Wasira: Historia imkumbuke Karume kama mpambanaji

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira akizungumza wakati wa kongamano la Saba la kumbukumbu ya kifo cha Abeid Amani Karume lililoandaliwa na kufanyika katika Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi ya Karume Zanzibar.
Muktasari:
- Ifikapo Aprili 7 kila mwaka Zanzibar huadhimisha kumbukizi ya kifo cha muasisi wa taifa hilo, Abeid Amani Karume na mwaka huu anafikisha miaka 53 tangu kifo chake mwaka 1972.
Unguja. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amesema historia ya Zanzibar haiwezi kuandikwa bila kumtaja muasisi wa taifa hilo, Abeid Amani Karume, au kuyataja mambo aliyoyafanya.
Amesema Abeid Amani Karume alipigania uhuru wa taifa hilo, kuondoa dhuluma iliyokithiri na kuleta haki kwa wote.
Wasira amesisitiza kuwa Karume anatakiwa akumbukwe kama mpambanaji wa kweli na kwa fikra zake ambazo ziliinua taifa hilo.
Kiongozi huyo ametoa kauli hiyo leo Aprili 3, 2025 katika kongamano la saba la kumbukizi ya kifo cha Karume lililoandaliwa na kufanyika katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi ya Karume Zanzibar.
Amesema lazima vijana wajue historia ya nchi yao kwani ni hatari mtu asiyejua anapotoka, hata anapokwenda anaweza kupotea.
“Niwakumbushe hasa vijana lazima tumkubuke Karume kama mpambanaji, haikuwa kazi rahisi kuleta mapinduzi kama wengine wanavyodhani, hivyo ipo haja kuisoma historia na kujua namna ilivyokuwa,” amesema Wasira ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi wa Chuo hicho
Wasira amesema mapinduzi yaliyofanyika Zanzibar yalikuwa kama yalivyofanyika katika mataifa mengine, lakini utofauti ni kwamba Zanzibar dhuluma ilikithiri kwa kiasi kikubwa jambo lililompa uchungu Karume na wenzake na kuamua kufanya mapinduzi.
“Walio wengi walinyimwa haki na wale wachache ndio walipewa haki, kwa asilimia kubwa watu wenye hali ya chini ndio walipata shida na kunyimwa haki zao,” amesema.
Pia, amesema hawawezi kuuzungumzia Muungano bila kumtaja Karume kwani bila yeye hata Muungano usingetokea maana alikubali kuacha nafasi yake kwa ajili ya Muungano.
“Huwezi kuyaandika hayo bila kumtaja Karume maana alileta usawa, elimu kwa wote na kuondoa dhuluma kunyimwa wenye haki na kupewa wasiokuwa na haki,” amesema.
Amesema Karume ndiye alikuwa kiongozi wa kwanza kukubali kuacha madaraka yake ya urais kwa ajili ya Muungano, na kwa sasa yanaonekana matunda mengi yaliyopo kwenye Muungano huo.
Amesema hata mafanikio yanayoonekana sasa ni fikra zake mwenyewe baada ya kufariki dunia, awamu zote za utawala zimekuwa zikiyaendeleza na kutekeleza mawazo yake.
Amewasihi wananchi kuendeleza mapinduzi na kwamba wakumbuke msingi wake ni amani, lakini wakiona ni tabu basi wajaribu shari, watakuja kujutia.
Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi ambaye alikuwa mgeni rasmi, Mgeni Hassan Juma amesema mchango wa Karume ni mkubwa na unastahili kuheshimiwa kwani jina lake halisahauliki sio tu Zanzibar, lakini Afrika kwani alijitoa kwa ajili ya Waafrika wote.
“Alikuwa na maono makubwa kwa Zanzibar na Afrika alileta ukombozi na watu kujiamulia mambo yao wenyewe kutoka kwenye minyororo ya wakoloni, hakika ndoto zake zinamchango mkubwa mpaka sasa, leo tunaona fikra zake kupitia sera ya uchumi wa buluu ambayo imekuwa ajenda kuu kwa Zanzibar,” amesema.
Kama alivyosema Wasira, Mgeni naye alitumia fursa hiyo kuwasihi vijana wapate mwamko wa kujua historia ili waelewe taifa lilipotoka, lilipo na linapoelekea kwa kupata maarifa ya kutosha iwapo wakisoma historia ya karume na kujua mawazo na fikra zake.
Amesema Karume anatakiwa kuenziwa kwa vitendo kwa kuzingatia tunu zilizoongozwa naye za upendo, amani, uadilifu, uwazi na mshikamano.
Awali, Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Profesa Haruni Mapesa amesema chuo hicho kinaendeleza falsafa za kiongozi huyo, ikiwa ni pamoja na kufundisha somo la maadili na uongozi vitu ambavyo vilizingatiwa zaidi katika harakati zake.
“Historia ni muhimu kwa vijana wetu kwani wazee wataondoka, hivyo wajibu utabaki kwa vijana ambao nao watafundisha vizazi vijavyo na kuendeleza historia,” amesema.