Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbeto: Mwinyi aliwatengeneza matajiri tulionao sasa

Rais mstaafu Hayati  Ali Hassan Mwinyi

Muktasari:

  • Hayati Ali Hassan Mwinyi alifariki Februari 29, 2024 akiwa na umri wa miaka 98. Alikuwa ni mume wa wake wawili na alijaaliwa kupata watoto 12, sita wa kike na sita wa kiume.

Unguja. Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis amesema Rais mstaafu, Hayati Ali Hassan Mwinyi,  ndiye aliyewatengeneza matajiri wakubwa waliopo sasa kupitia uamuzi wake wa kufungua uchumi kwa kuruhusu sekta binafsi kufanya kazi nchini.

Mbeto amebainisha hayo leo Jumamosi Machi 2, 2024 katika hafla ya kumuaga kiongozi huyo iliyofanyika katika Uwanja wa New  Amaan  Complex ambapo maelfu ya wananchi wamehudhuria kutoa heshima zao za mwisho.

Akizungumzia alivyomfahamu Mzee Mwinyi, Mbeto amesema wakati anaingia madarakani, njia kuu za uchumi zilikuwa zikimilikuwa na umma, lakini Mzee Mwinyi alifungua mambo na yakafunguka.

"Matajiri wengi mnaowaona sasa, Mzee Mwinyi ndiye aliwatengeneza kwa kuwaruhusu kufanya biashara kama sekta binafsi," amesema Mbeto.

Mbeto ameongeza kwamba wakati anatafutwa Rais atakayechukua nafasi ya Mwalimu Julius Nyerere, kulikuwa na majina matatu, Rashid Kawawa, Salim Ahmed Salim na Mwinyi.

Amesema baadaye Kawawa alijiondoa mwenyewe, yakabaki majina mawili; Mwinyi na Salim na hatimaye wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM wakamchagua Mwinyi.

"Mzee Mwinyi ni mtu mwenye historia kubwa hasa katika kujenga uchumi na kuwasaidia wananchi. Alikuwa na upeo wa kulea watoto ili kujenga upendo," amesema Mbeto wakati akizungumza na Mwananchi.

Kwa upande wake, mbunge wa Morogoro Mjini, Abdulaziz Mohamed Abood amesema Mzee Mwinyi alifungua uchumi wa Zanzibar na kipindi chake wafanyabiashara wakaanza kuingiza bidhaa mbalimbali na wananchi wakaanza kujipangia bidhaa muhimu.


Amesema wakati akiwa Rais wa Zanzibar, alianzisha sera yake iliyosema "Zanzibar ni njema, kila atakaye aje" ambayo iliwavutia wafanyabiashara wengi kwenda Zanzibar kufanya biashara mbalimbali na kukuza uchumi.

"Tutamkumbuka kama kiongozi aliyetutoa kwenye kisiwa, maisha ya wananchi yalikuwa magumu lakini alifungua milango, hali ikawa nzuri," amesema Abood.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema wakati hayati Mwinyi anaingia madarakani, hakukuwa na fedha za kigeni nchini na mazungumzo na mashirika ya fedha duniani yalikwama.

Amesema alifanikiwa kurejesha uhusiano ya mashirika ya kifedha na Tanzania ikapata misaada na kufungua uchumi wake, bidhaa muhimu ziliingia nchini na kutoa nafasi kwa sekta binafsi kuwekeza nchini ikiwemo kwenye sekta ya habari ambapo televisheni na redio binafsi zilianzishwa.

"Wakati akiwa Rais, Mwalimu Nyerere alikuwa mwenyekiti wa chama (CCM), lakini aliweza kufanya mabadiliko makubwa ya msingi.

"Mwaka 1986, aliwashawishi CCM na Serikali, mwaka 1986, akaanza safari ya mabadiliko ya kiuchumi. Yeye ndiye aliyeanzisha ushiriki wa sekta binafsi katika ujenzi wa Taifa," amesema Profesa Lipumba.