Pemba kupata soko la uhakika la mwani

Muktasari:
- Ni baada ya kusainiwa hati ya ushirikiano na uendeshaji wa kiwanda cha kuchakata mwani baina ya Kampuni ya Mwani Zanzibar (Zasco) na kampuni Nutri-san ya Uingereza.
Unguja. Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaaban amesema hatua ya kusaini mkataba wa uendeshaji wa kiwanda cha kuchakata mwani Chamanangwe kisiwani Pemba, inaakisi jitihada za Serikali kukuza uchumi wa Zanzibar.
Amesema hayo leo Novemba 23 wakati wa utiaji saini hati ya ushirikiano na uendeshaji wa kiwanda hicho baina ya Kampuni ya Mwani Zanzibar (ZASCO) na kampuni Nutri-san ya Uingereza katika hoteli ya Verde Mtoni.
Amesema sekta ya uchumi wa buluu, ni mtambuka kwani inagusa sekta mbalimbali ikiwemo kilimo cha mwani ambacho ni ahadi mpya katika kuimarisha uchumi visiwani humo na hivyo kumkomba mwananchi ambapo anapata fursa ya kujiongezea kipato kwa kuwa kuna soko la uhakika.
Waziri huyo amesema kwa wastani wa miaka 40, Zanzibar imekuwa ikijishughulisha na kilimo hicho na kwamba shughuli hiyo inafanya Zanzibar kuwa miongoni mwa wazalishaji wa mwani duniani.
“Kwa kipindi chote hicho shughuli hii imehusisha kuuza mwani ghafi katika masoko ya nje na hatua hii inaaminika kuchangia kwa bei ndogo ya ununuzi wa zao hilo,” amesema.
Amefahamisha kuwa katika jitihada za kukabiliana na hali hiyo hasa ya bei ndogo ya mwani Serikali imekuja na mikakati mipya ambayo inahusisha kuongezea thamani mwani hapa nchini na kuuza mazao yake nje ya nchi.
Ameeleza Serikali imeamua kujenga kiwanda cha kuchakata zao hilo chenye uwezo wa kusarifu wastani wa tani 30,000 kwa mwaka.
Waziri huyo amesema lazima jitihada za makusudi zichukuliwe, ili kuhakikisha kiwanda kinapata mwani ya kutosha kila inapohitajika na kuwataka wakulima na wadau kuongeza uzalishaji kwa wingi kwani soko la uhakika la mwani limefika.
Aidha, amemshauri mkurugenzi wa uwezeshaji wananchi kiuchumi kuelekeza nguvu kuwawezesha wakulima wa zao hilo, ili kuona mradi huo unafanikiwa katika kupata mwani wa kutosha, kwani sasa uzalishaji wa mwani ni tani 12,000 ambazo ni kidogo ukilinganisha na uwezo wa kiwanda.
Pamoja na hayo, amesema ni imani yake utekelezaji wa mkataba huo utafikia dhamira ya Serikali ya kutumia uchumi wa buluu katika kuimarisha uchumi wa nchi na kipato cha wananchi wake.
“Serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji ikiwemo kutunga sera nzuri zenye kuwavutia wawekezaji na usimamizi wa vifungu vya mkataba vitakavyotakiwa kutekelezwa jambo ambalo litawapa imani wawekezaji na kuongeza uwekezaji nchini,” amesema.
Sambamba na hayo, amewataka wabia hao kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao, ili kujenga imani kwa wawekezaji wapya watakaokuja katika viwanda, viwanda vidogo vidogo na vya kati.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mwani Zanzibar, Dk Masoud Rashid Mohammed amesema kampuni hiyo inajishughulisha na uchakataji wa mwani, hivyo makubaliano hayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa wakulima wanaozalisha zao hilo kukuza vipato vyao na kuunganishwa na masoko.
Amesema mpaka sasa kampuni hiyo imeshatumia Sh4.593 bilioni katika uwekezaji huo ambapo Juni mwakani wanatarajia kuanza uzalishaji katika kiwanda hicho.
Amesema kwa sasa dhana ya uchumi wa buluu imeanza kukua kwa kasi, kwani Serikali imeipa kipaumbele cha hali ya juu, ili kuona Zanzibar inakuwa kiuchumi ukiachia sekta ya utalii.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Nutri- San kutoka nchini Uingereza, San Chau amesema wamevutiwa na kiwanda hicho na wapo tayari kufanya ubia na Serikali kwa ajili ya kuendesha kiwanda hicho, kwani kitakuwa ni kiwanda pekee duniani kinachozalisha tarajina na kitafungua fursa nyingi.
Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM), Komodoo, Azana Hassan Msingiri, ambaye ni mkandarasi wa kiwanda hicho amesema tayari kiwanda hicho tayari kimeshakamilika na sasa wanakwenda katika makubaliano ya pili kumalizia majengo ya utawala.