mtiririko wa bajeti, kiasi hiki ni kidogo sana, licha ya nyingi zinagusa maslahi dhaifu watu wengi na inagusa watu wote,” amesema
“Usimamizi wa mazingira unastahili lakini, natoa malalamiko wizara hii zile shughuli tano ambazo zipo lakini haijapewa kipaumbele.
"Kazi za maendeleo zilipangwa ziwe Sh4 bilioni lakini hadi Machi zimepatikana asilimia 17, sasa hii hata kwenye chuo huwezi kupata D, tunawaulumu serikali kutoingizia fedha,” amesema Profesa Fakih.
Asilimia 13 ya fedha hizo ndio imetoka Serikalini na asilimia 37 ni mgawo wa wadau wa maendeleo hivyo bado serikali haijatoa kipaumbele.
Pia, kati ya Sh2 bilioni zilizoombewa kwa ajili ya dawa za kulevya, lakini wamepata Sh125 milioni.

Mwakilishi wa Pandani, Profesa Omar Fakih Hamad akichagia Bajeti ya makadirio Mapato na Matumizi ya wizara ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar.
Amesema suala la mazingira ni suala linalomgusa kila mmoja lakini “kwakweli kwa utaratibu huu hatuwezi kwenda popote.
Amesema hakuna sababu bajeti ndogo kama hizi zishindwe kutekelezeka tatizo ni kushindwa kuwa na msukumo wa Serikali.
Mwakilishi mwingine wa Kiembesamaki, Suleiman Haroub Suleiman naye amesema kiasi kinachotolewa hususani katika upande wa mazingira inakuwa kidogo zaidi ikilinganishwa na changamoto nyingi zinazojitokeza za kimazingira.
Mwakilishi wa Chumbuni, Miraji Khamis Mussa naye amesema imekuwa kawaida wizara hiyo kupewa fedha kidogo kwahiyo ifike wakati sasa seriklai itambue kazi kubwa inayofanywa na ofisi hiyo.
Matharani, kwenye uratibu wa mabadiliko ya tabianchi kati ya Sh2 bilioni zilizoombewa katika bajeti ya mwaka 2024/5 wamepewa Sh500 milioni tu.
Awali akiwasilisha bajeti ya ofisi yake Waziri Harusi, ametaja baadhi ya vipaumbele mwaka 2025/26 ni kutekeleza miradi ya kimazingira na mabadiliko ya tabianchi pamoja na utekelezaji wa mpango wa kuirithisha Zanzibar ya kijani na kutayarisha ripoti ya Tathmini ya kimazingira kwa kipindi cha miaka mitano 2020/25.
Pia, ni kufanya tathmini na kuandaa mpango mkakati mpya wa mazingira, kuendeleza mapambano dhidi ya dawa za kulevya na kuimarisha utoaji wa huduma za tiba na marekebisho ya tabia.
Kingine ni ujenzi wa kituo cha wanawake cha tiba na marekebisho ya tabia Kangagani, Pemba pamoja na kuendeleza miradi ya ujasiriamali kwa waraibu.
“Kukuza uwezeshaji, ujumuishwaji na upatikanaji wa haki na fursa kwa Watu wenye ulemavu kupitia mfuko wa maendeleo na kutayarisha na kutekeleza miongozo na mikakati miwili ya masuala watu wenye ulemavu.
Kipaumbele kingine ni kuwatambua watu wenye ulemavu nchini kwa kuwasajili katika mfumo wa Kidigitali wa kuhifadhia taarifa za watu wenye ulemavu.
Katika mpango huo, wataratibu utekelezaji wa mkakati wa IV wa Ukimwi ili kudhibiti maambukizi mapya kwa vijana, makundi maalumu na jamii kwa ujumla.
Kutekeleza mkakati wa mawasiliano na utetezi wa Ukimwi kwa vijana kwa kuanzisha mkakati wa nne waTaifa wa Ukimwi, miongozo ya kitaifa na kisheria ya ukimwi.
Amesema katika mazingira, watafanya utafiti wa kutambua maeneo yalioathirika na mabadiliko ya tabianchi Pemba pamoja na kufanya utafiti wa mabwawa ya asili na michirizi ya maji katika maeneo mbalimbali ya Pemba.
Kufanya tathmini juu ya wanyama adimu wanaopatikana Pemba pekee, kukuza uelewa kwa jamii juu ya masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Ujenzi wa kuta katika maeneo ya fukwe ili kuzuia maji ya bahari kuingia katika maeneo ya kilimo na makaazi kutokana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuendelea na utekelezaji wa programu ya kuirithisha Zanzibar ya kijani.
Walemavu
Katika kuthamini watu hao, watawajengea uelewa watu wenye ulemavu na jamii kuhusu masuala ya watu wenye ulemavu na kuendeleza mapambano dhidi ya udhalilishaji wa watu wenye ulemavu.
Kuhusu dawa za kulevya, amesema wataendelea kufanya operesheni kubwa na zakawaida, kuteketeza dawa za kulevya na kujenga kituo cha Pemba.