Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Madalali, sera mbovu chanzo kukwama kilimo cha mwani

Wadau wa zao la mwani nchini wakijadili changamoto zinazowakabili katika uzalishaji wa zao hilo katika mkutano uliofanyika leo jijini Dar e s Salaam.

Muktasari:

  • Katika kuhakikisha maendeleo kwenye uchumi wa buluu wadau wa zao la mwani wamekutana kujadili changamoto zinazowakabili huku wakieleza mwarobaini.

Dar es Salaam. Wadau na wakulima wa zao la mwani nchini wametaja teknolojia, bei ya chini, madalali na sera mbovu kuwa changamoto katika kilimo hicho.

Wakizungumza jana Juni 5, 2024 katika mkutano wa pembeni ulioandaliwa na Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF) jijini Dar es Salaam, baadhi ya wakulima wamesema soko la mwani bado halijatengemaa pamoja na uelewa mdogo wa zao hilo kwa Watanzania.

“Ufahamu wa faida za mwani bado ni changamoto miongoni mwetu, nashauri viandaliwe vipindi kwenye televisheni watu waelimishwe kuwa zao hili ni tiba pia. Vilevile mwani huwa inashuka ubora ikianikwa chini kutokana na ukosefu wa teknolojia,” amesema Kombo Kizanda mkulima wa zao hilo kutoka Mafia.

Dk Flower Msuya ambaye ni Mtafiti Mwandamizi na mshauri wa kujitegemea amesema changamoto nyingine ni ukosefu wa ushirikiano miongoni mwa walimaji wa zao hilo.

“Pia, lazima kuwe na eneo maalumu lenye kutambulika miongoni mwao ili kuepusha migogoro. Aidha tufanye uwekezaji wa kutosha katika eneo hilo,” amesema Dk Msuya.

Aidha, Kiongozi wa Programu ya baharini kutoka WWF Tanzania, Dk Modesta Medard amesema watu wa kati wanaopanga bei kutoka kwa wakulima wa zao hilo wamekuwa ni tatizo kwani hawampi mkulima nafasi ikiwa yeye ndio mzalishaji.

“Tunataka bei iwe ‘fair’ lazima kuwe na nguvu ya majadiliano ykwa wakulima wenyewe na si kwa madalali ambao wanasimama kama watu wa kati ya mkulima na mnunuzi,” amesema.

Aidha wadau hao wametaka mwani iuzwe ikiwa mbichi sambamba na kuweka mchakato wa kuliuza zao hilo likiwa bichi kama mazao mengine ya bahari mfano samaki.

Katika kujibu hayo Serikali kupitia Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Nazael Madalla amesema suala lililopo ni uwepo wa sera, mikakati na mipango kazi pamoja na mamlaka ya kutambua eneo la kilimo hicho.

Aidha amesema wameyapokea yale yote waliyoyashauri ikiwemo teknolojia ya ukaushaji wa zao hilo huku akiimiza wadau kama WWF kuibua teknolojia nyingi zaidi.

Katika jitihada za kuelimisha jamii amesema ndio maana wanakuwa na maonyesho ili Watanzania waelewe juu ya zao hilo.

Wakati Dk Madalla akiyasema hayo kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Serikali ya mwani chini ya Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Zanzibar (Zasco), Dk Masoud Rashid Mohamed amesema kwa kutambua hayo ndio maana wakaamua kujenga kiwanda kikubwa cha mwani visiwani Zanzibar.

“Tunataka tuzalishe mamilioni ya tani zamwani kwa juhudi za Serikali na kinatarajiwa kuanza hivi karibuni ambapo wakulima watapeleka mazao moja kwa moja bila kupitia kwa watu wa kati na bei itakuwa bora zaidi.

“Tunataka bei ya zao hili huko mbeleni ifikie angalau bei ya kilo ya mchele unajua mwani inafaida kemkem ikiwemo kuhifadhi hewa ukaa,” amesema.

Awali, Mkurugenzi wa WWF nchini, Dk Amani Ngusaru alisema lengo lao ni kusaidiana na Serikali katika kukuza sekta hiyo ikiwemo kuvumbua teknolojia mbalimbali na kuongeza uzalishaji.