Wasira: Waulizeni Chadema watazuiaje uchaguzi, Lissu awasikilize wenzake

Muktasari:
- Wasira ahoji njia ipi Chadema watatumia kuzuia uchaguzi mkuu 2025 usifanyie, ikiwa mchakato umeshaanza, amtaka Lissu kufikiria upya uamuzi wa chama chake, huku akiwafunda wasomi Tanzania wasidharau elimu ya Veta.
Kahama. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM)-Bara, Stephen Wasira amehoji ni njia ipi, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kitaitumia kuzuia kufanyika uchaguzi mkuu 2025, ikiwa mchakato wake umeshaanza kwa kuboresha taarifa kwenye daftari la kudumu la mpigakura.
Wakati akieleza hay oleo Alhamisi, jana Jumatano, Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akihutubia mkutano wa hadhara Mjini Sumbawanga mkoani Rukwa, alisema kugomea kila watakacho kuwa wanaambiwa na Serikali ni miongoni mwa njia watakayotumia kuzuia uchaguzi usifanyike.
Msingi wa msigano wa pande hizo mbili, ni baada ya Chadema kusema haitashiriki uchaguzi na kuja kampeni ya 'No reforms no election' inayolenga kuishinikiza Serikali kufanya mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi ili kutoa fursa kwa wananchi kuchagua viongozi wanaowataka.
“Chochote wanachopendekeza tukisusie, tukikatae kila watakachotuletea tukikatae na nimeangalia sheria za nchi sijaona sehemu kama tukikataa kwenda kupiga kura ni dhambi au tumevunja sheria lakini ukweli wa Mungu ni kwamba hata kwa Katiba hii inawezekana kuahirisha uchaguzi,” alisema Lissu.
Leo Alhamisi, Machi 27, 2025, akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika mji wa Kahama ikiwa ni muendelezo wa ziara ya kukagua utekelezaji wa ilani ya CCM, Wasira amesisitiza hakuna mwenye uwezo wa kuzuia uchaguzi huo: “Labda wawe wanaota ndoto ya mchana.”

Wasira amesema pamoja na kampeni wanazoendelea kuzifanya, hawana uwezo wa kuzuia uchaguzi usifanyike kwa sababu tayari hatua ya kwanza ya uchaguzi huo imeanza kwa wananchi kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la mpiga kura.
“Nasikia wanazunguka nchi nzima wakifika hapa Kahama, muwasikilize halafu muwaulize mnatumia njia gani ya kuzuia uchaguzi maana Katiba inakataa, inasema hakuna uchaguzi kuahirishwa kama kuna vita na hata kama ikiwepo vita, wanasema kwa miezi sita ndio unaweza kuahirisha ili vita iishe," amesema na kuongeza;
“Hakuna jambo jingine linaweza kuzuia uchaguzi, lakini wamesisitiza wanaweza kuuahirisha, sasa muwaulize wanatumia mbinu gani kuuairisha, halafu niliwaambia nilipokuwa Bukoba, mbona uchaguzi umeshaanza maana Dar es Salaam wamemaliza kujiandikisha na kujiandikisha ni sehemu ya uchaguzi,” amesema.
Kiongozi huyo amesema ni muhimu kwa Lissu kukubali kubadili msimamo wake kushiriki uchaguzi huo badala ya kuendelea kuweka mpira kwapani, hawezi kuwajenga zaidi ya kuua ndoto za wanaotaka kuwania ubunge na udiwani.
"Utaratibu wa uchaguzi baada ya wananchi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura, hatua zinazofuata ni kuweka wagombea na tume kuwapokea ikiisha hatu hiyo kinachobakia tume kuwapokea na kuanza kufanya kampeni.
"Sasa watazuia kampeni, yaani mimi hivi Makamu Mwenyekiti wa chama kikubwa wanizuie kuja Shinyanga kuomba kura, nitakuja tu watanifanya nini? Sheria inasema ukizuia mtu kwenda kutimiza haki yake ni kosa la jinai, hivyo wakija muwaulize mnatumia mbinu gani wakikosa majibu mjue hao ni watu hatari na mnatakiwa kuwaogopa kuliko ukoma," amesema.
Kulingana na maelezo ya Wasira amesema kinacho mfurahisha ni baada ya kuona makada wamegawanyiika kuna wanaopinga msimamo huo na kuona hauna maana na waruhusiwe kwenda kugombea.
“Sasa hapo kuna chama? Na wanachama wengine wa Chadema wapo wamejificha lakini wanasema wanataka kugombea udiwani huyu anatuchelewesha, mimi sikutumwa kuwa msaidizi wao, lakini ni vizuri awasikilize basi.
“Mbona sisi tumesikiliza naye awasikilize watu wake wanavyosema, ameng'ang'ania jambo ambalo hawezi kulitekeleza. Wabunge wanamaliza ubunge wao Juni 27 mwaka huu, nani atatunga sheria mpya ya uchaguzi wabunge wenyewe ndio hawa hapa presha iko juu," amesema Wasira.
Amesema sasa ni wakati wa kwenda kwenye uchaguzi halafu mazungumzo mengine yataendelea kwa kuwa Tanzania ipo haijahama wala Tanzania haipo kwa miezi mitatu ijayo.
Elimu ya Veta
Katika hatua nyingine, Wasira amewataka Watanzania kutumia vyema fursa ya elimu ya mafunzo ya ufundi stadi (Veta) yanayotolewa na vyuo hivyo nchini badala ya kubeza na kuyafanyia dhihaka mawazo yanayotolewa na viongozi wa juu kuhusu elimu hiyo.
Ushauri wa Wasira umekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwasisitiza wasomi nchini kujiunga na elimu ya Veta ili kuondoa changamoto ya ajira kwa kila mmoja kuwa na ujuzi na kujiajiri.
"Kasi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa madarasa pamoja na uboreshaji wa elimu ya juu ni kubwa hapa nchini, wasomi msione aibu kujiunga na Veta ili kuongeza ujuzi binafsi utakaowasaidia kujikwamua kiuchumi na kuongeza pato la Taifa,” amesema.
Amesema Serikali inaanza mfumo wa kuwekeza kwenye ujuzi wa vijana haswa wanaohitimu elimu ya juu ili waweze kujiajiri badala ya kubaki mtaani na kulalamikia ukosefu wa ajira.
"Mzee wangu (Jumanne) Kishimba (Mbunge wa Kahama) alisema bungeni suala la sera, kwamba lazima ukimpeleka mtoto shule akitoka awe anajua kazi ya kufanya, na sasa hivi ndio serikali inabadili kabisa mfumo wa elimu,” amesema Wasira.
Mbali na Wasira katika mkutano huo, Mjumbe wa Halimashauri Kuu ya CCM, Richard Kasesela amesema amewahi kuwa mwenyekiti wa bodi ya madini, kuna changamoto kubwa kwa wamiliki wa mashamba.
"Ni muhimu kuliangalia hili kwa upana wake kama ni mwekezaji kama unafaidika lazima na wenye mashamba watajirike. Lakini pia tuwaangalie wachimbaji wadogo," amesema Kasesera.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kutoka Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela amesema Kahama ni mji wa biashara ambao umedumu kwa muda mrefu zaidi na zimekuwa zikiimarika siku hadi siku.
“Kwa kutambua hilo, Serikali imeunda tume ya kuangalia na kusikiliza malalamiko ya wafanyabiashara na kuyafanyia kazi ili kuleta unafuu kwao,” amesema.