Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wakulima wa mwani walia zao hilo kushambuliwa, wataka utafiti

Wadau wa Kilimo wakionyesha bidhaa mbalimbali zinazotokana na kilimo katika viwanja vya maonyesho ya Kilimo Nanenane Kizimbani Zanzibar.

Muktasari:

  • Wamesema kwa kipindi kirefu zao hilo limekuwa likishambuliwa na maradhi ambayo yanasababisha mwani wanaootesha mashambani kutoota.

Unguja. Wakulima wa mwani wamesema wanasumbuliwa na maradhi katika zao hilo, hivyo kuiomba Serikali na wadau wengine kufanya utafiti kubaini kiini cha magonjwa hayo yanayowarudisha nyuma.

Wakizungumza katika kikao kilichowashirikisha wadau wa maendeleo kutoka UNDP, Chuo kikuu cha Dar es Salaam na Chuo cha Mipango Julai 20, 2024 wakulima wa hao wamesema iwapo maradhi hayo yataendelea kuna hatari ya kupoteza mwelekeo katika kilimo hicho.

Wamesema kwa kipindi kirefu zao hilo limekuwa likishambuliwa na maradhi ambayo yanasababisha mwani wanaootesha mashambani kutoota  na kuwafanya wapunguze uzalishaji wake.

Simni Haji ni mkulima wa mwani katika Shehia ya Uroa,  amesema wananunua mbegu za mwani zikiwa katika hali nzuri lakini wakizipanda katika mashamba yao zinakatika vipande vidogovidogo na baadaye huoza.

“Tunaomba utafiti wa zao hili, tunapata hasara kwa sababu mbegu zinaoza. Unanunua zikiwa nzuri ila ukipanda hazioti, tatizo hili limekuwa la muda mrefu,” amesema

Mkulima mwingine wa zao hilo kutoka Chwaka, Fatma Ali Rajabu amesema katika kijiji chao pia wanaathiriwa na maradhi ya mwani ambapo kwa sasa baadhi ya wakulima wameacha kulima zao hilo.

Kwa upande wake,  Ali Abdalla Ali ameshauri kwa hatua za awali kuangaliwa uwezekano wa kupatiwa mbegu nyingine ili kubaini iwapo mbegu wanazotumia  zinasababisha maradhi au vinginevyo.

Pia ameomba kupatiwa mabwana shamba wanaohusika na utaalamu wa zao hilo ili wawe wanawapitia mara kwa mara katika mashamba yao, kwa ajili ya kuangalia kama mwani umeshaanza kushambuliwa na maradhi ili kuchukua hatua za mapema.

Kwa upande wake,  Mkurugenzi wa Uratibu Uchumi wa Buluu, Christopher Mhando amesema lengo la kukutana na wakulima wa mazao ya baharini ni kutanua wigo wa kuwatoa eneo moja kwenda lingine ambayo itakuwa na tija zaidi.

Amesema Serikali imeleta wataalamu kwa wakulima wa mwani na wafugaji wa kaa na matango bahari, kutokana na changamoto nyingi zinazojitokeza kwa wakulima ili kuondoa upungufu uliokuwepo ili kuwa wazuri katika shughuli zao.

Naye ofisa Mkuu wa Uvuvi, kutoka Idara ya Maendeleo ya Uvuvi na Mazao ya Baharini,  Mohammed Soud amesema ushirikiano wa pamoja unahitajika kutokomeza uvuvi haramu unaosababisha kutoweka kwa baadhi ya samaki wanaokula wadudu hivyo kuwafanya wadudu wanaoathiri zao hilo waongezeke baharini.


“Serikali inatambua kuwepo kwa changamoto ya bei ya mwani ndiyo maana ikaona haja ya kujenga kituo cha Chwamanangwe Pemba ili kuleta ushindani wa bei kwa Serikali na kampuni binafsi kwa lengo la kumnyanyua mkulima wa zao hilo nchini,” amesema

Kwa upande wake Veronika Sigalla kutoka UNDP amesema lengo la kukutana na wakulima wa mwani, ni pamoja na kuangalia namna ya wakulima hao wanavyoweza kulima zao hilo katika kiwango cha kimataifa ili kuongeza thamani.

Amesema wakulima wa mwani ni wadau wakubwa katika kuitumia bahari, hivyo amewataka kutunza mazingira ya bahari isaidie kuwanufaisha zaidi.

Naye Mratibu wa kilimo, Dk Banamas Mbasa amesema wamebaini changamoto ya ubora katika maandalizi ya ukaushaji wa mwani,  hivyo wataandaa mafunzo maalumu ya kuwaelimisha wakulima hao namna nzuri ya kuwakausha waepukane na changamoto ya kukosa ubora na kushusha bei ya zao hilo katika soko.