Maslahi ya walimu Zanzibar kuboreshwa shule zikijengwa ghorofa

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi akisistiza jambo  katika muendelezo wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo kwa  kipindi cha miaka mitatu ya utawala wake.

Muktasari:

  • Rais wa Zanzibar amesema ataendelea na ujenzi wa shule nyengine mpya za ghorofa kwa kutumia fedha za ndani.

Unguja. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi amesema Serikali itaendelea na ujenzi wa shule za ghorofa kupitia fedha za ndani kwa lengo la kuleta maendeleo zaidi kupitia sekta ya elimu huku akiahidi kuboresha maslahi ya walimu.

 Rais Mwinyi ameyasema hayo leo Jumanne Oktoba 24, 2023 katika shehia ya donge mkoa wa kaskazini Unguja wakati wa ziara yake ya kukagua miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo sekta ya elimu.

Ziara hiyo ya Rais Mwinyi kukagua miradi ya maendeleo inakuja huku Zanzibar ikiwa inaekelea kilele cha maadhimisho ya miaka mitatu ya utawala wake tangu alipoapishwa kuitumikia Zanzibar baada ya kumalizika uchaguzi mkuu mwezi oktoba mwaka 2020.

Miongoni mwa aliyoyafanya ni pamoja na kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa skuli ya msingi Donge na kupata fursa ya kuzungumza na walimu na wanafunzi wa eneo hilo.

Pamoja na hayo Rais Mwinyi ameahidi kuboresha maslahi zaidi ya walimu ili waweze kufanya kazi katika mazingira mazuri zaidi na kutoa elimu bora kwa maslahi ya wote.

Akiendelea kueleza mafanikio ya utawala wake alisema anajua wapo baadhi ya watu wachache wamekua wakibeza maendeleo kutokana na kuzibwa kwa mianya na sasa fedha nyingi zimekua zikielezwa kwenye miradi ya maendeleo.