Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mahakama Kuu Zanzibar yafuta kifungu kinachodhibiti uagizaji vileo

Muktasari:

  •  Sheria ya Udhibiti Vileo iliyotungwa mwaka 2020 imeweka ukomo wa kampuni zinazoruhusiwa kuagiza vileo Zanzibar kuwa tatu, lakini Mahakama Kuu imesema  kifungu hicho kinakinzana na Katiba.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Zanzibar imebatilisha kifungu cha 33(1) cha Sheria ya Kudhibiti Vileo (LCA) ya mwaka 2020 kinachoweka ukomo wa kampuni zinazoruhusiwa kuagiza vileo ikisema kinakinzana na Katiba ya Zanzibar.

Uamuzi huo umetolewa na Jaji George Kazi katika hukumu ya kesi ya kikatiba iliyofunguliwa mahakamani hapo na kampuni ya Quality Meat and Beverage Supplies (QMB), dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Kampuni hiyo ilifungua kesi baada ya kunyimwa leseni ya uagizaji vileo kutokana na masharti ya kifungu hicho, yanayoweka ukomo wa kampuni tatu tu zinazoruhusiwa.

Katika kesi hiyo ya kikatiba namba 01 ya mwaka 2023, pamoja na mambo mengine kampuni hiyo ilikuwa ikiiomba Mahakama itamke masharti ya kifungu cha 33 (1)(a)(b)(c)(d), (2) na (3) cha Sheria ya Vileo Sheria namba 9 ya mwaka 2020 inakinzana na Katiba.

Pia iliomba mahakama izingatie kifungu cha 43(1) na (2)(a)(b)(c)(d)(e) cha Sheria ya Ushindani Sawa na Ulinzi Sawa kwa Mlaji (FCFCPA)  namba 5 ya mwaka 2018.

Katika maombi mbadala, kampuni hiyo iliiomba Mahakama ikiipendeza ielekeze wale wote walioathirika na masharti ya sheria hiyo, wapewe nafuu za kisheria kwa mamlaka yake kabla ya kutungwa au kufanyika kwa marekebisho katika Sheria ya Vileo kuweka masharti ya usawa.

Jaji Kazi katika hukumu aliyoitoa Aprili 4, 2024 baada ya kusikiliza hoja za pande zote amekubaliana na hoja za kampuni hiyo na kuamua kuwa kifungu hicho cha Sheria ya Vileo hakipaswi kutumika na ni batili kisheria, hivyo hakitekelezeki.

“Ni mtazamo wangu kwamba, kifungu cha 33(1), kinaweka ubaguzi dhidi ya wale wanaotaka kuingia soko la uagizaji wa vileo, na si haki kuweka ukomo wa fursa kwa kampuni tatu tu,” amesema Jaji Kazi katika hukumu.

Kwa uamuzi huo, Mahakama pia imeamuru Bodi ya Udhibiti Uagizaji Vileo Zanzibar (ZLCB), kuipa QMB leseni ya uagizaji vileo ambayo awali ilikuwa imenyimwa na kuirejeshea makontena yake yoyote yaliyokuwa yameshikiliwa na mapato ya mauzo yake.

Katika uchambuzi wa hoja kabla ya kufikia hitimisho hilo, Jaji Kazi amesema zuio la vibali vya uagizaji vileo linakiuka haki kadhaa za msingi zinazohifadhiwa katika Katiba ya Zanzibar, zikiwemo uhuru wa kuendesha biashara na haki ya kupata riziki.

Amebainisha, Katiba inalinda haki za wananchi kufanya biashara kwa ajili ya maisha yao na kwamba, Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Ushindani Sawa na Ulinzi Sawa kwa Mlaji inazuia ufanyaji biashara kwa namna ambayo inazuia ushindani au washindani wapya katika soko.

Hivyo, amehitimisha kuwa sheria yoyote inayokuwa na masharti yanayokinzana na Katiba na sheria hiyo ya ushindani si tu inakosa utekelezaji wa kisheria bali pia inakinzana na Ibara ya 10(d) ya Katiba ya Zanzibar.

Vilevile Jaji Kazi amehoji uhalali uliotolewa na Serikali kwa kizuizi hicho, akibainisha sheria hiyo haina kanuni zozote zinazoweka ukomo wa kiwango cha vileo.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, Serikali ilidai ilikuwa ni muhimu kudhibiti uagizaji wa vileo uliokithiri, lakini Jaji Kazi amesema Serikali imeshindwa kuwasilisha ushahidi kwa kuwa hapakuwa na ushahidi kuunga mkono madai hayo.

“Kuna uagizaji wa vileo uliokithiri Zanzibar unaozidi mahitaji ya soko? Sheria inaweka kizuizi chochote dhidi waagizaji watatu waliopewa leseni ya kuagiza vileo kuhusiana na kiwango cha vileo kinachotakiwa kuagizwa,” amesema.

Amesema Serikali haikuweza kuielezea Mahakama kuhusu maswali hayo.

Katika hoja zake, kampuni ilidai walikuwa wameagiza bidhaa kuepuka kuchelewa na kusababisha usumbufu kwa wateja, kabla ya leseni kuisha na kabla maombi yao ya kuihuisha kukataliwa.

Ilidai bidhaa hizo zilizuiwa baada ya kuwasili katika Bandari ya Zanzibar na kutangazwa kupigwa mnada.

Kampuni hiyo ilidai Sheria ya Udhibiti Uagizaji Vileo ni kandamizi, inayokiuka Katiba na inakinzana na Sheria ya Ushindani Sawa na Ulinzi kwa Mlaji.

Hata hiyo, inasubiriwa kuona iwapo Serikali itakata rufaa kupinga uamuzi huo au itatekeleza uamuzi wa Mahakama kwa kuifanyia marekebisho sheria kwa kuzingatia hoja zilizobainishwa kwenye uamuzi wa shauri hilo.