Sakata la RC na kadi za mpigakura latinga barazani, Serikali yajibu

Mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohamed Suleiman akizungumza katika mkutano wa Baraza la wawakilishi
Muktasari:
- Wawakilishi wahoji uhalali wa mkuu wa mkoa kukagua kadi za mpigakura, waziri asema hajavunja sheria, hata yeye ameshakaguliwa cha kwake.
Unguja. Sakata la Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrisa Kitwana, kuwataka wafanyakazi wa Serikali mkoani kwake wawasilishe kadi zao za mpigakura azikague, limeibukia Baraza la Wawakilishi, wakitaka kujua maagizo hayo aliyatoa wapi kwa sababu yanavunja sheria za nchi.
Akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais leo Alhamisi Mei 8, 2025 katika baraza hilo, Mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohamed Suleiman, amesema ni vema Serikali ikaweka wazi kilichofanywa na mkuu huyo wa mkoa kama ni agizo lake au la Serikali na hatua ilizochukua.
Itakumbukwa mkuu huyo wa mkoa Aprili 28, 2025, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, alieleza kusudio lake la kuwataka wafanyakazi wa ofisi yake na wale wa ofisi za wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri wawasilishe vitambulisho hivyo avikague.
Baada ya kutoa kauli hiyo, iliibua mjadala kwa wadau mbalimbali wa uchaguzi wakieleza namna kiongozi huyo anavyoingilia kazi ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na kuitaka tume hiyo ikemee jambo hilo.
Mbali na wadau hao, chama cha ACT-Wazalendo kupitia Mwanasheria wake Mkuu, Omar Said Shaaban, kilisema mkuu wa mkoa amevunja si tu Katiba, bali pia sheria tano za nchi.
Amezitaja sheria hizo kuwa ni pamoja na ya Uchaguzi Zanzibar na Tanzania Bara, Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2023, Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Sheria ya Utumishi wa Umma.
Akichangia hotuba hiyo, Dk Mohamed ametaka Serikali itoe kauli kuhusu kitendo hicho, akirejea kile ambacho kimeshasemwa na wengi kuwa amekiuka taratibu, lakini hawajaona hata Serikali kukemea kitendo hicho.
“Mheshimiwa Naibu Spika tunaomba kupata ufafanuzi wa jambo hili, Mkuu wa Mkoa kuwataka watumishi wawasilishe vitambulisho vyao kama ni maagizo ya Serikali au ameamua kufanya hivyo mwenyewe na hatua gani zinachukuliwa,” amesema.
Akitolea ufafanuzi hoja hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Hamza Hassan Juma, amesema bado hajavunja sheria, na hakuna mtu anayefuatwa kwa pingu kutoa kitambulisho, ila alitumia fursa hiyo kama njia ya kuhamasisha watumishi hao wajitokeze kupiga kura.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Hamza Hasan Juma akijibu hoja za Wawakilishi barazani
Amesema kuna baadhi ya watumishi huwa hawajitokezi siku ya kupiga kura kwa kuwa wanaona hakuna umuhimu kwao. Juma amesema hata yeye, Waziri Hamza, tayari ameshampelekea kitambulisho chake kukikagua.
“Hakuna aliyefuatwa na pingu kwamba mtu alete kitambulisho chake. Yeye amehamasisha, hata mimi tayari nimeshachukua hatua za kumuonesha kitambulisho changu, kwa hiyo bado hakuna kosa,” amesema Waziri Hamza.
Mei 5, Mwanasheria Mkuu wa ACT, Omar Said Shaaban, alisema kwa mujibu wa sheria hizo, alichokifanya Mkuu wa Mkoa ni cha kihalifu na kosa la jinai, huku akiwataka watumishi wasitishwe wala kutiwa hofu na kauli hiyo kwani ajira ni haki yao na siyo hisani. Wapo kwa mujibu wa Katiba.
“Upo pale kushiriki ujenzi wa nchi yako kutokana na kipaji na elimu uliyonayo.”
“Hii ni kauli ya aibu na kihalifu yenye nia ovu ya kuwatia hofu watumishi na viongozi katika mkoa huu wa Mjini Magharibi. Ni kauli ya kijinai, ukosefu wa maadili na mhemko wa kisiasa. Hili analotaka kufanya ni kuhamasisha uhalifu,” amesema Shaaban ambaye pia ni Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar.
Akifafanua namna sheria hizo zinavyovunjwa, Mwanasheria huyo amesema kifungu cha 118 (G) cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kinaeleza kwamba ni kosa mtu yeyote kuuza, kununua au kumpatia kitambulisho cha kupiga kura mtu ambaye hausiki.