LIVE: Viongozi washiriki mazishi ya hayati Mwinyi

Baadhi ya viongozi wastaafu wakiwa katika hafla ya kumuaga hayati Ali Hassan Mwinyi Uwanja wa New Amaan Zanzibar
Muktasari:
- Anatarajiwa kuzikwa baadaye leo eneo la Mangwapwani Unguja
Unguja. Viongozi mbalimbali wamehudhuria mazishi ya kitaifa ya Rais mstaafu wa awamu ya pili, hayati Ali Hassan Mwinyi, akiwemo Makamu wa Rais wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah.
Hayati Mwinyi alifariki dunia saa 11:30 jioni ya Februari 29, 2024 katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu ya saratani ya mapafu na anatarajiwa kuzikwa nyumbani kwake, Mangapwani, Zanzibar, leo Jumamosi, Machi 2, 2024.
Miongoni mwa watu mashuhuri waliohudhuria msiba huo ni Makamu wa Rais wa Namibia, Nandi-Ndaitwah ambaye ameteuliwa kushika wadhifa huo Februari 2024 baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Taifa hilo, Dk Hage Geingob.
Nandi-Ndaitwah aliwahi kufanya kazi na Rais Mwinyi mwaka 1985 - 1986 wakati alipokuwa akiishi hapa nchini kama mwakilishi wa chama cha Swapo. Ameishi Dar es Salaam kwa muda wa miaka sita.
Kati ya mwaka 1976 – 1978, Nandi-Ndaitwah alikuwa akifanya kazi kama naibu mwakilishi wa Swapo katika nchi ya Zambia na baadaye mwaka 1978 – 1980, alipanda cheo na kuwa mwakilishi mkuu wa chama hicho nchini humo.
Baadaye mwaka 1980 – 1986, aliteuliwa kuwa mwakilishi mkuu wa SWAPO wa Afrika Mashariki na makao makuu yake yalikuwa Dar es Salaam, Tanzania. Hivyo, ameishi Tanzania na anazungumza kidogo lugha ya Kiswahili.
Nandi-Ndaitwah ameshiri kikamilifu katika mapambano ya kupigania ukombozi wa taifa hilo akiwa ndani na nje ya nchi yake hadi hapo walipopata uhuru mwaka 1990 na SWAPO kuunda Serikali.
Mbali na Nandi-Ndaitwah, viongozi wengine wanaoshiriki hafla ya kumuaga Hayati Mwinyi ni Rais Samia Suluhu Hassan, Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi.
Wengine ni Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Abdulla Suleiman na Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda.
Shughuli ya kuuaga mwili huo unafanyika katika Uwanja wa Aman ambapo wananchi wengine wamejitokeza kumuaga kiongozi huyo. Mwinyi maarufu Mzee Rukhsa amewahi kuwa Rais wa Zanzibar, 1984 hadi 1985. Na Mwaka 1985-1995 alikuwa Rais wa Tanzania.
Tayari jeneza lenye mwili wake limekwisha kuwasilia uwanjani hapo likifikishwa na gari maalum la Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Endelea kufuatilia Mwananchi