Rais Mwinyi: Kunahitajika ubunifu sekta ya habari kusaidia utulivu Afrika

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akizungumza wakati akifungua mkutano wa 30 wa Umoja wa vyombo vya utangazaji vya umma kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SABA) Unguja, Zanzibar leo Oktoba 10, 2023.
Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema kunahitajika ubunifu kuhakikisha sekta ya habari na utangazaji vinakuwa nyenzo ya kutoa taarifa sahihi kwa wananchi ili kusaidia utulivu na amani hatua itakayoimarisha ushirikiano kati ya Serikali na jamii katika bara la Afrika.
Amesema vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika ukuaji wa uchumi, utengamano wa kitaifa na ustawi wa kisiasa hususani mwa bara hilo.
Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumanne Oktoba, 10, 2023 wakati akifungua mkutano wa 30 wa vyombo vya utangazaji vya umma kwa nchi za Kusini mwa Afrika (Saba) uliofanyika Unguja, Zanzibar.
“Sote ni mashahidi wa namna vyombo vya utangazaji na habari vikiwemo vyombo vya umma vya nchi zetu za Afrika vilivyo na umuhimu mkubwa katika kutoa taarifa zinazochangia maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kisiasa, kiutamaduni na kujenga amani, utulivu, usalama na utengamano wa nchi zetu,” amesema Dk Mwinyi.
Dk Mwinyi amesema Tanzania imeweka dira ya kuweka mazingira wezeshi ambayo yatachochea na kukuza uchumi kwa kasi kwa kuwa na ushirikiano na nchi nyingine, kushirikisha sekta binafsi na kukuza uwekezaji katika sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).
Katika Mkutano huo wa siku tatu, miongoni mwa mada zitakazojadiliwa ni mchango wa Tehama katika ukuaji wa uchumi wa kidijitali kwa mataifa ya Afrika na maendeleo endelevu ambapo Rais Mwinyi alisema ni wakati mwafaka kipindi hiki ambacho dunia inashughulikia wimbi la mapinduzi ya nne ya viwanda inayochagizwa Tehama.
“Mashirika ya umma ya utangazaji ya nchi wanachama wa Saba na Afrika kwa ujumla hayana budi kubuni, kusimamia na kutekeleza mikakati madhubuti inayopimika ya kuwezesha mashirika hayo kwenda sambamba na mabadiliko yanayojitokeza,” amesema Dk Mwinyi.
Hata hivyo, amesema wasipokuwa tayari kubadilika wakati utawalazimisha kubadilika, huku athari ya kusubiri kubadilishwa na wakati zinaweza kuwa hasi na pengine kufanya mashirika ya utangazaji ya umma kupoteza mvuto kwa umma.
Rais wa Umoja huo, Stanley Benjamin Similo alisema kiini na mkutano huo ni kuangali jinsi Tehama inavyochangia maendeleo ya utangazaji.
Alisema zipo changamoto zinavyozikabili vyombo vya habari vya umma na watafiti wameonyesha jinsi wafuatiliaji wa maudhui ya vyombo vya habari vya umma wanazidi kupungua wakikimbilia kwenye mitandao.
Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Tanzania, Kundo Methew amesema wanasisitiza matumizi ya Tehama kufikia malengo ya mapinduzi ya ukuaji wa uchumi na vyombo vya habari vinajukumu kusukuma ajenda hiyo.
“Tasnia ya habari ni nguzo muhimu, jitihada mahusii lazima zifanyike kupitia vyombo vya utangazaji, maudhui yanayoandaliwa na vyombo vya habari vya umma yazingatie mitazamo ya kuijenga jamii ikiwa na uwezo wa kujitambua na kujivunia uafrika wao,” alisema
Amesema kimefika kipindi teknolojia haikwepeki tena ama kwa kutaka au kutotaka na kwamba kwamba wapo wnaopata hofu kazi zao kuchukuliwa na akili bandia.
“Kinachotakiwa kama taifa au Afrika ni kubadilisha mitazamo ya akili zetu li kuendana na hali halisi na hakuna anayebaki nyuma kwa Afrika kwa hiyo tunaweza kuwa na lugha moja kutembea kama wamoja siyo kuona nchi jirani zinakuwa washindani bali ni kubebana,” amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji (TBC), Dk Ayub Rioba amesema mkutano huo ni mara ya tatu kufanyika Tanzania ambapo watakuwa na mafunzo kuangalia namna vyombo vya umma viendelee kuishi licha ya kuwapo wanaodhani kwamba vimepitwa na wakati.