Jaji Mkuu: Kesi nyingi hazihitaji kufika mahakamani, wananchi wanakosa msaada wa sheria

Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan Shaaban akizungumza wakati akizindua Kampeni ya msaada wa Kisheria ya Mama Samia Pemba.
Muktasari:
- Kampeni hii ya miaka mitatu, ambayo inalenga kutoa msaada wa kisheria na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu haki zao, ilianza rasmi Machi 2023 na inatarajiwa kukamilika Februari 2026, ikitekelezwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya sheria.
Pemba. Jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar, Khamis Ramadhan Shaaban amesema kuwa sehemu kubwa ya kesi zinazofikishwa mahakamani, hasa zile zinazohusiana na migogoro ya ardhi, mirathi na ndoa, zinaweza kutatuliwa nje ya Mahakama endapo wananchi wangepata msaada wa kisheria kwa wakati.
Akizungumza Mei 8, 2025 katika hafla ya uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika eneo la Mwanamashingi, Chake Chake Pemba, Jaji Khamis amesema kampeni hiyo ya miaka mitatu itakuwa msaada mkubwa kwa wananchi na kwa Mahakama zenyewe, kwani itasaidia kupunguza mrundikano wa mashauri yasiyo ya lazima.
“Ukiangalia kwa undani, migogoro mingi ya ardhi ni midogo sana. Kuna kesi zinazoletwa kwa sababu ya mipaka iliyopishana kwa mita moja tu, haya ni mambo ambayo yanaweza kutatuliwa kirafiki bila kufika Mahakama ya Rufaa,” alisema Jaji Khamis.
Ameeleza kuwa kwa miaka mingi, Mahakama zimekuwa zikikabiliwa na mzigo mkubwa wa mashauri, mengi yakiwa ni yale ambayo yangeweza kumalizwa kwa maelewano au usuluhishi nje ya mfumo rasmi wa mahakama.
Jaji Khamis amesema kukosekana kwa elimu ya sheria kwa wananchi ndicho chanzo kikubwa cha hali hiyo.
Kampeni hiyo, iliyoanza Machi 2023 na inatarajiwa kukamilika Februari 2026, inalenga kuwafikia wananchi wote wa Tanzania Bara na Zanzibar kwa kutoa elimu ya sheria, msaada wa usuluhishi wa migogoro, pamoja na kuwaelekeza njia sahihi za kutafuta haki zao kisheria.
Jaji Khamis amebainisha kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kusogeza huduma za mahakama karibu na wananchi kwa kujenga mahakama katika ngazi za wilaya, ili kurahisisha upatikanaji wa haki kwa haraka.
Aidha, ameeleza kuwa Mahakama zimejipanga kutumia mifumo ya teknolojia kuharakisha huduma, ambapo wananchi wataweza kufungua mashauri kwa njia ya mtandao au kutumia simu zao za mkononi. Hili, amesema, litapunguza muda wa usubiri wa mashauri na kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jumanne Abdallah Sagini, amesema kampeni hiyo ni mkombozi mkubwa kwa wanyonge, hasa wale wasio na uwezo wa kumudu gharama za mawakili na uendeshaji wa mashauri.
“Kampeni hii imesaidia sana kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi, kwa kuwa inatoa njia mbadala za kutatua migogoro, ikiwemo ya ardhi, ndoa na mirathi, bila kufika mahakamani,” alisema Sagini.
Ameongeza kuwa Zanzibar ni miongoni mwa maeneo yanayohitaji msaada wa kisheria kwa kiwango kikubwa kutokana na wananchi wengi kutokuwa na utamaduni wa kutafuta haki kupitia vyombo vya sheria, jambo linalochangia baadhi yao kunyimwa haki zao.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora wa Zanzibar, Haroun Ali Suleiman, amesema kuwa Serikali ya Zanzibar kupitia wizara yake imekuwa ikitekeleza juhudi mbalimbali za kuwafikia wananchi mijini na vijijini kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu sheria na haki zao.
“Tunataka kuona wananchi wa Zanzibar wanakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu namna ya kutafuta haki kwa njia halali, na si kwa kupitia nguvu au migogoro isiyoisha. Elimu ya sheria ni msingi wa jamii yenye haki na utulivu,” alisema Waziri Haroun.
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali, Mahakama, wadau wa sheria na asasi za kiraia, ikiwa na lengo la kufikisha elimu ya sheria kwa kila Mtanzania, na kusaidia kujenga jamii inayotambua haki na wajibu wake kwa mujibu wa sheria.