Ripoti yabainisha wazawa wawekwa kando fursa za ajira

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla (kushoto) akimweleza jambo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi Uchumi na Uwekezaji Shariff Ali Shariff wakati wa kikao cha baraza la wawakilishi Chukwani Unguja Zanzibar
Muktasari:
- Imebainika kuwa vijana wengi hukosa ajira si kwa sababu ya ukosefu wa nafasi pekee, bali pia kutokana na kutokidhi vigezo vinavyohitajika, ikiwamo ukosefu wa utayari wa kujiendeleza kitaaluma na kimuundo
Unguja. Wakati wimbi la vijana likiendelea kukumbwa na ukosefu wa ajira, ripoti ya utafiti wa ajira na mapato katika sekta rasmi kwa mwaka 2022/23 imebainisha kuwa, nafasi nyingi za ajira bado hazijajazwa, hasa katika kada ya mafundi stadi na wataalamu wa fani zinazohusiana nao.
Kati ya nafasi zote za ajira zilizokuwepo mwaka 2022/23, asilimia 38.6 zilihitaji wataalamu wa kada hiyo.
Kwa mwaka 2023/24, mahitaji ya wataalamu hao yaliongezeka na kufikia asilimia 41.5, huku makadirio ya mwaka 2024/25 yakionesha kushuka kidogo hadi asilimia 40 ya jumla ya mahitaji ya ajira.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff, leo Juni 10, 2025, wakati akijibu maswali ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika mkutano wa 19 unaoendelea huko Chukwani, Zanzibar.
Waziri Shariff amesema kuwa, licha ya malalamiko kutoka kwa vijana kuhusu ukosefu wa ajira, bado zipo fursa nyingi za ajira zinazopatikana.
Hata hivyo, changamoto kubwa ni kwamba baadhi ya Wazanzibari hawajitokezi kwa wingi kujifunza na kujiendeleza kielimu, jambo linalowafanya washindwe kukidhi vigezo vinavyohitajika katika soko la ajira.
Katika muktadha huo, Waziri amesema hali hiyo imesababisha nafasi nyingi za ajira, hasa katika sekta kama za hoteli na utalii, kuchukuliwa na wageni kutoka nje ya Zanzibar kutokana na upungufu wa vijana wenye sifa stahiki.
“Vijana wengi hawapendi kujifunza, wajitoe wajifunze hata fani za ufundi, fursa zipo lakini hatupati watu wenye sifa wanaotakiwa na ndio maana wanatoka watu nje kuja kuchukua ajira hizo, kwakweli hii ni changamoto kubwa kwetu,” amesema.
Ametolea mfano wa Indonesia akisema asilimia 100 ya ajira zake zinatoka ndani kwa sababu wamejikita kujifunza na kuchangamkia fursa hizo.
Katika swali lake la msingi mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohammed Ali Suleiman amesema kumekuwapo na ongezeko kubwa la vijana wa Zanzibar wanaomaliza masomo vyuo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi.
Amesema vijana wengi ambao wamemaliza masomo bado hawajafanikiwa kupata ajira rasmi jambo linaloleta maswali mengi kwenye mifumo ya elimu akitaka kujua takwimu rasmi ya vijana waliohitimu vyuoni lakini hawana ajira.
Pia, alitaka kujua taaluma zipi zina fursa nyingi na zipi zina fursa chache za kujiajiri au kuajiriwa baada ya kuhitimu.
Akijibu hilo, Waziri Shariff amesema hakuna takwimu rasmi za wahitimu, takwimu chache zinaratibiwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, hata hivyo, takwimu hizo za vyuo vikuu vikubwa vya Zanzibar zinaonesha kuwa, kuanzia 2020/21 hadi 2023/24 kupitia vyuo vikuu vitatu vilivyopo nchini jumla ya vijana 12,820 wamehitimu.
Amesema kwa sasa wizara kupitia mradi wa Sebep ambao uko chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, inaendelea na utafiti wa soko la ajira ili kufahamu kwa kina ni fursa zipi zipo kwa sasa na baadaye.
Utafiti huo pia unatarajiwa kuonesha upungufu wa ujuzi na aina ya ujuzi unaohitajika kwa sasa na baadaye.
Waziri Shariff amesema taarifa zinaonesha kuwa hadi kufikia Septemba 2024, jumla ya ajira 233,615 zimepatikana ndani ya nchi, asilimia 49.61 ni wanaume na 48.59 wanawake.